YANGA leo imeendelea kujiweka
vizuri katika harakati zake za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuichapa
Stand United mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es
Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga
iendelee kukaa kileleni ikiwa na pointi 30 huku Azam iliyo nafasi ya pili ikiwa
na pointi 26 lakini ikiwa nyuma mechi mbili. Azam leo inatarajiwa kucheza na
Majimaji Songea.
Mechi hiyo ilianza kwa timu
kushambuliana kwa zamu lakini iliichukua Yanga dakika 18 kuandika bao la
kuongoza lililofungwa na Amisi Tambwe baada ya kuunganisha pasi nzuri ya Thaban
Kamusoko.
Kuingia kwa bao hilo ni kama
kuliiamsha Stand ambapo dakika ya 28 mshambuliaji wake Elius Maguli alifurukuta
lakini nafasi ya wazi ya kufunga aliyoipata alishindwa kuitumia.
Tambwe aliwainua tena vitini
mashabiki wa Yanga baada ya kuongeza bao la pili katika dakika ya 36 kwa
kuunganisha pasi ya Juma Abdul.
Dakika moja kabla ya kwenda
mapumziko, Tambwe aliandika bao la tatu
safari hii akigongeana vizuri na Donald Ngoma.
Dakika ya 62 Kamusoko
aliifungia Yanga bao la nne pasi ikiwa na Abdul tena. Stand katika mechi ya
jana ilionekana kuzidiwa kuanzia dakika ya 20 za kipindi cha kwanza. Maguli na
Haruna Chanongo walikosa mabao katika dakika ya 40 na 42.
Kwenye uwanja wa CCM
Kirumba Mwanza, Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na wenyeji Toto Africans.
Daniel Lyanga ndiye aliifungia Simba bao la kuongoza katika
dakika ya 22 kwa shuti kali akiwa nje ya 18. Everisti Benard aliifungia Toto
bao la kusawazisha baada ya beki Hassan Isihaka kushindwa kuruka juu na kupiga
kichwa, mpira ukamkuta mfungaji akaukwamisha wavuni.
No comments:
Post a Comment