Na mwandishi wetu.
Washiriki wa
mbio za baiskeli zijulikanazo kama “Acacia Tufanikiwe Pamoja Lake Zone
Cycle Challenge” kutoka mikoa ya Shinyanga na Mwanza wameendelea
kuudhihirisha umma wa wakazi wa kanda ya ziwa na watanzania kwa ujumla kuwa
mpaka sasa hawana mpinzani baada ya washiriki wa mbio hizo kuibuka kidedea
katika fainali za kumtafuta mshindi wa kanda hiyo.
Washiriki wa
mikoa hii miwili wamejinyakulia nafasi zote za juu na hivyo kuwashinda wenzao
wa mikoa mingine ya Kanda ya ziwa ikiwemo Kagera, Mara, Geita na Simiyu.
Katika mbio
za wanaume za umbali wa kilometa 156.6 kutoka Kahama mpaka Tinde na kisha
Kurejea Kahama, mshindi wa mwaka jana Masunga Duba (Mwanza) aliibuka tena
kidedea huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Lupilya Hamis(Shinyanga) na nafasi
ya tatu ikimuendea Kulwa Tuki(Shinyanga), washindi hawa wamejinyakulia kitita
cha pesa taslimu Sh1,500.000/- kwa mshindi wa kwanza, Sh1,200.000/= mshindi wa
pili na Sh800,000/= kwa mshindi wa tatu.
Kwa upande
wa mbio za wanawake za umbali wa kilometa 80, kutoka Kahama mpaka Mwakata Kisha
kurejea Kahama, timu ya mkoa wa Mwanza imedhihirisha kuwa wao bado ni mabingwa
kwa kuibuka tena washindi wa mbio hizo, huku mshindi wa mbio za Mwaka jana
Martha Antony, akiibuka mshindi wa kwanza akifuatiwa na Laulensia Luziba na
nafasi ya tatu ikienda kwa Veronica Simon. Washindi hao wamepata zawadi ya pesa
taslimu Sh1,200.000/= kwa mshindi wa kwanza, Sh800,000/= mshindi wa pili na
Sh600,000/= mshindi wa tatu.
Mbio hizo
ambazo zimeandaliwa na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) kwa udhamini wa
kampuni ya uchimbaji wa Madini ya Acacia, inayomiliki migodi ya North Mara,
Bulyanhulu na Buzwagi, yote ikiwa mikoa ya kanda ya ziwa, kupitia mpango wake
wa Tufanikiwe Pamoja ikiwa ni mara ya pili sasa ambapo mashindano ya
mwaka huu yameonyesha mafanikio makubwa kutokana na maandalizi mazuri
yaliyofanyika.
Akizungumza
na washiriki wa mashindano hayo Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpyesa, ambaye
alikua mgeni rasmi wa fainali hizi, amesema ana imani kuwa mashindano
hayo yatasaidia kuibua vipaji ambavyo vitauletea sifa mkoa wa Shinyanga, Kanda
ya ziwa na hata taifa kwa ujumla kwani baiskeli kwa maeneo hayo ndiyo jadi yao.
Awali
akimkaribisha Mkuu wa wilaya kuzungumza na washiriki hao, Makamu wa Rais wa
Acacia Deo Mwanyika amesema kampuni ya Acacia imekuwa ikifanya shughuli za
uchimbaji unaojali na ndio maana iliona vyema kuweka udhamini wake pia katika mchezo
wa baiskeli, “toka tuanze huu sasa ni mwaka wa pili na tunayaona mafanikio
makubwa kwani hata maeneo ambapo mchezo huu ulikuwa hauchezwi sasa unachezwa,
hali ambayo imeongeza hamasa na idadi ya washiriki.”
Aidha Makamu
wa Rais huyo wa Acacia amesema mipango ya kampuni kwa sasa ni kuona pia
inashiriki katika kuendeleza michezo mingine ikiwemo na soka.
Mmoja wa washiriki wa mbio hizo akinywa maji wakati wa mashindano hayo.
Mshindi
wa mbio za Acacia Tufanikiwe Pamoja Lake Zone Cycle Challenge, Masunga
Duba aliyeinua mikono akishangilia mara baada ya kumaliza mbio hizo
akiwa mbele ya wenzake. Mshindi huyo anatoka mkoa wa Shinyanga.
Makamu wa Rais
wa Kampuni ya Uchimbaji wa dhahabu ya Acacia, Deo Mwanyika (wa kwanza
kushoto) akifurahia jambo na Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni ya
Acacia, Mishel Ash, (wa pili kutoka kushoto) ambaye pia ni kaimu Meneja
Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu.
Washindi
wa mbio za wanawake (kilometa 80). Aliyesimama katikati ni Martha
antony ambaye ndio aliibuka mshindi wa kwanza, akifuatiwa na Laulensia
Luzuba, (mwenye mtoto) aliyekuwa mshindi wa pili na Veronica Saimon (wa
kwanza kushoto) aliyejinyakulia nafasi ya Tatu.
No comments:
Post a Comment