Peter Sarungi aliyetenguliwa TAFF |
Na Rahel Pallangyo
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT),limevunja uongozi wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu kwa watu wenye ulemavu Tanzania (TAFF) na kuteua wajumbe wa kamati ya
muda itakayosimamia shughuli za shirikisho kwa muda wa siku 90 tangu leo.
Uongozi wa TAFF waliondolewa madarakani ni Peter Sarungi (Rais) na Moses Mabula (Katibu Mkuu).
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha
Uhusiano na Mawasiliano inasema BMT imevunja uongozi
huo kwa mamlaka lililopewa na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49
pamoja na kanuni za Baraza la Michezo la Taifa na kanuni za usajili namba 442
za mwaka 1999.
“Kamati hiyo itaundwa na Vincent
Kaduma (Rais), Athuman Lubandame (Makamu wa Rais), Iddi Lulida (Katibu Mkuu), Robert Manyerere (Naibu Katibu Mkuu) na Leonard Liunda (Mweka Hazina),” ilisema taarifa hiyo.
Aidha katika
kipindi hiki cha siku 90, kamati teule inapaswa kuratibu marekebisho ya Katiba
ya Shirikisho, kuratibu usajili wa wanachama, kuratibu mchakato wa Uchaguzi
Mkuu, kusimamia shughuli zote za shirikisho katika kipindi chote cha uteuzi na
kuunda kamati nyingine ndogo za kuwawezesha kutekeleza vizuri majukumu yao.
Kuvunjwa kwa uongozi huo kumetokana na kukizana na makubaliano yao na
serikali
ambapo jana uongozi wa TAFF walizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
kuwa timu ya Taifa ya soka ya watu wenye ulemavu ‘Tembo Warriors’, iko kwenye
hatihati ya kwenda kushiriki mashindano ya African Para Games yanayotarajiwa
kufanyika kuanzia Septemba 3 hadi 12 jijini Luanda, Ghana kwa sababu hawana fedha
za kupeleka timu.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Said Yakubu alisema
walikubaliana na TAFF wasipeleke timu kwenye mashindano hayo badala yake
serikali itaanda timu kwa ajili ya mashindano ya Afrika (CAAF) ya kufuzu
fainali za dunia yatakayofanyika Novemba mwaka huu.
“Mashindano
haya tulikubaliana nao wasiende kwa kuwa kuna mashindano makubwa zaidi yanakuja
ambayo tungeanza na kambi kabisa. Wameshazungumza na Baraza la Michezo Tanzania
(BMT). Hiyo nyingine sasa sijajua wanatoa wapi,” alisema Yakubu.
Naye Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha alisema
serikali haijatoa pesa ya kambi kwa ajili ya timu hiyo hivyo haiwezi kugharamia
kupeleka timu ambayo haijaandaliwa kwenye mashindano.
“Tulikubaliana kwa vile kuna mashindano mawili mwaka huu
na yamefuatana katika kipindi kifupi sisi tutapeleka timu kwenye mashindano ya
Afrika ya kufuzu fainali za dunia, hivyo haya tulikubaliana hatutapeleka timu,”
alisema Neema.
No comments:
Post a Comment