GRANIT Xhaka hatamaye sasa anaonekana
kama mchezaji mwenye thamani ya pauni milioni 30 ambayo kocha wa Arsenal Arsene
Wenger alitumia kumsajili nyota huyo wakati wa majira ya kiangazi akitokea Borussia
Monchengladbach .
Xhaka tangua ameanza kucheza na
kiungo wa kimataifa wa Wales Aaron Ramsey katika eneo la kiungo cha Arsenal
wameonekana kuunda ushirikiano mzuri na sasa anaonekana kuendana na dau la
pauni milioni 30 lililotumika kumtwaa.
Wakati Arsene Wenger alipomuelezea
Granit Xhaka kama aina ya mchezaji mwenye uwezo wa kucheza kama kiungo cha
chini na cha juu mwanzoni mwa msimu inawezekana hakuna mtu aliyechanganywa na
kauli hiyo ya profesa zaidi ya Xhaka mwenyewe.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23
sio mtu mwenye uwezo wa kujitengenezea nafasi na kuwatoka mabeki, huku tamko
hilo la Wenger likionekana kama la majaribio zaidi ingawa kwa sasa hakuna
mwenye shaka tena kama kiungo huyo wa kimataifa wa Uswisi anauwezo mkubwa wa
kwenda mbele kushambulia lakini wakati huo huo kutekeleza majukumu yake kama
kiungo mkabaji na ndicho kinachotokea kwa Arsenal kwa sasa.
Miezo miwili baadae, Wenger aliikana
kauli yake ya kuwa Xhaka ni aina ya kiungo mwenye uwezo wa kucheza sehemu ya
ulinzi na kiungo cha ushambuliaji kwa kusema kuwa ni aina ya kiungo mpiga pasi
zaidi kuliko uwezo wa kuwatoka mabeki na kutengeneza nafasi.
“Granit ni aina ya kiungo
kinachofanya shughuli zake kuanzia eneo la chini ya uwanja kuliko kukaba na
kwenda mbele kushambulia ,” alisema Wenger.
“Haonekani kwenye eneo la mwisho la
maadui mara nyingi. Ni aina ya mchezaji mwenye pasi za uhakika kupitisha
katikati ya wapinzani.“Anapata mpira kutoka kwa mabeki na kuwatafuta viungo wa
juu kwa pasi ndefu. Faida yake ni uwezo wa kile tunachokiita pasi za
wastani-pasi zinazotoka kwa kiungo wa chini kwenda kwa viungo wa juu.”
Huku msimu ukielekea ukingoni sasa
tunaanza kumuona Xhaka kwenye majukumu aliyoyatumikia kwenye maisha yake yote
ya soka.
Kiungo huyu wa kimataifa wa Uswisi
ni aina ya mchezaji anayefanya mambo yatokee kwa pasi zake za uhakika na maono
kwenye pasi zake maana yake ni hadhina kubwa kwa Arsenal zaidi ya hasa akipata
muda na nafasi katika eneo la katikati.
Kwenye mechi za karibuni zimeonyesha
faida ya kuwatumia Aaron Ramsey na Xhaka kwani hiyo inampa uhuru zaidi kiungo
huyo wa zamani wa Borussia Monchengladbach kuuona mchezo toka eneo la chini.
Ushirikiano mzuri wa Ramsey na Xhaka
ulionekana wazi dhidi ya Southmpton ambapo viungo hao wawili kwa ujumla wao
waligusa mpira mara 154 sawa na asilimia 89.5 ya pasi za uhakika kwenye mechi
hiyo huku wakichukua mpira toka kwa wapinzani mara 14-walipiga pasi nyingi
zaidi, walizunguka eneo kubwa zaidi lakini pia waligusa mpira mara nyingi
zaidi.
Haitaonekana kama inakuzwa sana
ikisemwa Ramsey anakimbia zaidi na Xhaka ni kama mafuta kwenye injini ya kiungo
huyo wa kimataifa wa Wales.
“Tunazoeana mechi hadi mechi na kwa sasa
inaonekana kuzaa matunda, hasa katika ulinzi inaonekana imara sana,” alisema Wenger
akisifu mabadiliko ya mfumo kwenye timu yake.
“Lakini kitu muhimu zaidi kwenye mfumo huu ni
kwamba unaendana na ubora wa wachezaji. Ramsey ni mzuri sana kujilinda nyuma
yake na ana uhuru zaidi kwenda mbele na kuingia eneo la penalty.
“Akiwa katika ubora wake kimwili,
anakuwa injini kubwa. Ana makadirio mazuri kwenye kukimbia kwake, anapokuwa
sawa kimwili anatumia faida ya mbinu alizokuwa nazo kwenye mchezo wake.“
TXhaka-Ramsey wamecheza dakika 783 pamoja
msimu huu na katika kipindi hicho Arsenal imefunga mabao 22 na kuruhusu mabao
manane. Mabadiliko ya kimfumo ya Wenger yanamuwezesha Ramsey kuwa na
nafasi ya kutosha kwenda mbele na kushuka chini na kasi yake kwenye eneo la
mwisho la maadui ni marejeo ya kiwango alichoonyesha kwenye fainali za Mataifa
ya Ulaya mwaka 2016 akiwa na timu ya taia ya Wales.
Ni muhimu ushirikiano huu wa eneo la
kiungo Arsenal ukaendelea hadi msimu ujao kama tulivyoona miaka iliyopita jinsi
gani ilivyo muhimu kwa eneo la kiungo kutawala mchezo.
Majeruhi ya Santi Cazorla yamemfanya
Ramsey kutumia nafasi yake vizuri kucheza sambamba na Xhaka katika eneo la
kiungo na ushirikiano wao unaonekana kuimarika mechi hadi mechi.
Hatimae Arsenal imepata ushirikiano
mzuri waliousubiri kwa muda mrefu katika eneo la kiungo na wale ambao walisema
Xhaka haendani na aina ya uchezaji wa Arsenal watakula maneno yao. Kiasi cha
pauni milioni 30 kilichotumika kumsajili kiungo wa umri wa miaka 23 ambae
anaanza kuimarika sio fedha nyingi kabisa.
No comments:
Post a Comment