MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi kwenye bonanza la kutafuta timu zinazoshiriki michuano ya NACTE
litakalofanyika kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani siku ya
jumamosi.
Bonanza hilo litashirikisha wanavyuo wa vyuo vya ufundi
vilivyo chini ya VETA sehemu mbalimbali kwenye michezo ya soka, kikapu,netiboli
pamoja na mchezo wa wavu ni sehemu ya tatu ya bonanza yanayoendelea kwenye
viwanja mbali mbali nchini.
Akizungumzia bonanza hilo Mratibu wa Michezo Vyuoni,
Mpalule Shaaban alisema kuwa Mwantumu anatarajiwa kufanya Uzinduzi wa Michezo
hiyo kwa Mkoa wa Pwani kwa sababu michezo hiyo itafanyika kila mwaka sehemu
mbali mbali za Tanzania.
"Ni heshima ya pekee ambayo Serikali imetoa kwa
Vijana wetu wa vyuo vya elimu ya kati kushiriki michezo, kumbuka kwamba michezo
hii haijawahi kuchezwa tangu NACTE imeanzishwa hivyo hii ni fursa ya pekee
kuhakikisha kwamba tunahamasisha michezo wakati wote ili vijana wanaojiunga na
Vyuo vya Elimu ya Ufundi Veta, na wale wa ngazi ya Diploma kushiriki michezo
vyuoni" alisema Mpalule.
Pia amewataka wanachuo watakao bahatika kuchaguliwa
kuunda timu za kanda wahakikishe wanafanya mazoezi ili kukabiliana na ushindani
kwenye mashindano ya fainali zitakazokutanisha kanda zote.
Aidha vyuo vyote vinavyohusika na michezo zimetakiwa
kuwahi viwanjani ili kukamilisha taratibu za ukaguzi mapema na michuano hiyo itaendeshwa
kwa mfumo wa Bonanza na itafanyika kila siku za Jumamosi kutokana na wanafunzi
kuwa masomoni katika siku za kawaida.
Michezo
mingine itakayokuwa ikifanyika kati ya wanafunzi na wanafunzi ni Debate, Riadha,
urembo, mashindano ya vipaji kwa viongozi wanaosimamia serikali za
wanafunzi kwa nafasi za Rais na Makamu, Waziri Mkuu, Mawaziri wa
Michezo,Fedha, na Spika , watakaokuwa wakichuana katika kujielezea,
kujibu maswali, na kuelezea mada katika nafasi zao na changamoto
wanazokabiliana nazo na washindi watakuwa wakipata tuzo mbali mbali kulingana
na ushindi wa kila mmoja.
No comments:
Post a Comment