Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, December 7, 2016

Wilhem Gidabuday:Mchawi mpe mtoto wako amlee

*Baada ya kukosoa sasa ni wakati wake wa kufanya kwa vitendo


Na Rahel Pallangyo
BAADA ya muda mrefu kuwa na kiu ya kuona Tanzania inafanya vizuri katika michezo, hususani ule wa riadha, Wilhelm
Gidabuday amekuwa Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT).

Sasa amevaa viatu vilivyoachwa na Suleiman Nyambui ambaye alikiacha kiti hicho cha ukatibu mkuu baada ya kupata nafasi ya kuwa kocha wa timu ya taifa ya Brunei.

Mkutano Mkuu wa uchaguzi Mkuu wa RT uliofanyika Jumamosi iliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wajumbe wa mkutano huo walimchagua Gidabuday kuwa Katibu Mkuu kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Baada ya kuondoka kwa Nyambui, nafasi hiyo ilikuwa ikikaimiwa na Ombeni Zavalla ambaye alikuwa katibu msaidizi.

Gidabuday siyo jina geni masikioni mwa wengi kwa jinsi ambavyo alivyokuwa akipigania maendeleo ya mchezo huo kwa kuwa mstari wa mbele kuwakosoa viongozi wa michezo.

Alikuwa mstari wa mbele kuosoa

Hakuna chombo cha habari kisichomjua Kidabuday kwanza kutokana na jina lake kuwa la kipekee  kuwa na kipaji kikubwa cha kuongea kwa mpangilio.

Kidabuday lianza kukosoa kuanzia RT hadi Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) akisema wameshindwa kuiwezesha Tanzania kupata medali.

Kuna wakati aliingia katika mgogoro mkubwa na TOC hasa katibu wake Filbert Bayi pale alipodaikuwa yuko tayari kuchoma vyeti vyake uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kama timu ya Tanzania iliyoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola Glascow, Scotland ingerudi na medali.

Timu hiyo haikurudi na medali na Gidabuday aliendelea kuchonga na kuzidi kujizolea umaarufu, lakini hakujua kuwa TOC haikuwa na wachezaji na jukumu la kuandaa timu liko kwa vyama vya michezo.

Gidabuday alitakiwa kuvisaka vyama vya michezo na sio TOC, ambayo haina wachezaji na haikuwa na fungu la kuvifaidia vyaka kuziandaa timu zao.

Mchawi mpe mwao amlee.

Kuna usemi wa Kiswahili usemao kuwa, mchawi mpe mwanao amlee kwani kufanya hivyo kutamzuia kumuua mtoto huyo kwani ataogopa akifanya hivyo atajulikana kuwa ni yeye aliyehusika na mauaji hayo.

Watu wa riadha hawakukosea kabisa kumpa Gidabuday kazi ya kuiongoza RT kwani baada ya kuongea mengi mazuri na mipango mingi ya kuuendeleza mchezo huo, sasa ni wakati wake wa kuyafanya kwa vitendo.

Yale ambayo aliweza kuyakosoa kwa muda mrefu, sasa wakati umefika wa kuyaweka katika vitendo, ili Tanzania iweze kupiga hatua kubwa katika mchezo wa riadha.

Malengo yake makubwa

Gidabuday anasema ili kuinua riadha hakuna budi kuimarisha vyama vya mikoa kwa kuvipatia vifaa kama ofisi, usafiri pamoja na komputa.

Katibu Gidabuday anasema kwa kushirikiana na makatibu tawala wa mikoa watahakikisha kila mkoa unapata ofisi, usafiri pamoja na komputa ili kuwarahisishia viongozi wa mikoa kwenye utendaji wao wa majukumu.

"Riadha Taifa haiwezi kuona vipaji vilivyopo mikoani ila vyama vya mikoa ndivyo vye uwezo wa kuvifikia vipaji hivyo vilivyopo wilayani hadi vijijini kinachotakiwa ni kuwawezesha tu, “ anasema.

Anasema kuwa wakifanikiwa kuwasaidia viongozi wa mikoa hakuna wasiwasi kuwa riadha itarejeakatikammstari kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ya 1970 hadi 1990.

Gidabuday anasema viongozi wa vyama vya mikoa walifanywa kama kiungo wakati wa mkutano mkuu kwa sababu ni wapiga kura tu lakini wakati wa maendeleo wamekuwa wakitengwa.


Kituo cha kuendeleza riadha
Ili kuendeleza na kukuza vipaji vinavyopatikana kwenye mashindano mbalimbali, Gidabuday anasema wanatarajia kuanzisha kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji.

"Kuna mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi Tanzania (UMISHUMTA), na ile ya Sekondari (UMISSETA) na mashindano ya bingwa wa taifa, hivyo washindi wanaopatikana tutakuwa tunawaweka kwenye kituo," alisema.

Pia Gidabuday anasema angependa kituo hicho kijengwe kati ya mikoa ya Kanda za Juu Kusini kwa sababu maeneo hayo hali ya hewa ni nzuri kufanyia mazoezi kuliko mikoa yenye joto.

Gidabuday anasema kuwa na kituo kunaweza kurudisha riadha kwani kipindi ambacho michezo ilisimama shuleni ilisababisha michezo kudorora kwa ujumla.

Pia Gidabuday anasema kuwa wanatarajia kuhamasisha mchezo wa riadha kwa mikoa ya Kusini kwani anaamini wanaweza kupata wanariadha wazuri tatizo hawajapata watu wa kuwahamasisha kupenda mchezo huo kama ilivyo kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kati.

Wataalamu wa riadha
Katika kuendeleza riadha Gidabuday anasema watahakkikisha wanawatumia wataalamu waliopo na kutoa mafunzo kwa wataalamu ili wale wanaowafundisha wanariadha wawe na elimu sahihi.

"Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAAF) linatoa kozi mbalimbali, hivyo ni jukumu la RT kuhakikisha linapeleka watu kwenda kusoma au unaweza kuomba mtaalamu aje kufundisha hapa nchini hivyo tutahakikisha tunatoa fursa za kuendeleza makocha," alisema.

Gidabuday anasema yeye kama mtendaji atakuwa makini kufuatilia ratiba ya IAAF kuona fursa zilizopo na kuzitumia,  kwani RT walipoteza uaminifu kwa IAAF

Pia alisema RT inajivunia kuwa na wataalamu kama Samuweli Tupa, Robert Kaliyahe na wengine wingi, ambapo ameahidi kuwatumia.

Nafasi za Mafunzo Marekani
Gidabuday anasema Tanzania ilikuwa inapata nafasi za masomo na mafunzo kwenye vyuo vikuu nchini Marekani, lakini nafasi hizo zilikoma kutolewa 1993 baada ya kuona viongozi wa RT (zamani TAAA) walikuwa wanapeleka watoto wao ama ndugu zao ambao siyo wanariadha.

"National College Athletics Association (NCAA) ya Marekani ilikuwa inatoa nafasi 25 kila mwaka, lakini tulikuja kukosa nafasi hizo baada ya baadhi ya viongozi kupeleka watoto wao ambao hawakuwa wanariadha, “alisema na kuongeza:

“Mimi ni nmoja na wanafunzi wa mwisho kwenda Marekani hivyo tutafanya mazungumzo na NCAA kuona kama tunapata tena hizo nafasi," anasema Gibabuday.

Gidabuday anasema kuwa wanafunzi wanariadha walikuwa wanalipiwa kila kitu na vyuo hivyo na vyuo vilikuwa vinaona fahari pale wanafunzi hao walipokuwa wakifanya vizuri kwenye michezo kwani ilisaidia kukitangaza chuo.

Wanariadha ambao wamesoma kupitia mpango huo ni yeye mwenyewe Gidabuday, Bayi, Mwinga Mwanjala, Makene, Suleiman Nyambui, Shahanga na wengine wengi.

Gidabuday anasema wana imani kupata hizo nafasi za masomo kwa sababu NCAA ilisema endapo Tanzania itapata viongozi wapya ambao watathibitisha kupeleka walengwa watarudisha.

"Tunaamini tutapata hizo nafasi hivyo na sisi itabidi tuingie makubaliano na wale ambao tutawapeleka kuwa sharti ni kurudi nyumbani kusaidia michezo baada ya kuhitimu na siyo kuzamia," anasema.


Mashindano ya Kimataifa
Tanzania ilikuwa ikipata mialiko mingi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, lakini ilipungua baada ya kuwa wanaopelekwa hawafanyi vizuri kwa sababu waliokuwa wanakwenda walikuwa hawana sifa.

Gidabuday anasema IAAF ikitoa nafasi ya kushiriki halafu ukafanya vibaya unapunguzwa maksi, lakini ukifanya vizuri pointi zinaongezeka, hivyo kwa sababu Tanzania ilikuwa ikifanya vibaya nafasi zilipungua.

Pia anasema kutopeleka wanariadha kwenye mashindano pia kulisababisha kukosa pointi na kulazimika kulipa faini ambazo zilikatwa kutoka kwenye mgao unaotoka IAAF.

"IAAF ilikuwa inatuma tiketi za ndege ambazo hazijaandikwa majina, hivyo RT ilitumia mwanya huo kuweka watu wao hali iliyosababisha kutofanya vizuri na nafasi zetu ziliongezewa Kenya hivyo tutahakikisha tunawaandaa wanariadha wetu ili wakafanye vizuri, " anasema Gidabuday.

Kuna nafasi za wanawake, wanaume na walemavu, ambazo Tanzania inatakiwa kupeleka wawakilishi au washiriki kwenye mashindano, lakini tumeshindwa kuzitumia.

Gidabuday anasema April 2017 watapeleka wanariadha nane nchini Uganda kwa ajili ya mashindano ya dunia ya mbio za Nyika.

Ufadhili wa Riadha                   
Gidabuday anasema kwa kushirikiana na serikali wanaamini watapata wafadhili kila mashindano kuanzia ngazi ya mkoa hadi Taifa.

"Kwa kushirikiana na makatibu tawala wa mikoa tuna imani tutapata wafadhili kwenye mashindano mbalimbali hali itakayosaidia kuinua riadha," anasema Gidabuday.

Pia Gidabuday anasema watamtumia balozi wa kampuni ya vifaa vya michezo ya ASICS nchini, Juma Ikangaa kuomba ufadhili wa vifaa vya michezo kwa wanariadha wa Tanzania.

"Tuna bahati Ikangaa ni balozi wa ASICS tangu 1984, hivyo tutaandika pendekezo letu kuomba kampuni hiyo itasaidie vifaa na naamini tutapata kwa heshima ya Ikangaa," alisema Gidabuday.

Pia alisema pendekezo lao watalipeleka kwenye makampuni mbalimbali hapa nchini na kwa kuwa anaaminika anaamini watapata wafadhili kwa sababu tutajitahidi pia kuwapa elimu ya faida ya kufadhili riadha.

"Wanariadha wanaweza kutangaza raslimali za nchi hii kimataifa hata bidhaa za makampuni yetu hivyo elimu inahitajika kwa wadau kufahamu faida zake," alisema Gidabuday.

Zawadi nono imeua mbio fupi 
Gidabuday anasema wanariadha wengi wameacha mbio fupi na kukimbilia mbio ndefu kutokana na zawadi zinazotolewa kwenye mbio ndefu kuwa na mvuto.

"Mbio fupi zimekosa washiriki kwa sababu wengi wamekimbilia mbio ndefu kutokana na ubora wa zawadi zinazotolewa kwa washindi na makocha kuhamasisha wanariadha kucheza mbio ndefu kwa kuangalia maslahi kuliko kuendeleza vipaji," anasema Gidabuday.

Gidabuday anasema watajitahidi kuhamasisha mbio fupi kwa wanariadha wachanga ili wasiogope mchezo huo na kuwapa faida za kuanza na mbio fupi kwani miili yao inakuwa haijazoea shuruba.

Mikoa kupewa kipaumbele
Gidabuday anasema RT itatoa kipaumbele kwa mikoa inayotoa asilimia kubwa ya wanariadha wanaowakilisha nchi kimataifa huku akitolea mfano mkoa wa Singida ambao umetoa wanariadha watatu walioshiriki mashindano ya Olympiki iliyopita.

Anasema kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza ushindani wa mikoa kutoa wanariadha bora.

Anasemaje kuhusu safu mpya?
Gidabuday anasema uongozi mpya wa RT ni alama ya  kuiondoa riadha hapa ilipo na kuipeleka sehemu nyingine kwa sababu Mwenyekiti wao Anthony Mtaka ni kiongozi wa mfano.

"Mtaka amesaidia riadha hata nafasi ya tano aliyopata mwanariadha wa Tanzania Alphonce Simbu katika Olimpiki ya Rio 2016 ni juhudi zake, hivyo kwa kushirikiana na mimi naamini tutaipeleka riadha mahali,  ambapo bendera ya Tanzania itaonekana,"anasema.

Gidabuday anasema Mtaka ni kiongozi mzalendo ambaye anapenda michezo kutoka ndani ya moyo wake, hivyo kwa dhamira hiyo anaamini riadha itarudi kama ilivyokuwa enzi za Filbert Bayi na Juma Ikangaa.


Gidabuday ni nani?
Gidabuday ni mwanariadha wa zamani mwenye taaluma ya elimu ya viungo kutoka Chuo Kikuu cha Life University, Atlanta, USA,1995/98
Elimu kidato cha tano na sita alisoma Riverside California, USA. 1993/95.

Wakati elimu ya msingi alisoma shule ya Msingi Nangwa 1980-1986 na kidato cha kwanza hadi cha nne alipata shule ya Balang'da Lalu, Hanang 1988-1991

 Gidabuday 1993/1994 California State Champion in X/Country USA, 1994 alishiriki California State meta 5,000 na meta 10,000 Champ USA, 1995 NCCA Runner-Up Milwaukee State USA, Winner of 1998 Los Angeles Super Bowl 10k USA
                                      
Pia ni mshindi wa kwanza kwa niaka mitatu mfululizo 2001/2002/2003 wa Los Angeles Revlon kilometa tano, mshindi wa NIKE Run Los Angeles 2004.
                           
Gidabuday kijana mwenye miaka 42, mzaliwa wa mkoa wa Manyara kutoka kijiji cha Dirma, Hanang ana mikakati mizito ya kuhakikisha RT inasonga mbele hapa nyumba na kimataifa.