MAKOCHA wa timu za Yanga na Gor Mahia ya Kenya wametambiana kila mmoja
kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa ufunguzi wa Mashindano ya kombe la Kagame
utakaochezwa kesho majira ya saa 10:00 kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja
wa Taifa.
Kocha wa mkuu wa Yanga Hans Van Pluijm amesema anawaheshimu wapinzani wake
timu ya Gor Mahia lakini haiogopi na ana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi
kwenye mchezo huo.
“Nimefundisha soka Afrika tangu mwaka 1996 hivyo nina uzoefu na soka la
timu za hapa kwa muda mrefu, lakini pia tumefanya maandalizi ya kutosha lakini mimi
sidharau mpinzani wangu kwa sababu kwenye soka lolote linaweza kutokea na hakuna
mtu anayejua matokeo”, amesema Pluijm.
Kocha mkuu wa Gor Mahia, Frank Nuttal amesema hana uzoefu mkubwa
kwenye soka la Afrika ukilinganisha na mpinzani wake (Van Pluijm) lakini
akasisitiza kuwa vijana wake wako vizuri kuikabili Yanga.
“Yanga ni timu kubwa japo sijawahi kuiona ikicheza lakini naamini ni timu
yenye ushindani na mechi ya kesho itakuwa ngumu lakini mwisho wa mchezo
tutajua matokeo”, amesema Nuttal.
Mchezo huu ambao mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Ujenzi, John
Magufuli ambaye pia ni mteule wa kugombea kiti cha urais kupitia chama tawala
(CCM) unatarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake kutokana na timu zote kuwa na
historia inayolingana kwenye mashindano haya kwani kila mmoja ametwaa kombe la
Kagame mara tano.
Yanga ndio mabingwa wa ligi kuu
Tanzania bara ambayo ilimalizika mwezi Mei mwaka huu wakati wapinzani wao
wakiwa wanaongoza ligi ya Kenya (KPL) inayoendelea kutimua vumbi nchini humo.
Wakati Yanga na Gor Mahia wakicheza mchezo wao jioni timu ya APR ya
Rwanda na Al Shandy ya Sudan, watakuwa kibaruani saa 8:00 kwenye mchezo wa
awali kwenye Uwanja huo wa Taifa na mchezo mwingine wa kundi A utachezwa kwenye
uwanja wa Karume ukizikutanisha KMKM dhidi ya Telecom kutoka Djibout
No comments:
Post a Comment