Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana hivi karibuni imekubali mapendekezo ya Kamati ya
Mashindano ya kurejesha michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL).
Lengo la kurejesha ligi hiyo ni kuongeza wigo wa
mashindano kitaifa ambapo itasaidia kushirikisha kundi kubwa zaidi la wachezaji
kwenye mashindano makini yanayozingatia viwango na vigezo ili kuwapa wachezaji
maendeleo ya kiuchezaji ikiwemo kuendelezwa vipaji vyao kitaalamu.
Ligi hiyo yenye timu 24 itachezwa katika hatua ya
makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ambapo
mshindi wa kila kundi atapanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Timu ya
mwisho kila kundi itarudi kwenye ligi ya mkoa wake.
Hatua ya pili ni kutafuta bingwa wa SDL ambapo timu
zilizoongoza makundi (nne) zitacheza kwa mtoano nyumbani na ugenini. Utakuwepo
mchezo wa fainali ambapo mshindi atkuwa bingwa wa SDL msimu wa 2014/2015.
Timu zitakazocheza SDL kwa msimu huu ni zile
zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nane katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL)
katika makundi yao msimu uliopita, na tatu zilizoshuka kutoka FDL msimu
uliopita.
Kundi A litakuwa na timu za Milambo FC (Tabora),
Mji Mkuu FC (Dodoma), Mpanda United (Mpanda), Mvuvumwa FC (Kigoma), Singida
United (Singida) na Ujenzi (Rukwa). Kundi B ni Arusha FC (Arusha), Bulyanhulu
FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), Mbao FC (Mwanza), Pamba FC (Mwanza) na
Rwamukoma JKT (Mara).
Timu za kundi C ni Abajalo (Dar es Salaam), Kiluvya
United (Pwani), Kariakoo FC (Lindi), Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC
(Dar es Salaam) na Transit Camp (Dar es Salaam). Kundi D ni Magereza FC
(Iringa), Mkamba Rangers (Morogoro), Njombe Mji (Njombe), Town Small Boys
(Ruvuma), Volcano FC (Morogoro) na Wenda FC (Mbeya).
Ligi itachezwa kuanzia Novemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment