Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, March 5, 2016

YANGA NA AZAM ZATOSHANA NGUVU TAIFA


BAO la kusawazisha la Azam lililofungwa na John Bocco leo, limefanya Yanga na Azam kumaliza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kukiwa hakuna mbabe kati yao baada ya kufungana mabao 2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo katika ligi hiyo Oktoba mwaka jana katika uwanja huohuo, zilitoka sare ya bao 1-1 na jana ulikuwa wa marudiano katika raundi ya 21 ya ligi hiyo, huku zenyewe ikiwa ni raundi ya 20.
Mechi 15 zilizopita baina ya timu hizo katika ligi zimeshindwa kumtoa ‘mbabe,’ kila timu imefanikiwa kushinda mara 5 na michezo mingine mitano ikimalizika kwa matokeo ya sare.
Timu hizo zilikutana katika robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame Julai mwaka jana, ambapo hadi muda wa kawaida unamalizika matokeo yalikuwa 0-0, Yanga wakapoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti na kuondolewa katika michuano ambayo Azam FC walitwaa ubingwa.
Zikakutana tena katika mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba, 2015 na kwa mara nyingine tena dakika 90 zilimalizika kwa matokeo ya 0-0, safari hii Yanga walishinda katika mikwaju ya penalti.
Baada ya sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu Desemba mwaka jana, timu hizo zilikutana tena Januari mwaka huu katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi  Zanzibar na zilifungana bao 1-1.
Kutokana  na matokeo ya jana, Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 47 sawa na Azam, lakini Yanga ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba yenyewe inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45 ikicheza michezo 20 sawa na Yanga, ambapo leo Simba itashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kucheza na Mbeya City.

Kama Simba itashinda mchezo wa leo itafikisha pointi 48 na kushika usukani wa ligi, ingawa itakuwa mbele mchezo mmoja ukilinganisha na Azam na Yanga.

Katika mchezo wa jana, Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 11 baada ya beki Juma Abdul kujifunga katika harakati za kuokoa.

Bao hilo lilionekana kumchanganga beki huyo na dakika ya 28 Juma Abdul alisahihisha makosa yake kwa kuifungia Yanga bao la kusawazisha kwa shuti kali nje ya eneo la 18 kutokana na pasi ya Donald Ngoma.

Yanga iliendelea kulisakama lango la wapinzani wao na dakika ya 41 ilipata bao la pili mfungaji akiwa  Ngoma, kutokana na krosi ya Amis Tambwe.

Washambuliaji wa timu zote waliendelea kufika katika maeneo ya hatari, lakini tatizo la umaliziaji lilikuwa likiwaathiri.

Dakika ya 70, John Bocco alifunga bao la kusawazisha baada ya kupokea pasi ya Kipre Tchetche, bao ambalo liliwanyanyua vitini mashabiki wa Simba timu yenye utani wa jadi na Yanga na kuanza kushangilia.

Mashabiki hao wa Simba walikuwa wakishangilia wakiamini ni fursa nzuri kwa timu yao kukaa kileleni kama itaifunga Mbeya City.

Hata hivyo, mchezo wa Mbeya City utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na mazingira ya timu zote mbili katika msimamo huku Mbeya City ikiwa nafasi ya 10 katika msimamo kutokana na pointi zake 21.

Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva/Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Pato Ngonyani, Donald Ngoma na Deus Kaseke.
Azam FC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, David Mwantika, Said Mourad, Serge Wawa, Farid Mussa/Didier Kavumbangu, Jean Baptiste Mugiraneza, Himid Mao/Frank Domayo, Ramadhani Singano ‘Messi’/Mudathir Yahya, John Bocco na Kipre Tchetche

Naye Alexander Sanga anaripoti kutoka Mwanza kuwa timu ya Toto Africans na Ndanda FC ya Mtwara jana zilitoka 0-0 katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Wachezaji wa Ndanda FC walimlalamikia mwamuzi Abdallah Kambuzi wa Shinyanga wakidai alilikataa bao la Atupele Green dakika ya 89 wakati lilikuwa halali.