Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, October 25, 2017

MAKONDA AMWAGA MIPIRA KIKAPU, KUKARABATI UWANJA WA NDANI

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametatua changamoto zilizokuwa zinakikabili Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), kwa kuwapa jenereta, mipira na mabati  huku akiwataka kuhakikisha wanafanya vizuri kitaifa na kimataifa.
Hiyo ni ahadi aliyowahi kuwaahidi baada ya kutembelea katika mashindano ya ligi ya mkoa na kuelezwa changamoto ya kukatika kwa umeme wakati mechi ikiendelea na mabati kuvuja maji mvua zikinyesha na kusababisha mchezo kusimama.
Akikabidhi vifaa hivyo jana Dar es Salaam Makonda alisema BD waliomba jenereta la KV 25 lakini ameamua kutoa la KV 35 litakalofanya kazi muda mrefu, lakini pia, waliomba  mabati 100 na kuamua kuwapa 150 na mipira 110 ili kusaidia kuendeleza mchezo huo.
Makonda alisema anataka kuona mchezo huo na mingine yote iliyoko katika mkoa wake kama netiboli, wavu na kuogelea inafanya vizuri ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Niliona namna mnavyotaabika nikaona niwatie moyo kwa kuwa kuna vijana wengi wanatamani kucheza mchezo huo wapate nafasi ya kushiriki, nategemea michezo yote Dar es Salaam itafanya vizuri pia,” alisema.
Pia, alisema ahadi yake ya kujenga viwanja vitatu vya mchezo huo ipo kama kawaida na muda wowote atasaini mkataba na wakandarasi kuanza mchakato wa ujenzi.
Pia, alitangaza neema katika mchezo wa kuogelea akiahidi kujenga bwawa moja la kisasa la kimataifa ili pia, mchezo huo ufanye vizuri zaidi.
Aliahidi kushirikiana na viongozi wa BD na wengine, kuhakikisha anatimiza ahadi zake huku pia, akiahidi kuunda Kamati maalumu itakayoshughulikia michezo yote ndani ya mkoa na kutatua changamoto zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BD, Okare Emesu alimuahidi mkuu huyo kuwa watahakikisha wanafanya vizuri na kuutangaza mkoa katika ngazi ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment