Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameelezea hatua
zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ilani yake siku 100 tangu alipoingia
madarakani.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo (Februari 7 mwaka huu) katika mkutano uliofanyika
katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi aliainisha
maeneo kadhaa yaliyopewa kipaumbele na tayari yameanza kufanyiwa kazi pamoja na
changamoto zilizopo.
Alisema
muundo wa Idara ya Ufundi umebadilishwa kwa kuundwa vitengo vya ufundi, elimu
na maendeleo ya mpira wa miguu huku maeneo ambayo tayari yameanza kufanyiwa
kazi kuwa ni;
Ujenzi
wa kituo cha mpira wa miguu (football centre of excellency), timu kupanda
daraja, kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani, mpira wa miguu wa
wanawake, maandalizi ya vijana (grassroot football), tiba, walimu na makocha,
utawala, uhusiano na Zanzibar, klabu za mpira wa miguu, wachezaji, masoko na
uwekezaji, kitengo cha habari, viwanja na timu ya Taifa (Taifa Stars).
Rais
Malinzi amesema changamoto zilizopo kwa sasa ni matumizi ya tiketi za
elektroniki, ufinyu wa bajeti, madeni, nidhamu, maadili na uchezeshaji wa
waamuzi.
Ametoa
mwito kwa wadau wote nchini wakiongozwa na Serikali, Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF), Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), vyombo
vya habari, mashirika ya umma na kampuni binafsi kushikamana na kuwa kitu
kimoja kwa nia ya kuinua kiwango cha mpira wa miguu Tanzania.
TANZANIA FOOTBALL
FEDERATION
TAARIFA
YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI
YA
RAIS WA TFF
Ndugu zangu,
Uchaguzi
mkuu wa TFF ulifanyika tarehe 27 Oktoba, 2013 na kukamilika alfajiri ya tarehe
28 Oktoba, 2013 ambapo Kamati ya Utendaji ya TFF ilitangazwa rasmi na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF Ndugu Hamidu Mbwezeleni.
Katika
kuelekea uchaguzi mkuu huo niliitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo
nilitangaza ilani yangu ya uchaguzi.
Lengo la ilani ilikuwa ni kuwaeleza wadau na wapenzi wa mpira wa miguu
Tanzania dira ambayo ingeongoza mpira wetu iwapo ningechaguliwa kuwa Rais wa
TFF. Aidha niliahidi iwapo
ningechaguliwa tungekutana katika chumba hiki hiki baada ya siku 100. Ninapenda nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa
Mkutano Mkuu wa TFF, walionipa kura na ambao hawakunipa kura, kwa kukamilisha
vyema zoezi la uchaguzi huo. Uchaguzi
umekamilika kazi iliyobakia mbele yetu ni kutekeleza majukumu yetu kama viongozi
wa mpira miguu Tanzania.
Ilani na Utekelezaji
wake
Ilani
yangu ya uchaguzi iliainisha maeneo kadhaa ya kupewa vipaumbele. Nitakumbushia maeneo haya na kueleza hatua
tulizofikia katika utekelezaji wake:
1.
Idara
ya Ufundi
1.1
Kikao cha Kamati ya Utendaji
kilichokaa tarehe 23 Novemba, 2013 pamoja na mambo mengine kilipitisha muundo
mpya wa Sekretariati ya TFF. Muundo huo
unaelezwa katika chati hii hapa chini:
Commercial
Manager
|
Media Officer Chief
Security Officer
Katika
muundo huu Idara ya Ufundi imepanuliwa
kwa kuundwa vitengo vya Ufundi,Elimu na Maendeleo ya mpira.
Aidha
katika kutekeleza azma ya kuboresha usimamizi wa mpira wa vijana (Youth
Football) Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limeamua kuajiri Desk Officer
wa vijana yaani msimamizi maalum wa mpira wa vijana na tayari ameajiriwa.
Zoezi
la kuimarisha Idara ya Ufundi kwa kuajiri Mkurugenzi wa Ufundi pamoja na
Wakurugenzi wake Wasaidizi linaendelea.
1.2
Ujenzi wa Kituo cha Mpira
(Football Centre of Excellency)
Limekuwa
ni jambo la kufurahisha na kutia moyo kuwa mara baada ya kuingia madarakani
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilitufahamisha
juu ya uamuzi wa Serikali, kwa kushirikiana na Kampuni ya SYMBION ya Marekani
na Klabu ya Mpira ya SUNDERLAND ya Uingereza, wa kujenga kituo cha michezo
(Sports Centre) Kidongo Chekundu , Ilala na kujenga kituo cha kulea na kukuza
vipaji vya vijana (Elite Academy) Wilayani Kinondoni. Wizara ilinikutanisha na Uongozi wa SYMBION
na mazungumzo yanaendela kuona ni jinsi gani mradi huu utashirikisha Serikali,
Mshirika wetu SYMBION, Klabu ya SUNDERLAND na TFF ambao kwa mujibu wa katiba
yetu ndio waratibu na wasimamizi wa
maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.
Vikao kadhaa vimefanyika na mwelekeo ni mzuri sana. Tunaamini mradi huu utatoa mchango mkubwa
sana katika kuendeleza mpira wa vijana (Youth Football).
Aidha
kamati ya utendaji ya TFF imeviagiza vyama vyote vya mpira vya mikoa kuomba
kumilikishwa viwanja vikubwa katika
maeneo mapya yanayopimwa, TFF italipia malipo yote yatakayotakiwa. Mkoa
wa Tanga tayari wametekeleza agizo hili na hati imekwisha toka.Msanifu tayari
anaanda michoro ya awali kwa ajili ya kujenga kituo cha michezo katika ardhi
hii. Mfano wa mchoro wa kituo hiki ndio utakaotumika nchi nzima iwapo
utapitishwa na kamati ya utendaji.
1.3
Timu Kupanda Daraja
TFF
tayari imeunda Kamati ya dharura (Adhoc) ya kuangalia mapungufu yaliyopo katika
utaratibu wa sasa wa kuwa na timu 14 za Ligi Kuu na 24 za Ligi Daraja la Kwanza
ili tuone ni kwa jinsi gani tutaweza kuboresha Ligi yetu. Ripoti ya Kamati ikikamilika italetwa mbele
ya Kamati ya Utendaji kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.
1.4
Kuanzisha Mashindano Mapya na
Kufufua ya Zamani
Juhudi
zinaendelea kuhakikisha mashindano ya Kombe la Taifa yanafufuliwa. Aidha taratibu za kuanzisha upya Kombe la
Shirikisho (Federation Cup) ambalo litakuwa ni la mtoano nchi nzima zimefikia hatua nzuri na muda si mrefu
taratibu zake zitatangazwa pindi mshirika wetu atakapokuwa amemaliza maandalizi
upande wake.
1.5
Mpira wa Wanawake
1.5.1
Katika kuhakikisha mpira wa
wanawake unatengenezwa mkakati maalum wa maendeleo matayarisho ya mpango wa maendeleo
ya mpira wa wanawake (women football development plan) yamekamilika na
yatawasilishwa katika kikao kijacho cha Kamati ya Utendaji kwa ajili ya maamuzi
ya mwisho. Mpango huu utatoa dira ya
maendeleo ya mpira wa miguu kwa miaka mitano ijayo na utakuwa ni sehemu ya mpango kazi wa TFF wa miaka mitano.
1.5.2
TFF inayo furaha pia kuufahamisha
umma wa wapenda mpira wa Tanzania kuwa shula ya kukuza na kuendeleza vipaji ya
Alliance Mwanza kwa kutambua mapungufu yaliyopo katika kuendeleza mpira wa
wanawake kuanzia mwaka huu imeanzisha mafunzo maalum ya mpira wa watoto wa kike
umri chini ya miaka 10. Matunda yake
tutayaona baadaye. Hawa watakuzwa na kulelewa pamoja.
1.5.3
Jitihada zinafanyika kuanza
mashindano ya kitaifa ya wanawake na muda si mrefu utaratibu wake utatangazwa
baada ya mshirika wetu kumaliza maandalizi yake.
1.5.4
TFF kwa kushirikiana na
Wizara ya Wanawake na Jinsia ipo katika
kuandaa mpango kazi wa kushirikiana na vyuo 55 vya Ustawi wa Jamii Tanzania
katika kuanzisha masomo maalum kwa wasichana katika vyuo nchini, masomo ambayo
yatahusisha ufundishaji wa mpira wa wanawake, urefa, ukocha na utawala wa
mpira. Lengo ni kutoa fursa kwa
wasichana kujifunza stadi hizi kama sehemu ya masomo yao katika vyuo vya
maendeleo ya jamii. Utaratibu wa mpango
huu unasimamiwa na chama cha mpira wa migu wa wanawake (TWFA) na taasisi
nyingine husika.
1.5.5
Pamoja na ufinyu wa bajeti
tulionao na timu zetu za wanawake kutokuwa na udhamini TFF bado inahakikisha
timu zetu za wanawake zinashiriki michuano yote ya kimataifa.Wiki iliyopita
timu yetu ya Taifa ya wanawake imesajiliwa kushiriki mtoano wa kushiriki
fainali za All Africa games Congo Brazzavile 2015.
1.6
Maandalizi ya Vijana (Grassroot Football)
Mpango
kazi wa maendeleo ya mpira wa miguu wa vijana Tanzania (Tanzania youth development plan) maandalizi yake yamekamilika na utazinduliwa
muda si mrefu. Vipaumbele vikuu vya
mpango huu ni pamoja na:
1.6.1
Kuhakikisha shule zote za
msingi 16,000 za Tanzania zinakuwa na viwanja vya kuchezea mpira, mwalimu
mmoja wa mpira na zinapata kwa mwaka angalau mipira 10 ya size 3 na 4
pamoja na jozi angalau 30 za viatu.
TFF
tayari inawasiliana na Mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili
yatukusanyie vifaa vya mpira vilivyotumika (has viatu) ili viweze kuletwa na
kugawiwa kwa watoto wetu kwenye shule za msingi na academies. Kwa sasa tayari kontena mbili za vifaa hivi
zimekwisha kusanywa nchini Uingereza na
utaratibu wa kuzileta unafanyika. Lengo
ni kuingiza nchini jozi za viatu 500,000 kwa mwaka na mipira 160,000 ya size 3
na 4 kwa mwaka. TFF inaomba ushirikiano
wa Serikalini, Taasisi za Umma, Makampuni Binafsi na Taasisi zisizo za
kiserikali katika kuhitimisha azma hii.
1.6.2
TFF ilipata fursa ya kukutana
na Balozi wa Uholanzi hapa nchini na kufanya naye mazungumzo. Nia na lengo ilikuwa ni kuangalia ni kwa
jinsi gani Uholanzi inaweza kutusaidia kufundisha walimu wa walimu (trainer of
trainers). Matumaini yetu ni kuwa walimu
hawa wakishafuzu watakuwa na jukumu la
kuwafundisha walimu wa michezo wa shule za msingi kwa kushirikisha vyuo vya walimu
vinavyotoa taaluma hii kama Malya, Murutunguru na Butimba.
1.6.3
TFF kwa kushirikiana na
taasisi isiyo ya kiserikali inaangalia uwezekano wa kujenga vituo vya michezo
169 katika Wilaya zote 169 Tanzania.
Vituo hivi pamoja na kufundisha mpira vitakuwa pia ni vituo maalum vya
kuwafundisha vijana juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya.
1.6.4
TFF kupitia Idara yake ya
Ufundi na Kamati ya Vijana iko mbioni kufanya sensa ya vituo vya kukuza na
kulea vipaji vya vijana (Academies) pamoja na vituo vya mpira (Sports Centres)
nchini kote Tanzania. Utaratibu
unafanywa wa kuweka vigezo vya kutambuliwa vituo hivi na TFF itaanzisha
utaratibu wa kusajili na kutoa vyeti vya usajili kwa vituo vitakavyokidhi
vigezo. Lengo ni kuweka utaratibu nchini
wa kusimamia na kuendeleza vituo hivi kitaifa.
1.6.5
Mpango wa muda mfupi wa TFF
ni kuandaa timu ya Taifa ya vijana itakayoshiriki mashindano ya Fainali za
Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
Tanzania tumeomba uenyeji wa Fainali hizi. Mwaka huu wa 2014 TFF itafanya mashindano
maalum ya vijana chini ya umri wa miaka 12 ili kuunda timu ya Taifa ya kuanzia
ya U12, timu ambayo itakua pamoja kuelekea 2019. Malengo ni kuiboresha timu hii kila mwaka kwa
kuongeza vijana U13 mwaka 2015, U14 mwaka 2016, U15 mwaka 2017 na mwishowe U16
mwaka 2018.TFF imekwisha pata mshirika wa mpango huu na akimaliza maandalizi
yake atatangazwa rasmi.
1.6.6
Ili Tanzania ifundishe mpira
unaofanana nchini kote, utaratibu unafanyika wa kuandaa mtaala wa kufundisha
mpira (National football curricullum).
Mtaala huu unaandaliwa na Idara ya Ufundi ya TFF kwa kusaidiana na
Mtaalam wa mpira toka Uholanzi. Mtaala
huu ukikamilika utakuwa nyenzo muhimu ya kufundishia mpira mashuleni na kwenye
Academies.
1.7
Tiba, Waalimu na Makocha
TFF imeandaa
mpango wa kukutana na wenyeviti wa vyama vya Tiba, Waamuzi na Makocha ili
kupanga nao mikakati ya maendeleo ya kitaaluma.
Mikakati hii ikiwa tayari itajumuishwa katika mpango mama wa maendeleo wa TFF (TFF National Business
Plan), mpango ambao maandalizi yake yatakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
1.8 Utawala
TFF
imeanza kwa kuboresha mazingara ya utendaji wa kazi. Vyama shiriki TAFCA, FRAT, TASMA, TWFA na
SPUTANZA tayari vimepatiwa ofisi za kisasa katika eneo la Ilala. Ofisi kuu za TFF nazo ziko mbioni kuhamia
katika jengo la kisasa la PPF Tower,nia ikiwa ni kuiwekea sekretariet ya TFF
mazingira ya kisasa ya kufanyia kazi na pia kupisha ujenzi wa kitega uchumi
eneo letu la Uwanja wa Karume.
Aidha
TFF imeunda kamati maalum (Adhoc) ya kupitia Muundo wa Bodi ya Ligi lengo
likiwa ni kutekeleza maagizo ya Mkutano Mkuu wa TFF ulioagiza Bodi ya Ligi
iundwe ikiwa ni ya mpito kuelekea uundwaji wa Kampuni ya kuendesha Ligi Kuu ya
mpira wa miguu.
1.9 Mahusiano na Zanzibar
Mahusiano
kati ya TFF na Chama cha mpira Zanzibar (ZFA) yamezidi kuimarishwa kufuatia
ziara kadhaa ambazo tumezifanya kati ya maeneo yetu mawili. Mipango ya kuimarisha timu zetu za Taifa za
wakubwa, za vijana na za wanawake inafanywa kwa pamoja. Juhudi za kuhakikisha Zanzibar inajiunga na
FIFA pia zinaendelea kupitia mazungumzo na wahusika.
1.10 Vilabu
vya Mpira
Mara
baada ya kuingia madarakani Uongozi wa TFF ulikutana na viongozi wa vilabu
vyote vya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.
Kikao hiki kilifanyika kama sehemu ya kuangalia ni maboresho gani yafanyike
ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Ligi zetu. Utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho unaendelea
kupitia wahusika mbalimbali.
1.11 Wachezaji
SPUTANZA
wameleta TFF mapendekezo yao ya jinsi ya kuboresha maslahi ya wachezaji wa
mpira wawapo mpirani na baada ya kustaafu kucheza soka. TFF inayafanyia kazi mapendekezo hayo. Lakini kubwa litakuwa ni kuanzisha Mfuko
Maalum (Trust Fund) utakaochangiwa na wachezaji wakiwa bado wanacheza pamoja na
TFF na taasisi nyingine ili mfuko huu uwasaidie pindi wakistaafu.
1.12 Masoko
na Uwekezaji
Kama
nilivyoeleza hapo juu TFF iko mbioni kuwekeza katika Kiwanja cha Karume, lakni
pia njia nyingine za kuiongezea TFF mapato ziko mbioni kuanzishwa ikiwa ni
pamoja na kuanzisha utaratibu maalum wa kuuza jezi za Timu ya Taifa (replica
shirts).
1.13 Kitengo
cha Habari
TFF
imeandaa utaratibu wa kuboresha kitengo hiki kwa kukiongezea nguvu kazi ili
upashanaji wa habari uwe ni wa haraka zaidi ikiwa ni pamoja na TFF kuanzisha
Blog yake,kuboresha Tovuti yake, na kuwa
na kurasa kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, Twitter, n.k.
Press officer ataajiriwa punde ili kuimarisha kitengo hiki.
1.14 Viwanja
Wakati
tunaingia madarakani FIFA kupitia mpango wake wa maendeleo ilikuwa imekwisha tenga pesa kwa ajili ya kuweza nyasi bandia
uwanja wa kihistora wa Nyamagana jijini
Mwanza. Uongozi wetu kwa kushirikiana na
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza na Meya wa Manispaa ya Mwanza tulifuatilia kwa karibu na kufanikiwa
kuondoa dosari zilizokuwa zimekwamisha mradi huu. Utandazaji wa nyasi bandia utaanza mara moja
kuanzia sasa.
Kwa
mafanikio haya Tanzania tuna viwanja vyenye/ vitakavyokuwa na nyasi bandia baadae
ambavyo ni Gombani Pemba, Amani Zanzibar,Uwanja wa Uhuru, Uwanja wa Karume,
Uwanja wa Azam Chamazi na Uwanja wa Nyamagana.
TFF
iko mbioni kuanza mazungumzo na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo ni wamiliki
wa viwanja kadhaa vya mpira ili kuangalia uwezekano wa kuingia ubia kwa nia ya
kuviendeleza.
1.15 Timu
ya Taifa (Taifa Stars)
Ili
kuandaa mkakati maalum wa kuboresha timu ya Taifa TFF iliitisha kikao maalum
cha walimu wa mpira waandamizi. Kikao
hiki kilifanyika Zanzibar kati ya tarehe 06-07 Desemba, 2013 na kilitoka na
maamuzi kadhaa. Tarehe 18-19 Januari,
2014 TFF iliitisha kikao kingine maalum cha Makatibu 30 wa vyama vya mpira vya
mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ajenda ikiwa ni uboreshaji wa Timu ya
Taifa (Taifa Stars). Matunda ya vikao hivi ni mpango kazi maalum
ulioandaliwa wa kuboresha timu ya Taifa
kwa kushirikiana na washirika wetu Tanzania Breweries ltd kupitia bia yao ya
Kilimanjaro Lager. Mpango huu utatangazwa rasmi wiki ya pili ya mwezi February 2014.
CHANGAMOTO:
Uongozi mpya tangia umeingia madarakani
umekutana na changamoto kadhaa. Baadhi yake ni kama hizi zifuatazo:
1.Tiketi
za Elektronik.
Uongozi mpya ulipoingia madarakani ulikuta
awamu iliyopita ilikwisha saini mkataba wa mradi huu.Jukumu la uongozi wangu ni
kutekeleza masharti ya mkataba. Changamoto nyingi zimejitokeza ikiwa ni pamoja
na mitambo kuzima mara kwa mara,mitambo kufanya kazi kwa spidi ndogo , mageti
yaliyofungwa mashine hizi kuwa machache (mfano Mkwakwani yamefungwa mitambo miwili
katika uwanja unaoingiza watu zaidi ya elfu kumi,uwanja wa Taifa mitambo 48 wakati
unaingiza watu 60,000,linganisha na uwanja wa Emirates London unaoingiza watu 60,000
mitambo imefungwa 125,karibia mara tatu ya uwanja wetu wa Taifa). Pia uelewa
mdogo wa wadau kuhusu taratibu za utumiaji tiketi hizi nao ni tatizo na mkataba
wa TFF na CRDB unaitaka TFF ibebe jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu
matumizi ya tiketi hizi na bajeti yake
haipungui shilingi milioni 500 ikijumuisha gharama za matangazo kwenye
radio,magazeti,televisheni,roadshows,mabango,vipeperushi n.k. Matokeo yake
yalikuwa ni vurugu katika baadhi ya viwanja, vurugu ambazo kama si busara za
TFF zingeweza kusababisha maafa.Mazungumzo yanaendelea kati ya TFF na mzabuni
CRDB ili kutafuta namna ya kuboresha
utaratibu wa mfumo wa tiketi za elektronik,lakini pia ni kuangalia ni kwa jinsi
gani tiketi hizi hazigeuki kuwa mzigo kwa mlaji maana licha ya watazamaji
kulipia gharama ya tiketi yenyewe lakini bado kuna asilimia inakatwa kama
kamisheni ya uwakala jambo ambalo pia ni mzigo kwa vilabu.TFF ina nia thabiti
ya kutumia utaratibu huu,ni mzuri iwapo utatekelezwa kwa taratibu stahili.
- Ufinyu wa bajeti
TFF
katika kutimiza majukumu yake inahitaji pesa nyingi hasa kuendeleza mpira wa
vijana, kukidhi gharama za kuendesha ofisi, kuvipa nguvu vyama wanachama na kusimamia
timu zake nane za Taifa (Za wakubwa mbili wanawake/wanaume,U17 mbili,U20 mbili
na za olimpiki mbili).Eneo lenye ufadhili mkubwa ni timu ya Taifa ya wanaume
tu.Hivyo ni dhahiri mahitaji ya fedha TFF ni makubwa sana na vyanzo
havikidhi.Jitihada zinafanyika kuhakikisha tunaongeza vyanzo mbadala wa mapato.
- Madeni
Madeni
ambayo uongozi mpya ulipoingia madarakani uliyakuta ni makubwa na yamelielemea
shirikisho. Juhudi za kuongea na wanaotudai ili aidha watupunguzie madai yao au
tuyalipe kwa masharti nafuu yanaendelea.Wale wote wanaotudai ambao wametuelewa
katika hili tunawashukuru sana. Kwa sasa kesi zote za madai dhidi ya TFF zilizokuwa mahakamani zimeondolewa baada ya
mapatano.
- Nidhamu
Nidhamu
bado ni tatizo si kwa wachezaji bali hata kwa viongozi wetu.Yupo mchezaji
amediriki kupigana na walinzi wa raia na wengine wakadiriki kumpiga mwamuzi,hili
halikubaliki na hatua kali zitakuwa zinatolewa dhidi ya watovu wa nidhamu bila
kujali wao ni kina nani kwenye mpira wa nchi hii.
- Maadili
Wizi
mdogo mdogo hasa wa mapato ya milangoni umeendelea.TFF tumekuta kesi za wizi wa
aina hii zaidi ya hamsini zilizoripotiwa polisi Chang’ombe na watuhumiwa
hawakuwahi kupelekwa mahakamani kwa kuwa mlalamikaji (TFF) hakujitokeza
kuandika taarifa (statement). Uongozi wangu umeamua utakuwa unafuatilia kwa
karibu kesi hizi ili kukomesha tabia iliyozoeleka ya udokozi.Pesa ya mpira
itumike kwenye mpira.
- Maamuzi uwanjani (Refeering)
Wapo
waamuzi wanaokosea kwa makosa ya kibanadamu, hao tunawaelewa.Lakini zinapotokea
tetesi au tuhuma za haki kutotendeka kiwanjani kwa sababu nyingine zaidi ya hii
shirikisho linashtuka sana na kamwe halitakubali lidhalilike kwa tuhuma kama
hizi.Shirikisho kwa sasa linafuatilia kwa karibu kinachoendelea uwanjani ili
kuhakikisha haki inatendeka kwa timu zote. Tayari mitihani imekwisha fanyika
kupandisha madaraja waamuzi mbali mbali ili kuongeza uwigo wa kupata
waamuzi.Kozi za waamuzi zitaendelea kutolewa ili kuzidi kunoa uwezo wao.
Aidha
vituo vya kuendeleza waamuzi vijana vya kambi ya Jenerali Twalipo na Alliance
academy Mwanza viko mbioni kuimarishwa ili viwe na nguvu zaidi ya kufundisha waamuzi vijana.
HITIMISHO
Ndugu
zangu nihitimishe kwa kutoa wito kwa wadau wote wa Mpira wa Miguu Tanzania
wakiongozwa na Serikali, CAF, FIFA,
CECAFA, vyombo vya habari, Mashirika ya Umma, Mashirika yasiyo ya Kiserikali,
Makampuni na watu binafsi wote kwa pamoja tushikamane kwa pamoja tukiwa na nia
moja tu, kuinua kiwango cha mpira Tanzania na kuzifanya timu zetu za mpira ziwe
za wakubwa, za wanawake na za vijana
ziwike, sio tu barani Afrika, bali
duniani pote. Kwa pamoja tunaweza.
Tukijaliwa
tutakutana tena ndani ya chumba hiki hiki baada ya siku 365 tangia
nimechaguliwa kuongoza TFF ili tufanye tathmini ya mwaka mmoja wa uongozi
wangu.
Mungu
ibariki TFF
Mungu
Ibariki Tanzania
Mungu
ibariki Afrika
Jamal
Malinzi
Rais wa TFF
07
Januari, 2014
No comments:
Post a Comment