TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UAMUZI
KUHUSU RUFANI DHIDI YA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU
MKOA WA MWANZA (MZFA), MKOA WA GEITA (GEREFA) NA KUHUSU MICHAKATO YA
UCHAGUZI YA VYAMA WANACHAMA WA TFF NA WANACHAMA WAO
OKTOBA 31, 2012
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni
za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 8(2), 10(6), 12(1) na 26(2) na
(3) katika kikao chake kilichofanyika Oktoba 30, 2012 ilijadili rufani
dhidi ya Kamati za Uchaguzi za MZFA na GEREFA na michakato ya uchaguzi
ya vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Mwanza, Rukwa, Chama cha Mpira
wa Miguu wa Wanawake (TWFA), Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu
Tanzania (TAFCA) na Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na kutoa
uamuzi kama ifuatavyo;
1. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)
(a) Rufani ya Ndg. Jackson Manji Songora: Kamati
ilijadili rufani iliyowasilishwa na Ndg. Jackson Manji Songora dhidi ya
Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF
kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kumpitisha Ndg. Jumbe
O. Magati kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MZFA, kwamba Kamati ya
Uchaguzi ya MZFA
ilikosea:
(i)Kupokea Statement of Results ya
Baraza la Mitihani Tanzania yenye jina la Fredrick J. Magati wakati
jina la mgombea alilojaza kwenye fomu ya maombi ya uongozi ni Jumbe O.
Magati.
(ii)Kumsaili Jumbe O. Magati kwa kuwa hakuwasilisha nakala halisi ya cheti cha elimu yake.
(iii)Kumpitisha
Ndg. Jumbe O. Magati kugombea uongozi na kuwa Ndg. Jumbe O. Magati hana
sifa zinazokidhi matakwa ya Katiba ya MZFA Ibara ya 29(2).
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ilipitia maelezo ya Mrufani na ilijiridhisha kuwa
rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Songora haikutanguliwa na
pingamizi mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, hivyo ilikosa sifa ya
kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Hata
hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1); Katiba ya MZFA Ibara
ya 47 na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 26(2), Kamati
ya Uchaguzi ya TFF, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba na kanuni za
uchaguzi, ilimuhoji Ndg. Magati kuhusu elimu yake na majina yaliyo
kwenye Statement of Results na fomu yake ya maombi ya uongozi.
Baada
ya kupitia vielelezo na maelezo yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu
majina ya Ndg. Jumbe O. Magati, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha
kuwa Jumbe O. Magati na Fredrick J. Magati ni mtu huyo huyo. Kamati ya
Uchaguzi imetupa rufani ya Ndg. Patrick Manji Songora.
2. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA)
(a) Rufani ya Ndg. Abdallah H. Hussein: Kamati
ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Abdallah H. Hussein
ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake
kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha
kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Geita. Kamati ilipitia vielelezo
vilivyowasilishwa mbele yake na Mrufani
na ilijiridhisha kuwa vielelezo hivyo vinakidhi kuthibitisha kuwa
mwombaji uongozi ni Mkazi wa Mkoa wa Geita. Kamati inakubaliana na
maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg. Abdallah H. Hussein kugombea
nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
(b) Rufani ya Ndg. Aziz Mwamcholi: Kamati
ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Aziz Mwamcholi
ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake
kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa GEREFA, kwa kigezo cha kushindwa
kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari. Kamati
ilipitia maelezo ya Ndg. Mwamcholi na ya Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA
na ikajiridhisha kuwa Ndg. Mwamcholi hakukidhi matakwa ya Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF, hususan Ibara ya 10(5). Kamati
imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA wa kutompitisha
Ndg. Mwamcholi kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa GEREFA. Kamati ya
Uchaguzi ya TFF imetupa rufani hiyo.
(c) Rufani ya Ndg. Kaliro Samson: Ndg.
Samson aliwasilisha rufani kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya
GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
TFF kwa kigezo cha kutowasilisha cheti cha kuhitimu elimu ya kidato cha
nne. Kamati ilipitia maelezo na vielelezo vya rufani ya
Ndg. Samson nay a Mrufaniwa na kujiridhisha kuwa nakala ya cheti cha
elimu ya kidato cha sita inakidhi matakwa ya Katiba ya GEREFA Ibara ya
29(2). Kamati inakubaliana na maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg.
Kaliro Samson kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
3. Mchakato wa Uchaguzi Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ilijadili mchakato wa uchaguzi wa MZFA ikiwa ni
pamoja na mchakato wa uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya
Ukerewe (UDFA), baada ya uchaguzi wa awali wa UDFA kuwa umefutwa na
Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kutokana na Kamati ya Uchaguzi ya UDFA
kutozingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Baada
ya maelezo ya kina ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na vielelezo
vilivyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa UDFA,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa Kanuni
na taratibu za uchaguzi uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya UDFA kwa
kutozingatia kikamilifu maagizo ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na hivyo
kusababisha mkanganyiko katika mchakato wa Uchaguzi ambao kwa wakati
mmoja ulikuwa na Kamati mbili za Uchaguzi kusimamia uchaguzi huo.
Mikanganyiko inayojionyesha dhahiri na kusababisha nafasi zote sita
zinazogombewa katika mchakato unaoendelea kuwa na mgombea mmoja mmoja tu
katika kila nafasi, imeufanya mchakato wa uchaguzi wa UDFA kupoteza
hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za Uchaguzi na misingi ya
demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa katika
Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka yake
ya kikatiba Ibara ya 49(1) ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF, Ibara ya 10(6) na 26(2) na (3) imeamua:
(i)Kuzifuta Kamati zote za Uchaguzi za UDFA zilizoteuliwa na Kamati ya Utendaji ya UDFA kabla ya baada ya mchakato wa uchaguzi wa sasa wa UDFA.
(ii)
Kuufuta Uchaguzi wa UDFA uliokuwa ufanyike Novemba 5, 2012. Mchakato wa
uchaguzi utaanza upya kwa tarehe zitakazopangwa na Kamati ya Uchaguzi
ya MZFA baada ya kupata maelekezo ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
(iii)
Kuiagiza Kamati ya Uchaguzi ya MZFA katika kutekeleza majukumu yake kwa
mujibu wa Ibara ya 6 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF
kutoiruhusu UDFA kushiriki Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa MZFA kwa kuwa
UDFA imeshindwa kuzingatia matakwa ya Katiba kuhusu ukomo wa mamlaka ya
Kamati ya Utendaji na kufanya uchaguzi kwa wakati muafaka unaozingatia
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
4. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA)
Kwa
kuzingatia changamoto za kuijenga TWFA ambayo bado ni change, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF imekubali ombi la TWFA la kusogeza mbele tarehe ya
uchaguzi kwa wiki mbili. Uchaguzi wa TWFA ngazi ya Taifa sasa utafanyika
Novemba 18, 2012.
5. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)
Uchaguzi wa viongozi wa FRAT utafanyika Novemba 17, 2012 kama ulivyopangwa.
6. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)
TFF
imesimamisha kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa RUREFA kutokana na
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya RUREFA kuendeleza malumbano kati yao
kuhusu uhalali wa uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA, uteuzi
ambao ulifanywa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA, Oktoba 18, 2012. Kwa
kuwa hali hii imetokea tena baada ya Kamati ya Utendaji ya RUREFA
kuwa imepewa fursa ya kikatiba kuteua Kamati ya Uchaguzi na ni
mwendelezo wa mgawanyiko ndani ya Kamati ya Utendaji ya RUREFA
unaoathiri mchakato wa uchaguzi wa chama hicho, Kamati ya Uchaguzi ya
TFF inatafakari hatua muafaka za kikatiba na kikanuni zitakazoondoa
ukwamishaji wa mchakato wa Uchaguzi wa RUREFA unaosababishwa na Kamati
ya Utendaji ya RUREFA. Uamuzi kuhusu mustakabali wa Uchaguzi wa RUREFA
utatolewa baada ya kikao
cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Novemba 6, 2012.
7. Mchakato wa Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na Chama cha Makocha (TAFCA)
Uamuzi
kuhusu mustakabali wa uchaguzi wa SPUTANZA na TAFCA utatolewa baada ya
vyama hivyo kuwasilisha taarifa za kina kuhusu michakato ya chaguzi za
wanachama wao katika ngazi ya mikoa, katika kikao cha Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kitakachofanyika Novemba 6, 2012.
Moses Kaluwa
Mjumbe- Kamati ya Uchaguzi TFF
No comments:
Post a Comment