Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Kwanza kabisa niwapongeze Simba
SC, kitendo cha kukusanya alama sita katika uwaja wa Mkwakwani, Tanga
ndani ya siku nne ni kipya kabisa kwao, lakini mwisho wa siku Simba
imefanikiwa kushinda 1-0 dhidi ya African Sports na 2-0 dhidi ya JKT
Mgambo. Ni mwanzo mzuri, tena ushindi mzuri wameupata katika moja ya
viwanja vigumu kwa timu za Dar es Salaam.
Awali sikuwa na imani, niwe
mkweli licha ya kutambua vipaji vipya katika timu na uwepo wa benchi la
ufundi jipya tena lililopangiliwa ila bado sikuwa na imani na safu ya
utawala ambayo ‘ilikuwa na mazoea ya kupaniki’ na hivyo kupunguza
uwajibikaji wa timu.
DYLAN KERR
Mwalimu huyo raia wa Uingereza
pengine ni mapema mno kuweza kumsifia lakini kwa namna alivyoweza
kuisimamia timu yake katika gemu mbili za awali hakika anastahili
kupongezwa. Simba imecheza vizuri katika mechi zote mbili. Timu imekuwa
ikicheza kwa kasi katika mtindo wa kupanga mashambulizi.
Katika mechi ya ufunguzi dhidi ya
Sport, Kerr aliwapaga wachezaji, Hassan Kessy, Mohamed Hussein
‘Tshabalala’, Juuko Murishid na Justice Majabvi katika idara ya ulinzi,
Said Ndemla, Awadh Juma, Mwinyi Kazimoto katika eneo la kiungo, Musa
Mgosi, Peter Mwalyanzi na Hamis Kiiza katika safu ya mashambulizi.
Safu ya ulinzi haijafanya makosa,
Kessy na Tshabalala wameendelea kucheza kwa viwango vya juu katika
fullbacks, wakati Juuko ameendelea kujiweka katika orodha ya mabeki bora
wa kati katika VPL, Mganda huyo amekuwa akitumia nguvu na akili kiasi
cha kumfanya Majabvi kucheza vizuri kama mlinzi wa mwisho katika gemu ya
kwanza na hata aliporudi Hassan Isihaka katika gemu ya Mgambo safu ya
ulinzi iliendelea kucheza kwa umakini, utulivu na kitendo cha kutoruhusu
bao katika dakika 180 ni dalili njema.
Ni dhamira iliyokuwepo, kuchukua
alama 6 katika gemu mbili za kwanza tena wakifunga magoli matatu
ugenini. Kerr alimuanzisha benchi Kiiza katika mchezo wa jana na nafasi
hiyo akacheza Mwinyi. Kutawala mchezo mbele ya Mgambo iliyokuwa na
Mohamed Samatta, Helbert Charles na Chande Magoya katikati ya uwanja ni
kielelezo kingine kuwa eneo la kati la Simba limeendelea kuimarika
lakini bado wana u-haba wa kupiga pasi za mwisho.
DHIDI YA KAGERA SUGAR
Itakuwa mechi ya tatu ya msimu na
ya kwanza kwa Simba katika uwanja wa nyumbani (uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam). Simba wamekuwa wakisisitiza kushinda kila mchezo na kabla ya
kuwavaa mahasimu wao Yanga SC wiki ijayo, Kerr atakutana na timu
nyingine inayowasumbua sana. Kagera imecheza gemu mbili ugenini,
walishinda 1-0 dhidi ya Mbeya City kisha wakapoteza Jumatano hii mbele
ya Majimaji FC kwa goli 1-0.
“Historia zimewekwa ili kuvunjwa, tutajitahidi kuhakikisha tunashinda kila
mechi inayokuja mbele yetu”, ni
maneno ya mkuu wa kitengo cha habari wa klabu ya Simba, Hajji Manara
mara baada ya kushuhudia timu yake ikishinda kwa mara ya pili mfululizo.
Baada ya kuvunja mwiko wa kutoshinda Tanga kwa misimu mitatu mfululizo,
je, Simba wataifunga Kagera Sugar kwa mara ya kwanza tangu msimu wa
2012/13 katika uwanja wa Taifa?
Kwa hisani ya Shafii Blog
No comments:
Post a Comment