Na Ezekiel Kamwaga,
Angola
MWAMUZI
Nhleko Simanga Pritchard kutoka nchini Swaziland ambaye alichezesha mechi baina
ya Wekundu wa Msimbazi na Al Ahly Shandi ya Sudan mwaka jana, ndiye
atakayechezesha mechi ya kesho dhidi ya Libolo.Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana kutoka Chama cha Soka cha Angola leo asubuhi, mwamuzi huyo atasaidiwa na na wenzake Mkhabela Bhekisizwe, Mbingo Petros na Fabudze Mbongiseni ambão wote wanatoka Swaziland.
Kati ya hao, ni Nhleko na Petros pekee ambão ndiyo waliochezesha mechi ya Shandi ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa na Haruna Moshi (77), Patrick Mafisango ambaye sasa ni marehemu (88) na Emmanuel Okwi (90).
Wachezaji wote hao watatu waliofunga katika pambano hilo hawatacheza katika mechi ya Libolo kwa sababu tofauti. Mafisango alifariki kwa ajali siku mbili baada ya kurejea kutoka Sudan kwenye mechi ya marudiano ambako Simba ilitolewa.
Okwi amehamia katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na Boban ameshindwa kusafiri na timu kwenda Angola kwa sababu ya kushikwa na malaria kali.
Kamisaa wa pambano hilo lililopangwa kuanza majira ya saa tisa kamili kwa saa za hapa (sawa na saa 11 jioni kwa saa za Tanzania) anatarajiwa kuwa Mandla Mazibuko kutoka nchini Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment