USHINDI wa
bao 1-0 iliyoupata Simba leo katika Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu
umeiwezesha kuongeza pengo la pointi dhidi ya Yanga timu inayoshika nafasi ya
pili.
Simba kwa
ushindi huo imefikisha pointi 41 ikiendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo
ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 37.
Kabla ya
mechi za raundi ya 17 kuchezwa jana na leo, Simba na Yanga zilikuwa
zinatofautiana pointi mbili, lakini mambo yalianza kubadilika jana baada ya
Yanga kutoka sare ya bao 1-1 na African Lyon na kisha Simba leo kuibuka na
ushindi huo.
Ni wazi kuwa
pengo hilo la pointi litaongeza ushindani zaidi katika ligi hiyo, ambapo
Jumatano Yanga itacheza na Ndanda FC Uwanja wa Uhuru kisha siku inayofuata
Simba itacheza na Ruvu Shooting uwanja huohuo.
Katika
mchezo huo wa jana, bao hilo pekee lilifungwa dakika ya 45 na Muzamir Yassin
akiunganisha krosi ya Javier Bukungu.
Hata hivyo
bao hilo lilizua malalamiko kwa wachezaji wa JKT Ruvu, wakidai kipa wao, Hamis
Seif aliumia katika harakati za kuokoa mpira na alianguka chini, hivyo mwamuzi
Hans Mabena wa Tanga alipaswa kupuliza filimbi kwa kuwa wachezaji wa Simba
hawakutoa mpira nje kwa kufuata taratibu za Fair Play.
Lakini
badala yake wakati kipa huyo akiwa chini, Simba waliendelea kucheza na kufunga
bao hilo.
Hata hivyo
hatua ya kipa huyo kuanguka wakati Simba wakishambulia lango lake haikuwashtua
wengi kwa vile katika kipindi hicho cha kwanza alianguka zaidi ya mara tatu
akitibiwa na kuendelea na mchezo, hivyo hata tukio hilo ilionekana kama ni
utaratibu wake uleule.
Kipindi cha
kwanza JKT Ruvu walijaribu kufika langoni kwa Simba mara kadhaa, lakini
walikosa mbinu za kuipenya ngome ya Simba, huku wenzao wakifika mara nyingi
langoni lakini umaliziaji ulikuwa hafifu.
Wachezaji wa
Simba wakiongozwa na Shiza Kichuya, Muzamir na Pastory Athanas nao watajilaumu
kutokana na kushindwa kutumia nafasi walizopata kwa nyakati tofauti kufunga.
Kipindi cha
pili Simba iliendelea kupoteza nafasi nyingi za kufunga, huku JKT Ruvu
inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ikifanya mashambulizi ya
kushtukiza, lakini umaliziaji ulikuwa butu. JKT Ruvu ina pointi 13 na inashika
nafasi ya 15.
Nayo timu ya
Majimaji ya huko na Azam FC zimefungana bao 1-1 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Kutokana na
matokeo hayo Azam imefikisha pointi 27 ikiendelea kushika nafasi ya tatu nyuma
ya Yanga, huku Majimaji ikifikisha pointi 17 ikiwa nafasi ya 14 kati ya timu 16
zinazoshiriki ligi hiyo.
Azam ilikuwa
ya kwanza kupata bao dakika ya 17 mfungaji akiwa Yahya Mohammed kabla ya
Majimaji kusawazisha dakika ya 67 mfungaji akiwa Alex Kondo.
Matokeo
mengine, Mtibwa iliifunga Ndanda FC mabao 2-0 Uwanja wa Nang’wanda Sijaona, Mtwara.
Mbeya City na Toto Africans zilitoka 0-0, huku Kagera Sugar ikiifunga Stand
United bao 1-0 na Mwadui ikiifunga Mbao FC bao 1-0.
No comments:
Post a Comment