KAMATI ya Utendajia ya Shirikisho la soka Tanzania
(TFF) imepitisha ombi la usajili wa wachezaji saba wa kigeni kwa klabu za Ligi
Kuu Tanzania Bara.
Hicho kilikuwa kilio kikubwa kwa klabu za ligi, hasa
Yanga, Azam na Simba ambazo ndizo zinazosajili wachezaji wengi wa kigeni.
Kabla ya TFF kupitisha uamuzi huo, klabu
ziliruhusiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni bila kulipa TFF ada lakini
sasa watalazimika kulipia kila mchezaji wa kigeni atakayesajiliwa.
Habari kutoka ndani ya kikao cha kamati ya utendaji
kilichofanyika mjini Zanzibar leo, zilisema mvutano ulikuwa mkali wa ama
kusajili wachezaji watano ama saba.
“Mjadala ulichukua muda mrefu sana, lakini kama
unavyojua hiki kitu klabu kubwa zinamaslahi nacho, na ndio waliotoa ushawishi
kwa wajumbe wengi kutaka usajili wa wachezaji saba mwisho tukakubaliana hivyo
na hao saba wanaruhusiwa kucheza wote kwenye mechi moja,” alisema mtoa habari
wetu kutoka ndaniya kikao hicho.
Lakini timu
zimewekewa sharti gumu ambalo ni lazima
kila mchezaji alipiwe ada ya dola za Marekani 2000 kwa mwaka lakini pia
mchezaji anayesajiliwa kutoka nje lazima awe anacheza timu ya taifa ya nchi husika au Ligi Kuu.
Hii si mara ya kwanza kwa klabu za Ligi Kuu
kuruhusiwa kusajili wachezaji zaidi ya watano, miaka ya nyuma ilikuwa ikisajili
wachezaji kumi na kuruhusiwa kutumia watano kwenye mechi moja, lakini hakukuwa
na masharti yoyote ya aina ya wachezaji wa kusajiliwa, hali iliyofanya klabu
kusajili wachezaji wasio na uwezo, ama majeruhi ambao wakifika nchini hushindwa
kutoa msaada kwa klabu husika.
Mwaka 2007 kulifanyika kangamano Bagamayo ambapo
baadhi ya maazimio kwenye kongamano lile ni kupunguza idadi ya wachezaji wa
kigeni ambapo ilikubalika mpaka msimu uliopita klabu zisajili wageni watano na
watakaotumika kwa mechi moja wawe watatu.
Lakini hali imekuwa tofauti baada ya baadhi ya klabu
kudai kuongezewa idadi ya usajili wa wachezaji wa kigeni ili zifanye vizuri
kwenye michuano ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment