Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, August 5, 2017

YANGA YADHIHIRISHA NI BORA ZAIDI YA SINGIDA UNITEDGEORGE Lwandamina ameanza kuonesha ubora kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, baada ya Yanga kutoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa kirafiki, Singida, ndiyo walioutawala mchezo huo kwa asilimia kubwa na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko alikuwa wa kwanza kuifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya tano baada ya kupiga mpira wa faulo, ulikwenda moja kwa moja wavuni na dakika tatu baadaye, Dany Usengimana akaisawazishia Singida United bao akiunganisha kwa kichwa krosi ya Deusi Kaseke.
Mshambuliaji Mzimbabwe, Simbarashe ‘Simba’ Nhivi Sithole akaifungia bao la pili Singida katika dakika ya 23 akitumia tena makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga na kufanya matokeo kubaki hivyo hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Yanga iliwatoa baadhi ya wachezaji wake wenye majina makubwa kama akina Donald Ngoma, Nadir Haroub Cannavaro, Kelvin Yondan, Thaban Kamusoko na Beno Kakulani na kuendelea kupambana ili kusawazisha mabao hayo, lakini walikuwa ni Singida United walioonekana kucheza kwa kuelewana na kuwapoteza Yanga.
Mambo yalianza kuwabadilikia Singida dakika ya 83, baada ya Amissi Tambwe, kuisawazishia timu yake bao kwa mkwaju wa penalti baada ya kipa Said Lubawa kumuangusha kwenye eneo la hatari Mussa Abdallah.
Bao hilo lilionekana kuwazindua mashabiki wa Yanga, ambao kwa muda mrefu walionekana kutoridhishwa na kiwango kinachooneshwa na timu yao hususani baada ya kutoka kwa wachezaji wenye majina makubwa.
Dakika ya 90 Martin alimaliza mchezo kwa kuifungia Yanga bao la ushindi kufuatia shuti kali la mbali ambalo lilimshinda kipa wa Singida United na mpira kujaa wavuni.
Katika mchezo huo Singida United ilipoteza penalti mbili zilizotolewa na mwamuzi Martin Saanya,  huku Yanga ikiutumia vizuri mkwaju huo kupitia kwa Tambwe.
Kiujumla Yanga haikuonyesha kiwango kikubwa sana hasa wachezaji wageni ambao ndiyo macho ya wengi yalikuwa yakiwafuatilia.
Huo ni mchezo wa saba wa majaribio kwa Singida United bila kushinda bada ya hivi karibuni kufungwa na wenzao walipanda daraja wa Lipuli ya Iringa.
Wakati huohuo, Yanga imefanikiwa kuinasa saini ya beki wa kushoto wa Azam FC, Gadiel Michael baada ya viongozi wa timu hiyo kumalizana na timu hiyo.
Msemaji wa Azam FC, Jafari Idd Maganga, alisema wanamtakia kila la kheri kwenye maisha yake mapya akiwa na kikosi cha Yanga
Kikosi cha Yanga ; Beno Kakolanya/Youth Rostand, Juma Abdul, Hajji Mwinyi/Hassan Kessy, Kevin Yondan/Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Abdallah Hajji ‘Ninja’, Thabani Kamusoko, Pius Buswita/Emmanuel Martin, Raphael Daudi/Juma Mahadhi, Donald Ngoma/Amiss Tambwe, Ibrahim Hajib/Said Juma na Baruan Akilimali.

Singida United; Said Lubawa, Michael Rusheshagonga, Shafiq Batambuze, Elisha Muroiwa, Juma Kennedy, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Tafadzwa Kutinyu, Nhivi Simbarashe, Danny Usengimana na Kigi Makasi.