Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, October 15, 2017

OKWI AIOKOA SIMBA DAKIKA ZA MAJERUHI IKILALA KWA MTIBWA SUGAR


EMMANUEL Okwi aliinusuru Simba na kipigo baada ya kuifungia bao la kusawazisha katika dakika za nyongeza na kuifanya timu hiyo kulazimisha sare ya 1-1 kutoka kwa Mtibwa Sugar.
Mtibwa Sugar walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 37 kupitia Stahimili Mbonde na kuifanya Simba kuhaha katika dakika zote zilizobaki ikisaka bao la kusawazisha.
Okwi alifunga bao lake hilo la saba na kuendelea kuongoza katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu, ambacho hupewa mchezaji aliyefunga mabao mengi.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda alifunga kwa mpira wa adhabu kubwa baada ya Erasto Nyoni kuvutwa na beki wa Mtibwa Sugar, Cassian Ponera na mwamuzi kutoa adhabu hiyo.
Kwa sare hiyo, Simba imerejea kileleni baada ya kufikisha pointi 12 sawa na Mtibwa Sugar, Azam na Yanga baada ya kila moja kushuka dimbani mara sita.
Kabla ya mchezo huo, Yanga ilikuwa kileleni baada ya juzi kuifunga Kagera Sugar mabao 2-1 na kuiondoa Simba kileleni katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 16.
Vikosi vilikuwa, Simba; Aishi Manula, Ally Shomari, Erasto Nyoni, Salim Mbonde/Juuko Murshid, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Said Ndemla, James Kotei, John Bocco, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima.
Mtibwa Sugar: Benedict Tinoco, Salum Kanoni, Issa Rashid Baba Ubaya, Dickson Daud, Cassian Ponera, Shaaban Nditi, Salum Kihimbwa/Henry Joseph, Mohamed Issa, Stahimil Mbonde/Kevin Sabato, Salum Khamis/Hassan Dilunga na Ally Makarani.

Nayo Tanzania Prisons imeshindwa kuifunga Stand United katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya baada ya kutoka suluhu.