Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, May 30, 2017

TAIFA STARS YAPAA MISRI LEO, MAYANJA AJINASIBU KUIFUNGA LESOTHO

KOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Salum Mayanga  amesema amepata mbinu za wapinzani wao hivyo, wanakwenda kambini  Misri kwa tahadhari.
Mayanga na kikosi cha wachezaji 21 kimeondoka leo nchini Misri kwa kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa kufuzu kombe la mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Lesotho utakaochezwa Juni 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuelekea Misri Mayanga alisema watakuwa wanafanya mazoezi kwa  tahadhari wakijiandaa kiufundi na kimbinu kuwakabili wapinzani wao.
“Tumewaona Lesotho ni wazuri, wamekuwa wakishambulia kwa pamoja na kuzuia kwa pamoja. Pia ni timu inayojua kumiliki mpira,”alisema na kuongeza kuwa alifuatilia kupitia mechi zake za mwaka jana ambapo wanaonyesha kupata matokeo mazuri.
Alizungumzia sababu za kuchagua Misri kwa ajili ya kambi hiyo kwamba kuna hali ya hewa nzuri inayofanana na Dar es Salaam na vile vile, kuna miundombinu bora kwa ajili ya mazoezi.
Mayanga alitaja sababu za kuwaacha wachezaji wawili Mwinyi Haji na Aggrey Morris na nafasi zao kuchukuliwa na Gadiel Michael wa Azam na Nurdin Chona wa Tanzania Prisons ni kutokana na mkanganyiko wa sheria na kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya Zanzibar kujiunga kuwa mwanachama.
Alisema bado  kuna hofu kwa jamii juu ya wachezaji wa Zanzibar na Tanzania bara hivyo, ameona awaache kwanza  mpaka jamii itakapoelimishwa sheria na kanuni na nani anayehitaji kuchezeshwa.
Alisema Zanzibar itaanza kushiriki michuano ya CAF  mwaka 2022 hivyo, kwa sasa kuna wachezaji ambao walianza kucheza Taifa Stars wataendelea kuitumikia timu hiyo kama ambavyo sheria zinaelekeza. Lakini kwa wachezaji  pia, wanaweza kuchagua timu ipi wachezee.
Pia, alifafanua kuwa wachezaji ambao hawakuwahi kuitwa kuchezea Taifa Stars ndio ambao wanaweza kuichezea Zanzibar heroes.
Waliokwenda kambini ni makipa Aishi Manula  (Azam FC), Benno Kakolanya  (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar). Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael.
Walinzi wa kati Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) ilihali viungo wa kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na timu kwa sasa.
Viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla  (Simba SC) na Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga SC), Shiza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting).

No comments:

Post a Comment