Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, October 22, 2016

MANJI ATII AMRI YA MAHAKAMA

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga Yusuph Manji amethibitisha kuwa mkutano wa dharura uliopangwa kufanyika kesho kwenye uwanja wa Kaunda hautakuwepo baada ya kupokea zuio rasmi la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Aliyekuwa Mwanasheria wa klabu hiyo Frank Chacha na Juma Magoma ndiyo waliopeleka kesi hiyo Mahakamani kutokana na madai ya kwamba mkutano huo umekiuka katiba ya Yanga ili kulinda maslahi mapana ya Wana Jangwani hao.

Manji amewaambia Waandishi wa Habari kuwa maandalizi yote ya mkutano huo yalikuwa yameshakamilika na baadhi ya wanachama kutoka sehemu mbali mbali nchini na nje ya nchi walishaanza safari kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo.

Manji alichukua nafasi hiyo kuwaomba radhi wanachama wa klabu hiyo ambao walishajiandaa kwa ajili ya mkutano huo ambao ungejadili masuala mbali mbali likiwemo la ukodishwaji lakini kutokana na zuio hilo la Mahakama Mkutano huo hautakuwepo ili kutovunja sheria za nchi.

"Nichukue nafasi hii kuwatangazia wanachama wa Yanga kuwa mkutano hautakuwepo kesho kutokana na zuio la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

" Niwaombe radhi wale waliotoka nje ya jiji la Dar es Salaam ambao wameingia gharama za kutaka kuja mkutanoni na pia kesho hatutaruhusu mkusanyiko wowote wa wanachama klabuni ili kutopinga zuio la Mahakama," alisema Manji.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa kuna mtu yupo nyuma ya Wanachama hao walioenda Mahakamani kwakua watu hao hawana uwezo wa kifedha wa kufanya hivyo huku wengi wakishindwa kulipa hata ada ya uanachama.

Aidha Manji amewataka wanachama wa Yanga kuendelea kuwa watulivu na wasikubali kuvurugwa kwa namna yoyote ili watetee ubingwa wao msimu huu na kwamba jambo hilo ndilo lipewe kipaumbele zaidi.