SERIKALI imewahimiza wanawake viongozi wa michezo nchini
kuondokana na unyonge na kujiamini kwa uwezo wa kufikiri ili wapate
kuheshimika.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel wakati akifungua kongamano la
wanawake na michezo lililoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
“Nasikitika kuwaona akina mama
ni wanyonge. Msipojiamini hata muwe na mabilioni kiasi gani haisaidii. Mjiamini
kwa uwezo wa kufikiri,”alisema.
Pia, alizungumzia ubunifu
katika vyama au klabu wanazoziendesha ulenge kutoa michango yao kwa watu
wanaowaongoza na kujiepusha kuwa sehemu ya migogoro au matatizo.
Alisema yapo matatizo mengi yanaweza kutatuliwa kwa njia ya
michezo, kwa kuwa michezo ni umoja na hushirikisha watu wa matabaka mbalimbali
bila kujali itikadi zao za kisiasa wala dini.
Professa Gabriel alisema serikali iko pamoja nao hivyo,
wanachotakiwa kufanya wanawake hao ni kusimamia utakelezaji wa mambo
watakayoazimia.
Aliomba wadhamini mbalimbali kuwasaidia wanawake katika michezo
yao kwani wamekuwa wakiwakilisha vyema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa BMT Jennifer Shang’a alisema mwanamke ili aweze kuleta mabadiliko anatakiwa kujiamini
mwenyewe kwa kuhakikisha anakuwa ni Kocha mzuri kabla ya kuwafundisha wengine.
Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kutekeleza tamko la Brighton
linalotoa mwito kwa taasisi zote binafasi na serikali kushiriki katika maendeleo ya michezo.
No comments:
Post a Comment