Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, May 14, 2017

VITUKO VINAVYOACHA WATU HOI UWANJANIKUNA vitu ambayo hungetarajia kwa kawaida vitokee uwanjani; si ndani
ya dimba tu, bali hata kwenye benchi au kwenye ile njia ya wachezaji
kuingia uwanjani.
Hizo ni sehemu ambazo inatarajiwa kwamba kila mchezaji anakuwa makini,
ama akitafakari jinsi ya kufanya mambo akiingia uwanjani,
akibadilishana mawazo haraka na mwenzake, au akicheza hasa dimbani.
Si kawaida wachezaji kabla ya kuingia waanze kuzungumza na wa timu
pinzani, maana wanavuruga maandalizi waliyoweka na kumbukumbu za
waliyoambiwa na kocha au kuambizana wenyewe.
Hata hivyo, wapo waliopata kusema, japo si sawa, sheria na kanuni
ziliwekwa ili zivunjwe, ndiyo maana zikaambatana na adhabu juu yake.
Benchi ni la kazi gani? Ni eneo ambalo makocha hukaa wakifuatilia
mchezo na kupanga mbinu tofauti za kupata ushindi – kuzuia kufungwa na
kujaribu kufunga.
Wengine hawapendi kukaa, huona benchi moto hivyo muda mwingi huwa
wamesimama mbele yake kidogo wakienda kulia na kushoto kidogo pia
maana kuna mpaka.
Lakini pia ni eneo ambalo wachezaji wa akiba hukaa, wakifuatilia
wenzao wanavyopigania timu, wakiwa tayari pia kuingizwa uwanjani
wakati wowote wakihitajika, ili wakatengeneze mabadiliko kwa timu.
Si sehemu ambayo ungetarajia watu wawe wanakula maandazi, pipi au
biskuti. Lakini kwenye mechi ya Jumapili iliyopita baina ya Arsenal na
Manchester United katika dimba la Emirates, kulikuwa na kitu.
Kando ya wachezaji wa Arsenal waliokuwa wamekaa wakifuatisha mpira,
kulionekana kasha tupu la biskuti, ikimaanisha walizila pale pale
wakati wenzao wakihaha kumpatia Arsene Wenger ushindi wa kwanza dhidi
ya Jose Mourinho katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Mchambuzi wa masuala ya soka, Gary Neville hakufurahia jambo hilo,
akisema kwamba si busara kwenda na vyakula, hata kama ni ‘bites’ eneo
hilo, kwani kuna muda wake, kabla na baada ya mechi.
Wenger huenda hakuona, maana alikuwa makini kuwaongoza vijana wake
kwenye mafanikio. Hangeweza kufurahia kuona wachezaji wake wakiwa
pikniki wakati wenzao wakitokwa jasho na kuumia kwa ajili ya timu.
Aina ya biskuti zilizoliwa hapo zinaitwa ‘Malteser’, hivyo
wafuatishaji wa habari mtandaoni mara moja wakabatiza tukio hilo
‘Malteser-gate’, lakini kuna utetezi kwamba eti waliokula si wachezaji
wa akiba wa Arsenal, bali ni wafanyakazi wa uwanja au walinzi
waliokuwa wamezidiwa njaa. Kwa nini wadondoshe kasha pale lakini?
Waliokuwa benchi kwa Arsenal ni Gabriel Paulista, Olivier Giroud,
David Ospina, Theo Walcott, Alex Iwobi, Hector Bellerin na Francis
Coquelin. Nani alikula na nani hakula? Waseme wenyewe.
Lakini hii si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Arsenal kufanya lisilo
la kawaida, kwani golikipa wao, Wojciech Szczesny alipata kudakwa
akipiga pafu la sigara kwenye chumba cha kubadilishia nguo uwanjani.
Tangu Wenger awasili London Kaskazini zaidi ya muongo mmoja uliopita,
amekuwa akikataza vitu kama hivyo, japokuwa mwenyewe alikuwa na
kawaida ya kuvuta miaka iliyopita, akisema ilikuwa kabla madhara ya
kiafya ya uvutaji kutangazwa kwa kiasi kikubwa. Anasema enzi akicheza
kulikuwa na uvutaji, na hakuna mtu angekuambia usivute.
Lakini alipomdaka kipa wake namba moja wakati huo, Szczesny akivuta
sigara vyumbani, hakumlazia, bali alimbamiza faini ya pauni 20,000 kwa
kuliwasha kwenye vyumba vya kubadili nguo uwanjani St Mary’s, kwa
klabu ya Southampton mwaka 2015.
Tukondoka Arsenal tunakuta vitendo vya kivivu na visivyotakiwa benchi
kwa watu wengine – Diego Costa na Xabi Alonso, wachezaji wa Timu ya
Taifa ya Hispania – La Furia Roja.
Hawa wakiwa wamekaa benchi na kuelekea kuchoka wakati wa fainali za
Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, kitu kisichotakiwa, walianza
kuchezea mipira ya soksi kwakuivuta.
Walikuwa na wakati mgumu, wakiwa wameshajua wanaelekea nyumbani licha
ya kwamba walikuwa wamewadunga Australia 3-0.
Costa alianza kuishika soksi na kuchunguza uimara wa mipira (nyuzi)
yake, akamshirikisha Costa, na ukawa ndio mchezo wao pale, wakipoteza
kabisa ufuatiliaji wa mechi, hata kama wangeitwa kuingia hawangemaizi
haraka ni wapi palikuwa pamepwaya.
Costa angefanya nini tena katika hali ile ya mkato wa tamaa, na
mwenzake Alonso, wakijua hata wakiingia uwanjani mambo yangebaki vile
hata kama ni kufunga mabao 12. Walichachafukwa kwa  kupoteza nguvu
mechi zilizotangulia.
Siku si nyingi sana zilizopita, tuliona kituko, cha kipande cha mtu,
Wayne Shaw, akila pai kubwa kabisa uwanjani.
Ilikuwa ni kwenye mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA baina ya timu
yake ya Sutton na Arsenal, Shaw akaonekana akila ‘kwa bidii’ kwenye
‘dugout’.
Wenzake walikuwa wakihangaika kuwamudu Arsenal ambao walikuwa
wakiongoza, Shaw akiwa mchezaji wa akiba akaamua kula, na inasemwa
kulikuwa na dau limewekwa kwamba kwa jinsi alivyo na uchu, angekula
humo, kamera zikaelekezwa humo, akadakwa akila.
Ilimgharimu, kwani baada ya kusemwa sana kwenye vyombo vya habari,
aliangua kilio kabla ya kuamua kuachana na soka.
Golikipa huyo mwenye umri wa miaka 45 alieleza kusononeshwa na hali
hiyo, FA wakaanzisha uchunguzi, na Kocha wa Sutton, Paul Doswell,
akasema kilichotokea hakikuwafanya waonekane kama kweli ni wachezaji
wa kulipwa.
Vituko vya uwanjani haviwagusi wachezaji tu, bali na makocha
kadhalika, na sasa tunamwangalia Kocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani,
Joachim Low; hapa ni juu ya masuala ya afya.
Ni kocha mahiri aliyewapa Kombe la Dunia, mwenye mbinu nyingi, akili
na uwezo mkubwa wa kubadili mchezo, lakini kwenye afya anaacha maswali
mengi anapokuwa kwenye eneo lake la fundi.
Amekuwa akionekana kujikuna sana, kuitikisa pua yake na hata kupenga
makamasi kwa mkono mtupu na siku moja alimaliza kupenga hivyo akaenda
moja kwa moja kumshika mkono Cristiano Ronaldo wa Ureno.
Ilibidi aombe radhi baada ya kamera za paparazzi kumnasa akiwa
ameingiza mkono wake sehemu ya mbele, ndani, chini ya suruali na
alipouondoa mkono wake humo akawa anaunusa. Hiyo ilikuwa wakati wa
michuano ya Euro 2016 – mwaka jana tu.
“Niliona picha zile na kwa kweli wakati mwingine unajikuta tu umefanya
jambo bila kuwa umepanga. Ilitokea nami naomba radhi,” akasema Law.
Kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson, anajulikana kwa
ukali wake lakini pia hasira kumzidi kimo anapokuwa kwenye benchi la
ufundi au akiranda randa kwenye eneo lake la kujidai.
Na hivi ukiwa msaidizi wake, kama alivyokuwa Mike Phelan, kitu cha
mwisho ambacho ungependa kitokee ni kutenda jambo la kumkasirisha.
Phelan alijikuta matatani wakati wakiwa kwenye ‘gemu’ kubwa dhidi ya
mahasimu wao, Chelsea, ambapo akiwa kando yake, alipasua baluni,
aliyeshituka, akaruka, akamgeukia Phelan kabla ya kuanza kummiminia
maneno.
Yaani baluni dogo tu, lisilo na nguvu wala nini likaweza kumtia hofu
kubwa mmmoja wa makocha wakali zaidi kwenye ligi.
“Hilo ni tukio lililonifanya kuwa maarufu. Baluni lilikuja kichwani
mwangu, kwa hiyo nikalipiga lakini matokeo yake nusura nipoteze
kibarua changu, alinifokea na tangu hapo nikawa maarufu,” anasema
Phelan.
Marcelo Bielsa – raia wa Argentina – ni mmoja wa makocha waliojizolea
sifa kwenye soka. Akiwa na klabu ya Marseille, akifanya ‘doria’ kwenye
mstari wake uwanjani kama kawaida, alijondoa ghafla.
Akataka apumzike kidogo ajipange maana mechi ilikuwa imemchanganya.
Sasa mmoja wa watumishi wa Marseille alikuwa ameweka kahawa katika
vikombe vya karatasi na kuweka kwenye benchi; Bielsa akaikalia, na
ilikuwa moto, akaruka huku akigugumia kuungua.
Tumalizie na tukio la Jumapili iliyopita, ambapo wachezaji wa Arsenal
walionekana wakizungumza na kucheka na wale wa Man United kabla ya
mechi. Aliyezidisha ni Nacho Monreal, aliyesogea na kuwa na Andre
Herrera, akicheka na kufurahia, kana kwamba alikuwa kwenye sherehe ya
ubatizo.
Wenger anakiri alishangazwa na urafiki uliooneshwa na Arsenal dhidi ya
mahasimu wao, lakini akasema jambo jema ni kwamba hawakuathiriwa
mpangilio wao kwenye mechi.
“Nadhani naelewa kwamba wachambuzi wanashangazwa kidogo kwa sababu
miaka 10 au 15 iliyopita hapakuwa na kitu kama hiki, lakini kwa sasa
kwa ujumla ni kitu cha kimataifa. Real Madrid vs Barcelona ni hivi
pia, watu wanacheza pamoja kutoka nchi moja, ila nilishangaa,”
akahitimisha Wenger.