Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, May 30, 2016

VICTOR WANYAMA AIPA TANO TAIFA STARS



Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba mchezo ujao kati ya Mapharao wa Misri na Taifa Stars, utakuwa ni fainali ya kuamua taifa litakalofuzu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON hapo mwakani kutoka kundi G.
 Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo kati ya Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya Tanzania Mei 29, 2016, uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Mkwasa maarufu kama Master anasema kwa msimamo na hali ilivyo kwa sasa, “Najua Misri wanatufuatilia. Na hata Kenya kwa siku zote tatu walikuwako. Najua  Misri wanahitaji sare ili wafuzu kwa fainali hizi, lakini hawataipata Tanzania.”
Mkwasa anasema mchezo dhidi ya Misri, ana uhakika vijana wake watajitahidi ili kupata matokeo mazuri baada ya Jumapili kufanya vema dhidi ya Harambee Stars waliocheza mechi hiyo mbele ya mashabiki wao wachache ambao pia hawakuchangamka kama wale wa Tanzania ambao licha ya kuwa ugenini walichangamsha mji na uwanja.
Wakati Misri wana pointi saba, Taifa Stars ina pointi moja na hivyo wa kuibania au kupindua matokeo ya Misri isiende AFCON mwakani, basi ni Tanzania hasa kama itawafunga Mapharao Jumamosi kabla ya kwenda Nigeria Septemba, mwaka huu kucheza na Nigeria.
“Kama nilivyosema, Misri wanakuja wanahitaji pointi moja lakini sisi tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa leo unatosha kuona mapungufu (upungufu). Maana ilikuwa mechi ngumu iliuyojaa nyota wote wa Kenya ambao ni professionals, lakini mimi nilikuwa na local based players na matokeo yamekuwa hayo.
“Tilianza kufunga bao, lakini wakarudisha. Bora mchezo umeishia hivi maana najua Wakenya hawana uvumilivu, tungewafunga hapa sijui kama tungetoka salama,” amesema Mkwasa ambaye baadhi ya waandishi, hususani wale wa Kenya walianguka kicheko kuashiria kuwa kuna matatizo katika utawala wa soka.
Mkwasa anasema ana taarifa namna ambavyo Misri wanaifuatilia Taifa Star hususani ukusanyaji wa video kwa ajili ya kuona aina ya soka la Tanzania, huku akisema: “Hawatafanikiwa kwa sababu soccer is the game of different approach (Soka ni mchezo wenye mifumo tofauti). Hivyo tulivyocheza na Kenya sivyo nitakavyocheza na Misri, nitakuwa na approach yake.”
Anasema ushindi wa Jumamosi ijayo ni wa kuvuna pointi tatu ili kupata kasi ya kushinda mchezo dhidi ya Nigeria na kufungua ukurasa mpya wa Taifa Stars kutengeneza mazingira mazuri ya kuwashinda Nigeria katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi utakaofanyika Septemba, mwaka huu.
“Tunaomba Wakenya mtuombee. Nasi tunawaombea ili kama wote inatokea mwaka huu tunakosa mafasi, basi iwe kheri kwa kipindi kijacho. Sisi tumekuja kucheza kwenu katika mji wenu wenye baridi basi nanyi karibuni siku moja dar es Salaam, Tanzania katika mji wetu wetu wenye joto, huenda mkaambulia sare vile vile,” anasema.
Mkwasa alipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (FKF), kwa kuandaa mchezo huo angalau kwa asilimia 70 kwa kushirikiana na Tanzania iliyojazia gharama za juu sambamba vijana wake kwa kucheza kwa kujituma licha ya kuwakosa nyota wake wa kulipwa na hivyo kupata picha na mbinu sahihi za kuivaa Misri Jumamosi ijayo.
“Bado tunaendele kujenga timu yetu, wengi ni vijana kama mlivyoona na wengine ni mara ya kwanza wanacheza. Nimewapa nafasi na mmeona uwezo wao, bila shaka tutafanya vema maana wengine ni under 21 wako kwenye kikosi. Huko mbele tutakuwa na timu nzuri,” anasema Mkwasa akimtolea mfano Shiza Ramadhani ambaye alipewa nafasi kwa mara ya kanza katika kikosi cha kwanza akichukua winga ya kulia.
 VICTOR WANYAMA
“Kwa hiyo tayari tumeona kitu gani cha kuongeza,” anasema Mkwasa hoja yake iliyoungwa mkono na Nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama ambaye kwa dakika chache, alizungumza na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania na kuhoji: “Unasema leo hamkuwa na professional pale uwanjani?” alipohakikishiwa ukweli huo, akasema:
“Basi mna kikosi kizuri. Wengi ni vijana, wanaweza kama mkicheza kwa kutubana kama mlivyobana hapa, Misri mnaifunga na hata hao Nigeria, si ajabu nikasikia mnakwenda AFCON mwakani. Ninaitakia kila la kheri timu hii, nawatakiwa kila la kheri Watanzania katika harakati zao. Sisi mwaka huu tumepotea kabisa, hatuna matumaini tena, tunajipanga ndiyo maana nimekuja kutetea taifa langu, hata kama tumekosa nafasi,” alisema Wanyama anayekipiga Southampton ya England.
Katika mchezo huo, Taifa Stars iliwakosa nyota wake Mbwana Samatta anayechezea Genk ya Ubelgiji kwa kuwa alikuwa na mchezo muhimu wa kupa nafasi timu yake ama icheze Ligi ya Uropa au ibaki nje katika michezo ya kimataifa ngazi ya klabu Ulaya. Shirikisho la Soka Tanzania na Kocha Mkwasa walimruhusu kama ilivyo kwa Thomas Ulimwengu anayekipiga TP Mazembe waliokuwa na mchezo mkali dhidi ya AS Vita ambao wana utani na ushindani mkali wa soka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
 MWINYI KAZI MOTO
Naye Nahodha wa Taifa Stars katika mchezo huo, Mwinyi Kazimoto amesema kwamba mchezo dhidi ya Kenya, umeonesha picha ya kinachotakiwa kufanyika katika michezo ijayo inayoikabili timu hiyo baada ya kusifu maandalizi, mapokezi mazuri na sapoti nzuri kutoka kwa mashabiki wa Kitanzania, hasa wale waliosafiri umbali mrefu kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, Kenya kuishangilia Stars. Nahodha wa Taifa Stars ni Mbwana Samatta anayesaidiwa na John Bocco ambao katika mchezo huo, hawakucheza. Bocco ni Majeruhi.

 MCHEZO WA HARAMBEE STARS, TAIFA STARS
Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza mashabiki walishuhudia mabao 1-1 kwa kila upande na ndiyo yaliyokuwa matokeo ya mwisho katika dakika 90, lakini kipindi cha pili wadau wa soka walishuhudia mabadiliko ya kila timu kujaribu nyota wake kwa mujibu wa sheria na taratibu za Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA), linaloruhusu kubadili wachezaji hadi wachezaji sita. Lakini hakukuwa na mabadiliko ya matokeo.
Kuhusu mabao ni Elias Maguli ndiye aliyetangulia kuifungia Taifa Stars bao katika dakika ya 30 kwa kichwa baada ya kupokea krosi murua kutoka kwa Juma Abdul kutoka Mashariki ya Uwanja wa Moi Kasarani kabla ya dakika saba baadaye kumfanyia madhambi Winga Ayub Masika ndani ya eneo la hatari hivyo Mwamuzi, Brian Nsubuga kutoka Uganda, kuamuru penalti iliyokwamishwa wavuni na Victor Wanyama.
Katika mchezo huo ambao wakati wote ulikuwa ni wa kushambuliana kwa timu zote mbili, Taifa Stars iliwapumzisha kipa Deogratius Munishi na nafasi yake ikachukuliwa na Aishi Manula na kwa wakati mmoja kuwatoa Jonas Mkude na Shiza Ramadhani na nafasi zao kuchukuliwa na Farid Mussa na Mohammed Ibrahim baadaye Kocha Mkwasa alimwingiza Jeremiah Juma kuchukua nafasi ya Maguli.


Kenya wao waliwatoa Humphrey Ochieng kwa kuingia Cliford Miheso; akatolewa tena Jesse Were kwa Wyclif Ochomo; Ayub Masika akapumzishwa na John Makwata akapewa nafasi kama alivyopumzishwa Anthony Agay na nafasi yake kuchukuliwa na Mayeko Mohammed. Pamoja na mabadiliko hayo, matokeo yalibaki vilevile 1-1 hadi dakika ya 90 katika mchezo ambao Wanyama alipewa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Kazimoto.

VIKOSI VYA TIMU ZOTE
Vikosi vya kwanza katika mchezo, Kenya: 1. Boniface Oluoch, 9. Joakins Otieno Atudo, 5. Abud Omar Khamis, 12. Eugene Ambuchi Asike, 8. David Owino Odhiambo, 14. Anthony Akumu Agay, 15. Victor Mugubi Wanyama, 23. Ayub Timbe Masika, 19. Humphrey Mieno Ochieng’ 16. Eric Johanna Omondi, 29. Jesse Jackson Were
Wachezaji wa akiba: 3. David Okello Abongo, 10. Eric Ouma Otieno, 6. Mayeko Musa Mohammed, 24. Victor Ali Abondo, 27, Wycliff Okello Ochomo, 20. John Mark Makwata, 21. Clifford Miheso Ayisi
 Tanzania XI: 1. Deo Munishi, 6. Juma Abdul Jafari, 2. Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, 13. Aggrey Morris, 15. Erasto Edward Nyoni, 17. Jonas Gellard Mkude, 7. Himid Mao Mkami, 16. Shiza Ramadhan Yahya, 12. Mwinyi Kazimoto Mwitula, 10. Elias Mrugao Maguli, 4. Deus David Kaseke
Wachezaji wa akiba walikuwa: 18. Aishi Salum Manula, 5. David John Mwantika, 9. Farid Mussa Shah,  11. Jeremiah Juma Ally, 8. Abrahim Hajibu Migomba, 3. Mwinyi Haji Mngwali, 14. Mohammed Ally Ibrahim
 WAAMUZI
Brian Nsubuga (Mwamuzi wa kati), Hussein Bugembe (Msaidizi wa Kwanza), Ronald Katenya (Msaidizi wa Pili), Amir Abdi Hassan (Kamishna wa mchezo) and  Davies Omweno (Mwamuzi wa Akiba, Mezani.)

No comments:

Post a Comment