Uchaguzi Mkuu wa TASWA wasogezwa mbele sasa kufanyika Machi 2
UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Waandishi
wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 16
umesogezwa mbele kwa wiki mbili na sasa utafanyika Machi 2, mwaka huu jijini Dar
es Salaam.
Uamuzi wa kusogeza
mbele tarehe ya kufanyika uchaguzi huo imechukuliwa na Sekretarieti ya TASWA
kutokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kutoa nafasi kwa wanachama wengi
zaidi kulipia ada zao kwa ajili ya kushiriki mkutano huo wa uchaguzi.
Hadi kufikia leo
mchana idadi ya wanachama waliokuwa wamelipia ada ni 57 kati ya wanachama
karibu 150 waliopo katika leja na kati ya waliolipa ni wanne tu ndiyo wamelipia
ada ya miaka mitatu kama walivyotakiwa wakati waliobaki wamelipia mwaka mmoja.
Kumekuwa na
changamoto mbalimbali zimejitokeza katika suala hili la kulipia ada, ikiwa ni
pamoja na maombi ya baadhi ya wanachama walipie mwaka mmoja na kisha ada
nyingine chama kiwawekee utaratibu wa kulipa siku za usoni kadri
itakavyoonekana inafaa.
Kutokana na hali
hiyo sekretarieti ya TASWA imepokea maombi hayo na kwa vile uamuzi huo ulifikiwa
na kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA, itayawasilisha kwenye kikao kama
hicho kitakachofanyika Jumatatu Februari 17 kujadili masuala mbalimbali
yahusiyo mkutano huo, ikiwa ni pamoja na kupitia orodha ya wanachama
wanaostahili kushiriki mkutano wa uchaguzi.
Hatua ya awali
ambayo imefanyika ni kusogeza mbele tarehe ya mwisho ya kulipia ada, ambayo
awali ilikuwa Februari 4 na sasa itakuwa Februari 15 mwaka huu saa kumi alasiri
na hakutakuwa na muda wa ziada.
Imetolewa na;
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
07/02/2014.
No comments:
Post a Comment