Kipa wa Yanga, Juma Kaseja amehitimu
mafunzo ya awali ya ualimu wa mpira wa miguu na kupata alama ya daraja A
katika mafunzo yaliyoanza Mei 5 mwaka huu na kumalizika jana katika
Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi katika ukumbi wa Bwalo la Umwema la JWTZ, Mkufunzi wa mafunzo hayo
Meja Mstaafu Abdul Mingange amesema Juma Kaseja ni miongoni mwa
wanafunzi 34 waliomaliza kozi hiyo huku watatu kati yao wakipata alama
ya daraja la A.
Mingange amesema waliopata daraja A
ni Kaseja, Emmanuel Majengo na Richard Ngwanda baada ya kufanya vizuri
katika mitihani ya darasani na vitendo vya uwanjani.
“Juma Kaseja amepata alama ya daraja A
na wengine wawili, huku waliopata daraja B ni 16 na watano walipata
daraja C,”amesema Mingange.
Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa
Morogoro (MRFA), Hamis Semka (kulia) akimkabidhi cheti mlinda mlango wa
klabu ya Yanga, Juma Kaseja baada ya kuhitimu mafunzo ya awali ya
ualimu wa mpira wa miguu na kupata alama ya daraja A katika hafla
iliyofanyika Bwalo la Umwema, Morogoro. Picha na Juma Mtanda
Mkufunzi huyo amesema kuwa vitu
walivyojifunza kwa siku 10 katika mafunzo hayo ni pamoja na mpira
kinadharia na vitendo, sheria 17 za mchezo wa soka na matibabu ya
wanamichezo.
“Kila muhitimu tumempatia CD za
kufundishia na vitabu vya muongozo wa namna ya kufundisha mchezo wa soka
na baada ya miezi sita wanaruhusiwa kuchukua kozi ya pili kujifunza
zaidi,”amesema Mingange.
Akizungumzia juu ya kuchukua mafunzo
ya kozi ya awali ya ualimu wa soka, Kaseja amesema amekuwa akifanyishwa
mazoezi ya soka, lakini hakuwa anaelewa ni kwa nini anafanyishwa mazoezi
na faida yake, baada ya kupata mafunzo hayo hivi sasa anaelewa faida
yake.
Kaseja alisema kwa sasa anajua mambo
mengi ikiwamo kupanga programu za kufundisha mchezo wa soka na sheria za
soka ingawa baadhi alikuwa akizifahamu.
“Wenzetu wachezaji wa Ulaya jambo
hili siyo geni, tumeshuhudia Ryan Giggs wa Manchester United akicheza
soka na kufanya kazi ya ukocha, hili linafaa kuigwa kwani moja ya faida
ya kupata mafunzo ya ukocha huku unacheza ni kufahamu mambo mengi ndani
ya soka kwani yatakuepusha kufanya makosa yatakayoigharimu timu,”amesema
Kaseja.
Kaseja amesema baada ya kuhitimu kozi
hiyo ya awali dhamira yake siyo kuacha soka ila ni kuongeza ujuzi na
kuwataka wachezaji wenzake kufanya uamuzi wa haraka wa kupata kozi hiyo.
“Sina mpango wa kustaafu soka leo
wala kesho eti kwa sababu nimehitimu mafunzo haya ya ualimu wa soka,
naongeza ujuzi tu kwani siku za usoni nitaamua niendelee na soka au
nifanya mambo mengine nje ya soka,”amesema Kaseja.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment