TIMU ya Taifa ‘Taifa Stars’ leo asubuhi ilionja
adha ya kuzomewa na mashabiki kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam
ilipokwenda kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa ma mchezo wa kufuzu fainali
za kombe la mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) dhidi ya Uganda.
Taifa stars iliwasili uwanjani hapo saa 3:30
asubuhi na kukuta mashabiki wakiangalia
mazoezi ya Yanga ambayo inajiandaa na mashindano ya Kagame yanayotarajia kuanza
Julai, 9.
Baada ya kuwasili
meneja wa timu hiyo Boniface Clemence alianza kushusha vifaa vya mazoezi
na wachezaji kuanza kushuka, mashabiki walipowaona ndipo wakaanza kupiga kelele
za kuzomea huku wengine wakiwaita watalii hali iliyofanya kocha kuamuru vifaa
virudishwe ndani ya gari.
“Buuuh watalii hao, buuu watalii hao,” walizomea
mashabiki hao.
Kelele hizo ziliongezeka kwani mashabiki waliokuwa
kwenye jengo la Machinga nao walipowaona walizomea zaidi.
Baadae zomeazomea hiyo ilikuja kutulizwa na meneja Clemence
pamoja msaidizi wa rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
Juma Matandika waliowataka mashabiki kuwa wazalendo kwani hiyo ni timu yao ya
taifa hakuna haja kuizomea.
“Jamani mnapozomea haisadii kwani hii ni timu yetu
sote watanzania ni kweli tumefungwa lakini angalia rekodi ya Misri, hakuna timu
ambayo imekwenda kucheza pale ikatoka bila kufungwa tena kwa idadi kubwa ya
mabao,”, alisikika akisema Clemence.
Baada ya hali kuwa shwari wachezaji na benchi la
ufundi walitoka wakaingia Uwanjani kuanza mazoezi huku wakipishana na Yanga
ambao nao walikuwepo kwenye Uwanja wa Karume wakifanya mazoezi.
Taifa stars inatarajiwa kuondoka leo kwenda visiwani
Zanzibar kwa ajili ya mchezo dhidi ya Uganda utakaochezwa keshokutwa.
Akizungumzia
mchezo huo kocha wa Taifa Stars Mart Nooij alisema anaamini watashinda kwani
wachezaji wake wapo vizuri kuanzia mbinu, akili na morali ipo juu kwani wanajua
wana deni kwa watanzania.
“Naamini
tutashinda kwani tumejiandaa kwa ajili ya mchezo huo na wachezaji wameshasahau
yaliyopita tunachoomba ni ushirikiano kwa watanzania wote”, alisema Nooij.
Aidha, rais
Malinzi amemwambia kocha huyo kuwa akishindwa kuivusha timu
katika michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kibarua chake kitaota mbawa.
Baada ya mchezo huo wa Jumamosi,
mchezo wa marudiano dhidi ya Uganda utachezwa Julai 4, mwaka huu nchini Uganda.
No comments:
Post a Comment