Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, June 25, 2017

WANYAMA APEWA MTAA UBUNGO




SERIKALI ya wilaya ya Ubungo imempa heshima kiungo mshambuliaji wa Tottenham ya England na timu ya Taifa ya Kenya, Victor Wanyama kwa kuipa moja ya barabara za Ubungo jina lake.
Wanyama ambaye pia alikuwa mgeni wa heshima kwenye mchezo wa mashindano ya Ndondo kati ya FC Kauzu dhidi ya Faru Jeuri baada ya kuzindua alifurahi kutambuliwa na kupewa heshima nje ya nchi yake.
 “Ni kitu kizuri kwangu ina maana kubwa kwa sababu kutambuliwa nje ya nchi yako si rahisi sana, imenifundisha najua kila mtu anaponiangalia apata motisha na mambo yote ninayofanya yanaonekana, nawashukuru na nawaambia asante,” alisema Wanyama.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Jacob Boniface alisema zawadi walioamua kumpa Wanyama itafanya wachezaji kutoka mataifa mengine kuja Tanzania kutokana na wageni wanavyopokelewa.
“Sisi tunashukuru kama manispaa ya Ubungo tumepata hamasa kubwa ya michezo ambayo inafanyika kwenye maeneo ya Halmashauri ya manispaa ya Ubungo na halmashauri ni mpya na watu wanavyofurika kuona nafarijika sana.”
“Tumefarijika na ujio wa Wanyama mchezaji kutoka timu ya Tottenham ya England na halmashauri ya Ubungo imempatia jina kwenye moja ya barabara zake ambazo zipo katika eneo hili kwa hiyo wanamichezo wote watakaokuwa wanakuja watakuwa wanaona jina la Victor Wanyama,” alisema Jacob
Baada ya kuzindua barabara hiyo Wanyama alikwenda kuangalia mchezo kati ya Kauzu na Faru jeuri kwenye Uwanja wa Kinesi, Unbungo ambapo Farujeuri ilishinda kwa bao 1-0.          
Baada ya kusalimiana na wachezaji alizungumza na wachezaji na kusema yeye amewahi kucheza ndondo akiwa Kenya ambapo kwao wanaiita ‘Kothbiro’ ikiwa na maana ya msimu wa mvua.
“Kwetu pia kuna ndondo sisi tunaiita ‘Kothbiro’ nikiwa na timu yangu ya mtaani inayoitwa Ziwani na Kothbiro manaa yake ni msimu wa mvua, wanaocheza ni wachezaji wa mitaani na wachezaji wanaocheza ligi kuu wanachanganyika pamoja,”
“Kothbiro ina nafasi kubwa Kenya kwa sababu imetoa wachezaji wakubwa na inasaidia timu za ligi kupata wachezaji kwa sababu makocha mbalimbali wa ligi huwa wanahudhuria kuangalia vipaji,” alisema Wanyama.
Wanyama alisema anatarajia kushuhudia mechi kali yenye ushindani kwa sababu ameambiwa timu hizo zilishawahi kukutana kwenye fainali ya michuano hiyo.
Wanyama azungumzia jezi namba 67
Victor Wanyama alisema alivyosajiliwa Celtic ya Scotland alichagua kuvaa jezi namba 67 ambayo ni namba kubwa, lakini alifanya hivyo makusudi na haikuwa bahati mbaya.
Wanyama alisema sababu kubwa iliyomfanya aache namba nyingine zote na kuchagua namba 67 ambayo kiuhalisia ipo mbali sana alisema alifanya uchunguzi na kugundua Celtic ilishinda Champions League mwaka 1967.
“Kila mchezaji ana ndoto, kwa hiyo nilivyokwenda pale nilikuwa na ndoto na nilikuwa najua Celtic ni timu ambayo inashiriki Champions League hivyo nilikuwa na ndoto siku moja niweze kushinda ubingwa wa Champions kitu ambacho bado sijafanikiwa lakini bado nina ndoto.”
“Nilifanya uchunguzi wangu nikagundua Celtic walishinda Champions League mwaka 1967 ndio maana nikamua kuvaa namba 67 ili iwe kumbukumbu kwangu nikiingia ndani nakumbuka mwaka wa mafanikio.”
Alipohamia Southampton Wanyama amekuwa akivaa jezi namba 12 hadi sasa Totenham anavaa jezi yenye namba 12 sambamba na akiwa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.
Pia Wanyama amezitaja sababu ambazo zinazosababisha wachezaji wa Afrika Mashariki kushindwa kutoka kwenda kucheza nje ya Afrika kuwa ni kuridhika mapema na kukata tama
 “Wachezaji wa huku tunakata tamaa mapema na kuridhika haraka, kwa sababu unakuta mchezaji lengo lake ni kwenda kucheza Mali akifika pale anatosheka badala kujituma ili afike mbali zaidi hata mimi kuna wakati nilikaribia kukata tamaa lakini nilipambana kwa sababu nilikuwa nikijua kuna wakati utafika mambo yatakaa sawa,”
“Kuchelewa kuoneshwa kwa ligi zetu kumechangia wachezaji wengi wa ukanda wa Afrika Mashariki kuchelewa kutoka kwenda nje ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika hasa Afrika Magharibi,” alisema Wanyama.
Wanyama alisema akiwa Ubelgiji kuna wakati mambo yalikuwa magumu kwa sababu alienda kule kabla hajafikisha miaka 18 kwa hiyo hakuweza kucheza moja kwa moja bali aliishia kufanya mazoezi akawa anawapigia simu nyumbani kutaka kurudi lakini walimzuia kwa kuniambia kama ana nyumba arudi lakini kama hana aendelee kukaa hukohuko.
Anasema anamshukuru ndugu yake Mariga kwani alimshauri asirudi ndipo akaamua kupambana akaendelea kukaa.

No comments:

Post a Comment