TIMU ya Taifa ya wasichana waliochini ya miaka 20, jana
ilipokea kichapo cha mabao 3-1 toka kwa timu ya wavulana ya Karume Kombaini ya
U-16 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mchezo huo ambao ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo
wa kutafuta kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji utakaochezwa Oktoba 26
mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Katika mchezo huo timu ya Taifa ya wanawake ndio ilikuwa ya
kwanza kupata bao katika dakika ya pili lililofungwa na mshambuliaji Neema
Paulo kabla ya Abdul Biteko kuisawazishia timu yake ya Kombaini katika dakika
ya saba matokeo yaliyodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko
lakini kombaini ndio walionufaika baada ya kuongeza mabao mawili yaliyofungwa
na Abdul Biteko katika dakika ya 70 na 81 na kufanya matokeo kuwa 3-1.
Pamoja na kufungwa timu ya taifa ya wasichana walicheza
mchezo mzuri na wa kuvutia na kuwapa matumaini mashabiki waliofurika uwanja
hapo kufanya vizuri katika michezo yao
ya kutafuta kufuzu Kombe la Dunia.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa timu ya Taifa ya wanawake, Rogasian Kaijage, alisema timu yake imecheza vizuri na anaamini wafanya vyema kwenye michezo inayowakabili licha ya kutopata mechi za kirafiki za kimataifa.
“Timu yangu imecheza vizuri na naamini itafanya vema katika
mashindano yanayotukabili pia nawaomba watanzania watupe sapoti kwa kufika kwa
wingi uwanjani kutushangilia”, alisema Kaijage.
Fainali za Dunia za U-20 kwa
wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hii,
raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana
na Zimbabwe na ikifanikiwa kupita Tanzania itashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya Kombe la
Dunia kwa wasichana.
No comments:
Post a Comment