MAMBO
yanazidi kunoga kuelekea mchakato wa mabadiliko ya klabu ya na sasa wale
wanaotaka kuwekeza kwenye klabu hiyo wajipange na mwisho wa kutuma maombi ya
kuimiliki Simba ni Oktoba 18 mwaka huu.
Hiyo maana
yake itakuwa ni siku kumi kabla ya Simba kuivaa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu
Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Jana
Mwenyekiti wa Kamati ya Zabuni ya Simba, Jaji mstaafu, Jaji Thomas Mihayo
alisema taarifa rasmi ya mwaliko wa kuchukua nyaraka utatangazwa katika
vyombo vya habari kwa muda wa siku 10.
“Wazabuni
wanatakiwa kujiandaa na kuwa na nyaraka muhimu na kufanya mashauriano
kabla ya kuwasilisha nia ya kushiriki mchakato wa kiuwekezaji ambao
utafungwa Oktoba 18,” alisema Jaji Mihayo.
Pia alisema
baadae itafuatiwa na uchambuzi wa mawasilisho yatakayopokelewa, ili kutambua wazabuni
watakaokuwa wamekidhi sifa na vigezo.
Pia Jaji
Mihayo alisema jopo la wathamini wenye sifa na uzoefu limeundwa, ili
kupitia maombi yote yatakayopokelewa, baada ya kukamilisha tathmini na
wazabuni watakaokuwa wamekidhi sifa na vigezo watapokea nyaraka za
zabuni kwa ajili ya kuendelea na hatua zinazofuata.
Alisema
kamati itaendelea kutoa taarifa kuhusu hatua zitakazofuata kadri
itakavyohitajika, ili kuhakikisha wanachama, mashabiki, wadau na taasisi
zenye mamlaka ya kimichezo na usimamizi zinapata fursa ya kufuatilia mchakato
huo.
Agosti 20, mwaka huu, wanachama 1,216 wa klabu ya Simba waliridhia mfumo
wa klabu yao kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC), Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Kaimu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Salim Abdallah
'Try Again' alisema asilimia 50 ya hisa zitauzwa kwa mwekezaji yeyote au wowote
watakaoungana wasiozidi watatu, kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu
hiyo.
Alisema mwekezaji anatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20, ili
kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu, wakati kwa kuanzia wanachama wote wa
Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa.
Alisema asilimia nyingine 40 zitawekwa kama mtaji wa klabu na zitauzwa
kwa wanachama baadaye, lakini wale wawekezaji walionunua asilimia 50 awali,
hawataruhusiwa kununua hata hisa moja kwenye asilimia 40 za mtaji.
No comments:
Post a Comment