TIMU ya soka ya
Taifa, Taifa Stars leo imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga Burundi
mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam.
Huo ni ushindi wa
pili kwa Stars katika mechi za kirafiki za kimataifa baada ya mwishoni mwa wiki
iliyopita kuifunga Botswana mabao 2-0.
Mabao ya Stars jana
yalifungwa moja kwa kila kipindi kupitia kwa wachezaji Simon Msuva na Mbaraka
Yusuf.
Msuva ndiye aliyeanza
kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 20 akiunganisha pasi ya Ibrahim Ajibu
na kuachia shuti lililomzidi mlinda mlango wa Burundi, Nahimana Jonathani.
Bao hilo liliiamsha
Burundi ambayo nayo ikaanza kufanya mashambulizi na dakika ya 31 nusura mshambuliaji
Laudit Mavugo aandike bao, lakini akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya hivyo
shuti lake lilipaa juu na kufanya Stars kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao
hilo.
Mavugo aliisawazishia
Burundi bao katika dakika ya 54 akitumia vema makosa ya kipa wa Stars,
Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyeacha lango ambapo Mrundi huyo alimwahi na
kuujaza mpira wavuni.
Bao hilo lilidumu kwa
dakika 24 tu kwani Yusuf aliiongezea Stars bao la pili katika dakika ya 78 akiunganisha pasi ya Ajib na kuachia shuti
ambalo liligonga mwamba na mpira kumrudia kabla ya kuuwahi na kuuweka kimiani.
Ushindi huo, Stars
imelipa kisasi kwa Burundi ambayo ilicheza nayo mwaka 2014 na kufungwa mechi
zote.
Kocha Mkuu wa Stars,
Salum Mayanga aliitumia mechi hiyo kuangalia kikosi kitakachocheza mechi za
kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan)
zinazotarajiwa kuchezwa baadaye mwaka huu.
No comments:
Post a Comment