Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, March 15, 2018

WAMBURA AFUNGIWA MAISHA KUJIHUSISHA NA SOKA


Image result for WAMBURA

KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia kujihulisisha na soka maisha Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, baada ya kumkuta na hatia katika tuhuma tatu zilizokuwa zinamkabili kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.

Wambura alifikishwa kwenye kamati ya maadili na sekretarieti ya TFF juzi kwa makosa ya kupokea fedha za TFF kwa malipo yasiyo halali, kugushi barua na kushusha hadhi ya taasisi hiyo hivyo pamoja na kufungiwa maisha kamati imeielekeza Sekretarieti, kwa kupitia kifungu cha 6(3) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, ilifikishe suala hili katika vyombo vya dola ili vifanye uchunguzi.

Katika suala hilo Kamati inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Ukaguzi kuwa waliokuwa viongozi wakuu wa TFF wakati malipo hayo yanafanyika, Jamal Malinzi (Rais) na Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) nao waunganishwe katika uchunguzi huo.
Kamati ya maadili ilikutana juzi na kusikiliza shauri hilo ambalo Wambura aliwakilishwa na wakili Emanuel Muganyizi kwani kisheria alikuwa na hiari ya kufika kutoa utetezi huo kwa njia ya mdomo, kutuma kwa maandishi, kuleta mashahidi au kutuma mwakilishi akiambatana na barua ya uwakilishi
Hukumu hiyo ilisomwa leo na Kaimu Ofisa habari wa TFF, Cliford Ndimbo kwa mamlaka ya kamati hiyo akiwa na Mwenyekiti Wakili Hamidu Mbwezeleni katika Ukumbi wa mikutano wa TFF

Baada ya kuelezwa mashtaka yanayomkabili mteja wake, Wakili Muga aliiomba Kamati kuwa mteja wake anaomba kupewa muda wa kupitia shauri hilo ili aandae utetezi, vielelezo, na mashahidi. Mara baada ya kutoa ombi hilo Kamati ilimruhusu asubiri ili ipitie kabla ya kufanya uamuzi. Baada ya majadiliano wajumbe walikubaliana kuwa suala hili si geni kwa Ndugu Wambura; hivyo siyo kweli kuwa hana ufahamu nalo. Pia moja ya vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Kamati ni utetezi wa maandishi wa Ndugu Wambura kuhusiana na suala hilo ulioandikwa 4/12/2017. Hivyo Kamati ilijiridhisha kuwa Ndugu Wambura anao ufahamu wa kutosha wa suala hilo na alikuwa na uwezo wa kufika mbele ya Kamati ili kutoa maelezo ya ziada.

Kamati ilimjulisha Wakili Muga kuhusiana na uamuzi huo na kumtaka aanze kujikita katika kujibu mashtaka yaliyowasilishwa mbele yake. Hata hivyo Wakili Muga hakutaka kufanya hivyo na badala yake aliomba apewe muda zaidi wa kuandaa utetezi, vielelezo, na mashahidi. Kamati ilimkumbusha Wakili Muga kuwa wito wake ulijieleza vizuri hivyo ilikuwa ni wajibu wake kumshauri mteja wake ipasavyo na kumsaidia katika kujibu mashtaka yaliyofikishwa mbele yake. Baada ya maelezo hayo Kamati ilimuuliza Wakili Muga kama yuko tayari kuendelea na shauri au vinginevyo na yeye akaridhia kuwa shauri liendelee.

Baada ya makubaliano hayo, Wakili Muga alipewa nafasi ya kujibu mashtaka matatu yanayomkabili mteja wake.

Shitaka la kwanza:
“Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”

Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Michael Richard Wambura alipokea malipo kutoka Chama cha Miguu Tanzania (FAT) na baadaye TFF ikiwa ni marejesho ya mkopo ambao FAT ilikopeswa dola la kimarekani $30,000 kutoka katika kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 2002. Mkataba wa deni hilo ulisainiwa na Ndugu Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT. Hata hivyo Kamati haikupata nyaraka wala kumbukumbu zozote zile zinazoonyesha kuwa Ndugu Wambura alipata idhini ya kukopa kiasi hicho cha fedha kutoka katika Kamati Tendaji ya FAT. Vilevile Kamati haikuona uthibitisho wa kiasi hicho kupokelewa kwenye akaunti za FAT zaidi ya Mkataba ambao ulisainiwa na Ndugu Wambura peke yake bila kuwa na shahidi mwingine kutoka FAT kinyume na taratibu za kawaida za mikataba. Vile vile Kamati imeshangaa ni taratibu gani zilitumika kwa taasisi kama FAT kuchukua mkopo mkubwa kama huo kwenye kwenye kampuni hiyo badala ya taasisi za fedha kama vile benki ambazo ndizo zinazojishughulisha na masuala hayo.

Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Wambura, kwa nyakati tofauti, alipokea jumla ya sh.84,000,000.00 kutoka FAT na baadaye TFF kama marejesho ya mkopo kwa niaba ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED. Hata hivyo Kamati haikupata uthibitisho wa kisheria kutoka kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED unaomuidhinisha Bw. Wambura kupokea malipo ya mkopo huo kwa niaba yake zaidi ya barua Kumb. Na. JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo. Hata hivyo barua hiyo, licha ya kuandikwa miaka 10 baada ya Bw. Wambura kuchukua nusu ya mkopo huo, haikuwahi kupokelewa TFF na wala haikidhi matakwa ya kisheria ambayo ni kuwa na Power of Attorney iliyosajiliwa kwa Msajili wa Hati na Nyaraka.
Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na Sekretarieti malipo ya mkopo huo yalifanyika kwa awamu ambapo mara ya kwanza Ndugu Wambura alilipwa $15,000 alizopokea tarehe 29/4/2004. Hata hivyo Kamati ilibaini mapungufu katika fomu hiyo kwani maombi ya kulipwa fedha hiyo yalitolewa na Ndugu Wambura na kuidhinishwa na yeye mwenyewe, kinyume na taratibu za fedha.

Malipo hayo ya mkopo hayakufanyika kwa kipindi cha miaka 10, chini ya Uongozi wa Ndugu Leodgar C. Tenga, mpaka alipoondoka madarakani na kuingia uongozi mpya chini ya Ndugu Jamal Malinzi ndipo yalipoanza kufanyika tena. Kamati inapata mashaka juu ya uhalali wa deni na malipo hayo kwani hakukuwa na madai wala malalamiko yoyote yaliyowasilishwa kudai au kukumbushia deni hilo kwa kipindi chote hicho. Katika hali ya kawaida siyo rahisi kulipa deni hilo bila kujiridhisha uhalali wake.

Shitaka la pili
Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”

Sekretarieti iliwasilisha nakala ya barua ya tarehe 21/6/2016 kutoka kwa Bibi Irene W. Maganga ambaye ni  mke wa mmiliki wa kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED, Marehemu Enock Maganga na mmoja wa wasimamizi wa mirathi ya marehemu walioteuliwa na Mahakama Kuu Dar es Salaam. Barua hiyo inakanusha kuwa kampuni hiyo haikuwahi kupokea malipo yoyote ya deni hilo. Hii inaonyesha kuwa Ndugu Wambura hakuwahi kupewa mamlaka ya kupokea fedha hizo na pia hakuwahi kuziwasilisha kwa wamiliki wa kampuni hiyo fedha alizopokea kutoka FAT na TFF. 
Kwa msingi huo hata uhalali wa barua Kumb. Na. JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo aliyoiwasilisha kuonyesha kuwa ameidhinishwa kupokea malipo hayo unatia shaka. Ndugu Wambura hajawahi kukanusha maelezo yaliyomo kwenye barua hiyo licha ya kupewa nafasi akiwa Makamu wa Rais wa TFF.

Shitaka la tatu:
“Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015)”

Kamati imejiridhisha bila shaka kuwa vitendo vya Ndugu Wambura vinashusha hadhi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF). Kitendo cha Ndugu Wambura kuiingiza FAT na baadaye TFF katika mkopo wa $30,000 bila kufuata taratibu zozote ni ukiukwaji mkubwa wa maadili. Vile vile kitendo hicho kimelipaka matope shirikisho hilo mbele ya umma kwani mambo aliyoyafanya hayaakisi ukubwa na umuhimu wa taasisi hiyo. Kwa nafasi yake ya Makamu wa Rais, Ndugu Wambura ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango, hivyo vitendo hivyo haviendani na hadhi na majukumu ya nafasi yake hiyo.


HUKUMU
Kosa la kwanza:
Kulingana na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, Ndugu Michael Richard Wambura, amefanya kosa la kifisadi ambalo adhabu zake ni;
  1. (i) faini isiyopungua shilingi 10,000,000.
(ii) kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5
  1. Kama suala ni zito na limekuwa likijirudia rudia, kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha.

Kosa la pili:
Kwa kosa la kughushi kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, kinatoa adhabu ya kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5.

Kosa la tatu:
Kwa kosa la kushusha hadhi ya Shirikisho ni kwenda kinyume na Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015). Hili ni kosa la kimaadili ambalo adhabu zake zinaenda sambamba na adhabu nyingine zinazotolewa na Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.

Baada ya kupitia shauri hili na kuridhika pasipo na shaka kuwa Ndugu Michael Richard Wambura ametenda makosa hayo yote, Kamati imemfungia Ndugu Michael Richard Wambura kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha. Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia uzito wa kosa lake kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.

Kwa kuwa suala hili linahusisha masuala ya rushwa, Kamati inaielekeza Sekretarieti, kwa kupitia kifungu cha 6(3) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, ilifikishe suala hili la Ndugu Michael Richard Wambura katika vyombo vya dola ili vifanye uchunguzi. Aidha Kamati inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Ukaguzi kuwa waliokuwa viongozi wakuu wa TFF wakati malipo hayo yanafanyika, Ndugu Jamal Malinzi (Rais) na Ndugu Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) nao waunganishwe katika uchunguzi huo.

HITIMISHO
Kamati haikupendezwa na taarifa zilizowasilishwa na Sekretarieti kuhusu juhudi zilizofanywa na vyombo mbalimbali kuizuia isifanye kazi yake kwa mujibu wa Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015) na Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013. Kamati inaviasa vyombo hivyo kutoingilia mambo ya mpira wa miguu, hasa vyombo vya kimaamuzi, kwani athari zake zinaweza kuwa kubwa kwa ustawi wa mpira wa miguu nchini.