Ni msimu mpya
utakaotoa timu bingwa mpya itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa
na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), msimu wa 2019.
Itakumbukwa, msimu wa
CAF wa 2018, timu itakayoiwakilisha nchi ni Yanga ambayo ni Bingwa
wa msimu 2016/17 wakati michuano ya Kombe la Shirikisho, Tanzania
itawakilishwa na Simba.
TFF tunazitakia kila
la kheri timu zote zinazoshiriki ligi hii, tukiamini kwamba uadilifu utaongoza
mbele ya taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia mpira wa miguu hapa nchini na
kwingineko.
Kwa mechi za kesho
Jumamosi, Simba inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting katika mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Mbao watakuwa wageni wa
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mchezo mwingine
utakuwa ni kati ya Majimaji ya Songea itakayosafiri hadi Mbeya kucheza na Mbeya
City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo huku Njombe Mji ikiialika Tanzania
Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba huko Makambako.
Kadhalika Uwanja wa
Manungu ulioko Turiani, Mtibwa mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar itaikaribisha
Stand United ya Shinyanga kwenye mchezo mwingine wa VPL ilihali Azam atakuwa
mgeni wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mwadui watakuwa
wenyeji wa Singida United ya Singida kwenye Uwanja wa Mwadui huko Shinyanga na
Jumapili kutakuwa na Mchezo mmoja utakaokutanisha Yanga na Lipuli
kwenye Uwanja wa Uhuru.
No comments:
Post a Comment