Meneja wa klabu ya Man utd Louis van Gaal, ameahidi kuingia sokoni na kufanya usajili wa wachezaji mara atakaporejea nchini Uingereza, ambapo itakua ni siku chache kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi nchini humo.
van Gaal, amesema ipo haja ya kufanya hivyo baada ya kubaini mapungufu ya baadhi ya wachezaji wake ambao amewasoma katika kipindi chote cha maandalizi ya msimu mpya wakiwa nchini Marekani.
Hata hivyo van Gaal, amesema pamoja na kutarajia kufanya hivyo bado suala la nani anaondoka kikosini kwake ama anabaki, litaendelea kuwa moyoni mwake na atalifanya kuwa siri mpaka utakapowadia wakati wa majina ya atakaowaacha kutolewa katika vyombo vya habari.
Amesema atakachokifanya mara baada ya kurejea Old Trafford ni kuzungumza na mchezaji mmoja baada ya mwingine na kumueleza ukweli kama yupo katika mipango yake ama la, na katu hatofanya hivyo kupitia vyombo vya habari ambavyo kila leo vimekua vikidadisi kwa kutaka kufahamu ni nani anaondoka ama anasajiliwa kwenye klabu ya Man Utd.
Hata hivyo pamoja na Louis van Gaal, kuahidi kufanya maamuzi ya kuwacha wachezaji kwa siri baada ya kufanya nao mazungumzo binafsi atakaporejea mjini Manchester, tayari gazeti la The Mirror la nchini Uingereza hii leo limetoka na habari za wachezaji ambao wapo kwenye wimbi la kuondoka Old Trafford.
Wachezaji waliotajwa katika wimbi hilo kupitia gazeti la The Mirror ni Marouane Fellaini, Luis Nani, Shinji Kagawa, Wilfried Zaha pamoja na Anderson ambaye msimu uliopita alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Fiorentina ya nchini Italia.
No comments:
Post a Comment