“Kwa
niaba ya mteja wetu, Emmanuel Arnold Okwi, napenda kutoa maelezo kuhusu
Uamuzi wa kihistoria katika soka la Tanzania ambao umefanywa na Kamati
ya Sheria na hadhi ya wachezaji ya TFF. Uamuzi huo ni wa kihistoria kwa
misingi ifuatayo:
MOSI: Ni
mara ya Kwanza katika historia ya soka la Tanzania ambapo Kamati inakaa
kujadili haki ya mchezaji dhidi ya klabu kubwa na hatimaye kuamua kwa
manufaa ya mchezaji, tena pasipo kupiga kura kwa misingi ya upenzi na
unazi. Kamati ya Mwanasheria Mashuhuri na mwenye Msimamo Bw. Richard
Sinamtwa iliamua kustafsiri kanuni kwa kufuata ushahidi uliopo na kwa
haki kabisa pasipo kujiingiza katika mtego wa kupiga kura kama ambavyo
tumekua tukiiona huko nyuma.
PILI:
Kamati ikiongozwa na Mwenyekiti ilitumia busara ya hali ya juu kwa
kukataa ombi la Yanga la kutengua uteuzi wa Bw. Hans Pope katika Kamati
hiyo. Ikumbukwe kuwa Yanga ilileta hoja ya kumkataa Bw. Hans Pope kwa
misingi ya mgongano wa kimaslahi na kumtaka mwenyekiti atoe uamuzi juu
ya suala hilo. Endapo mwenyekiti angetoa maamuzi ya kumuondoa Hans Pope,
basi angejiingiza katika uvunjaji wa Katiba ya TFF kwasababu yeye sio
mamlaka ya uteuzi wa Hans Pope katika Kamati hiyo. Mwenye mamlaka hayo
ni Kamati ya Utendaji ya TFF. Hivyo Yanga walipaswa kuelewa hilo na si
kuishinikiza kamati, hususan Mwenyekiti, amuondoe Hans Pope kwenye
Kikao.
TATU: Maamuzi
ya Kamati yamefungua njia kwa wachezaji wengi ambao mikataba yao
inachezewa na vilabu kwa muda mrefu pasipo kuwa na nafuu yoyote ya
kisheria kwa wachezaji hao ambao ndio nguzo ya muhimu katika mpira wa
Tanzania. Hata hivi sasa kuna wachezaji ambao bado hawajalipwa stahili
za mikataba yao ndani ya Yanga. Tunawaomba wajitokeze ili tuwasaidie
wapate haki zao za kisheria kama ambavyo imetokea kwa Okwi.
NNE: Pamoja
na madai ya Yanga ya kukata rufaa FIFA / CAS, naomba wajue kuwa haki
yao ya kukata rufaa inatokana na ukweli kuwa Kamati ya Sheria na Hadhi
ya Wachezaji ya TFF imetekeleza wajibu wake. Uamuzi huo wa Kamati
umejenga msingi muhimu sana katika suala zima la kuheshimu na kutekeleza
mikakaba kwa mujibu wa kanuni za FIFA. Endapo Yanga watakata rufaa kama
wanavyodai, itakuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha nguzo ya
kuheshimu mikataba ya wachezaji inapewa msisitizo unaostahili.
MGOGORO KATI YA YANGA NA OKWI
Mkataba wa Yanga na Okwi, ambao ulisainiwa tarehe 12 Disemba 2014 umekuwa na mapungufu yafuatayo:
1. Mkataba
huo umempa majukumu mchezaji kufuatilia ITC na suala zima la yeye
kupata vibali vya kucheza. Hii ni kinyume na Kanuni za FIFA ambao
zinatamka bayana kuwa jukumu la kufuatilia ITC ni la wanachama wa FA,
lakini Yanga walimtwisha Okwi zigo hilo. Okwi alitekeleza jukumu hilo.
Kamati ililiona hilo na kusema wazi kuwa hilo sio sahihi. Ni vema wachezaji wajue kuwa hilo sio jukumu lao.
2. Pili
Yanga, kwa mujibu wa mkataba, walikuwa na haki ya kumkata mchezaji
theluthi moja ya mshahara wake wa mwezi endapo atakosa mechi tatu au
zaidi. Yanga walimkata Okwi Mishahara ya miezi mitano, kinyume na
matakwa ya mkataba na pasipo maelelzo yoyote.
3. Yanga
na Okwi walikubaliana kuwa mchezaji atalipwa ada ya kusaini mkataba
(signing on – fee) ya US$ 100,000, kwa Awamu mbili. Awamu ya kwanza
wakati wa kusaini mkataba na awamu ya pili tarehe 27 Januari 2014. Mpaka
hivi sasa, Yanga wamelipa US$ 50,000 tu na bado kuna deni la US$
50,000. Huu ni uvunjaji wa mkataba wa wazi kabisa.
4. Kipindi chote mchezaji akiwa na klabu ya Yanga, hajapewa nyumba kama ambayo walikubaliana. Huu ni ukiukwaji mwingine wa mkataba.
Baada
ya Okwi kuanza kudai haki zake tajwa hapo juu, Yanga waliamua kutomlipa
mteja wetu mishahara ya miezi mitano kinyume na matakwa ya mkataba kati
yao.
MPANGO WA SIRI WA YANGA
Yanga
walikuwa na mpango wa siri wa kuvunja mkataba na Emmanuel Okwi ili
wamkomoe mteja wetu, ashindwe kucheza mpira, kiwango chake kiporomoke na
itumike kama onyo kwa wachezaji wengine ambao wanadai haki zao. Mpango
huu ulitekelezwe kama ifuatavyo:
a. Tarehe
27 Juni 2014, Yanga waliandika barua kwenda TFF, ikiitaka TFF, pamoja
mambo mengine, itambue kuwa mkataba kati yao na Okwi umefutwa. Barua
hiyo haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba
ambao unapaswa kufutwa.
b. Tarehe
25 Julai 2014, Yanga waliandika barua ya pili kukumbushia barua yao ya
tarehe 27 Juni 2014. Barua hiyo ya pili haikuwa na nakala kwa Okwi,
ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
c. Tarehe
20 Agosti 2014 Yanga waliandika barua nyingine tena wakikumbushia hoja
zao tajwa hapo juu. Kwa mara ya tatu, barua hiyo haikuwa na nakala kwa
Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
d. Yanga
waliandika barua nyingine ya nne tarehe 25 Agosti 2014 ikiwa na hoja
zile zile za kusitisha mkataba na mteja wetu. Kwa mara ya nne barua hiyo
haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba
ambao unapaswa kufutwa.
Baada
ya TFF kupanga tarehe ya kikao cha Kamati ya Sheria na hadhi ya
wachezaji na kutoa barua ya wito tarehe 27 Agosti 2014 ndipo kwa mara ya
kwanza mchezaji Emmanuel Okwi akafahamu kuwa Yanga wameomba kuvunja
mkataba wake.
Tarehe 27 Agosti 2014, Emmanuel Okwi aliiandikia Yanga KUKUBALI ombi lao la kuvunja mkataba.
Mambo muhimu ya kujiuliza ni:
Mosi,
Kama Mkataba ulikuwa ni kati ya Yanga na Okwi, ni kitu gani kiliifanya
Yanga ishindwe kumpa angalau nakala ya barua nne ambazo ilizipeleka TFF?
Pili, Wakati Yanga wanaomba kuvunja mkataba, walikuwa wameshamlipa Okwi stahili zake kwa mujibu wa Mkataba huo?
Tatu, Je visingizio vya kuvunjwa kwa mkataba wa Okwi vina uhusiano na idadi ya majina ya wachezaji wa kigeni wa Yanga?
Ni
bayana kuwa Yanga walitafuta kila aina ya kisingizio ili mteja wetu
aonekane kuwa ndio amevunja mkataba wakati ni wazi kuwa Yanga ndio
waliokuwa wa kwanza kuvunja mkataba huo tarehe 27 Januari 2014 kwa
kushindwa kumlipa mteja wetu US$ 50,000 za ada ya kusaini mkataba.
HOJA MBELE YA KAMATI
Mbele
ya Kamati Yanga walileta hoja kuwa: Hans Pope ana mgongano wa maslahi
kwa kuwa amemsajili Okwi Simba na yeye ni mjumbe wa Kamati hii; Okwi
amekataa kuongeza au kupunguza mkataba kama ilivyopendekezwa na Yanga;
Okwi ameleta madai yasiyo na msingi ya kutaka apewe nyumba ya kuishi;
hajacheza mechi 6 hivyo kuikosesha Yanga ubingwa. Okwi amefanya
makubaliano na Klabu ya Wadi Geldi ya Misri wakati ana mkataba na Yanga.
Hivyo basi Yanga waliitaka Kamati itamke kuwa mkataba kati yao na Okwi
umesitishwa, imfungie Okwi kucheza mpira Tanzania Maisha na ailipe Yanga
dola za kimarekani laki mbili.
Tukimwakilisha
Okwi, tulitoa hoja kuwa: Mteja wetu amekubali ombi la Yanga la kuvunja
mkataba ambalo limo katika barua zake nne; Yanga ndio wamevunja mkataba
kwa kushindwa kulipa signing fee US$ 50,000; Mishahara ya miezi mitano
US$ 15,000 na kodi ya nyumba US$ 2,800. Madai hayo ni kwa mujibu wa
mkataba.
Baada
ya Maswali toka kwa Kamati kwa pande zote mbili, Yanga waliomba kufuta
barua zao, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na kamati.
Kamati,
hatimaye ilifanya maamuzi ya kihistoria katika kulinda haki za
kimkataba za wachezaji kama ambayo imeelezwa hapo juu. Kwa mtu yoyote
mwenye akili timamu, anapaswa kuipongeza kwa dhati kamati kwa maamuzi
ambayo wanajenga mpira wa nchi hii. Vilabu vinapaswa kufahamu kuwa haki
za mchezaji lazima ziheshimiwe.
Hoja
za Yanga kuwa hakukuwa na madai ya fedha sio sahihi kwasababu Majibu
toka kwa Okwi na mabishano ya maneno mbele ya kamati hiyo ilijadili kwa
kina madai ya fedha ya Okwi na hata Yanga walikiri kutolipa madai hayo.
Hivyo basi si sahihi kusema kuwa eti suala la madai ya fedha
halikujadiliwa. (ona kiambatisho MNA1)
Msingi
wa malalamiko ya Yanga ni barua ya tarehe 27 Juni 2014, ambayo hakuna
sehemu ambayo inatamka suala la Simba. Kama kuna kesi dhidi ya Simba,
wasubiri wakati wa kupitia pingamizi za usajili lakini suala ambalo
Yanga walilalamikia ni kusitisha mkataba na Okwi na madai ya fidia.
Kamati
ya Sheria na Mwenyekiti wake hawana mamlaka ya kujadili uteuzi au uwepo
wa Hans Pope kwenye kikao hicho. Mamlaka ya Uteuzi ndio, kwa mujibu wa
katiba ya TFF, yenye uwezo wa kutoa uamuzi kuhusu suala hilo.
Kwakuwa rufaa ni haki ya kila mtu, Uamuzi wa kukata rufaa Fifa / CAS ni haki ya kisheria lakini tuwakumbushe Yanga kuwa “UKITAKA HAKI, TENDA HAKI KWANZA”.
“Imeandikwa
na Dk. Damas Daniel Ndumnbaro (PhD) wa kampuni ya Maleta & Ndumbaro
Advocates, ambao ni Mawakili wa Mchezaji Emmanuel Okwi”
No comments:
Post a Comment