LONDON, England
WADAU wa soka Manchester United
wamemkingia kifua kocha wao, David Moyes wakisema kuwa kuchelewa kumkabidhi
timu hiyo ndicho chanzo cha kufanya vibaya mwanzo wa msimu huu.
Wadau hao ndani ya timu hiyo,
walisema jana kuwa klabu hiyo ilipaswa kununua mkataba wa Moyes wakati akiwa
bado yupo Everton, ili kumuwezesha
kufanya kazi ya kusajili wachezaji aliowahitaji badala ya kumkabidhi timu hiyo
ya Old Trafford, Julai mosi mwaka huu.
Kauli ya wadau hao imekuja wakati
klabu hiyo ikijiandaa kumpa kila msaada ambao kocha huyo anauhitaji ili kuweza
kutatua matatizo yake wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari,
wamiliki hao wa Man United, wanajiandaa kumsaidia Moyes wakati wa usajili huo wa dirisha dogo
litakapofunguliwa mapema Januari mwakani, ili kuhakikisha kocha huyo wa klabu
hiyo ya Old Trafford anaondokana na kipindi kigumu alichopo katika msimu wake
wa kwanza.
Vyanzo hivyo vinaeleza kuwa baada ya
timu hiyo kutotumia fedha nyingi chini ya
Moyes, vigogo hao watafanya kufuru wakati wa usajili huo wa Januari kwa
kununua wachezaji kama beki wa timu ya Everton,
Leighton Baines na kiungo wa timu ya Atletico Madrid, Ander Herrera
ambao wanampasua kichwa Moyes.
Kipigo cha Jumamosi ilichoambulia ikiwa
nyumbani dhidi ya timu ya West Brom, kimeifanya Manchester United kuning’inia kwenye nafasi ya 12 ya msimamo wa
ligi, huku ikiwa imeshachapwa mara tatu kwenye ligi hiyo na Moyes ameshakiri
kuwa timu yake ina tatizo la ukosefu wa wachezaji nyota duniani.
Mbali na wamiliki hao, pia nyota wa zamani wa timu
hiyo Gary Naville amewatabiria mabaya
nyota wa timu hiyo akisema kuwa watatupiwa virago kabla ya Kocha Mkuu wa timu
hiyo, Moyes kufukuzwa.
No comments:
Post a Comment