RAIS wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu (TFF), Wallace Karia amesema maandalizi ya michuano ya Kombe la
Mataifa ya Afrika ya Wanawake (WAFCON) na michezo ya kalenda ya Fifa ni
miongoni mwa sababu za kuipeleka Twiga Stars kushiriki
michuano ya Kombe la Wanawake Tunisia.
Twiga Stars ilikuwa nchini Tunisia kuanzia Julai
9, mwaka huu ambako ilicheza michezo miwili mmoja dhidi ya Tunisia na kuifunga
mabao 5-0 na Botswana ambao walitoka suluhu.
Akizungumza baada ya wachezaji hao kuwasili
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam leo, Karia
alisema ushindi walioupata Twiga Stars kwenye mashindano ya Kombe la Tunisia
utawasaidia kufanya vizuri kwenye Wafcon itakayofanyika nchini Morocco mwakani.
"Mashindano hayo
yalikuwa ni maandalizi kuelekea mashindano ya Wafcon ambayo yatafanyika mwakani
kwani malengo yetu ni kuona timu inakwenda kushindana na si kushiriki,” alisema
Karia.
Rais huyo alisema
wameamua kuitumia kalenda ya Fifa ili benchi la ufundi lihakikishe linaunda
timu yenye ushindani katika mashindano hayo.
Naye Kocha Mkuu wa timu
hiyo, Bakari Shime alisema amefurahishwa na viwango vilivyooneshwa na wachezaji
wake katika mashindano hayo na kudai walikwenda kwa lengo la kutwaa kombe hilo.
Alisema kuelekea kwenye
mashindano ya Wafcon watakaa na kuzungumza na TFF kwa ajili ya kurekebisha
mapungufu yao na changamoto kuhakikisha wanakwenda kufanya vema nchini Morocco.
"Tumefurahishwa na
mafanikio haya na tumetumia kalenda ya Fifa kwa kucheza michezo mfululizo
itakayotusaidia kufanya vizuri kwenye Wafcon,” alisema Shime.
Nahodha wa timu hiyo,
Anastazia Katunzi alisema ushindi huo utawasaidia kuipeperusha vema bendera ya
Tanzania na kuwataka Watanzania waendelee kuwaamini kwa kuwa malengo yao ni
kufika mbali.
No comments:
Post a Comment