Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiomba
Serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya mpira wa
miguu ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda kwa
mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji.
Timu hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani Pwani
chini ya Kocha Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya
kwanza itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya
TFF, Lina Kessy amesema hiki ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo ili
iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Ameitaka jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo
haina mdhamini wala mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya
kusubiri ifanye vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.
Kessy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa
Miguu wa Wanawake Tanzania
(TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa fursa ya kambi kwani timu hiyo
hailipii malazi badala yake inalipia huduma nyingine inazopata hapo.
Vilevile amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa
wakijitolea kutokana na ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira wa miguu
wa wanawake kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.
“Shukrani za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao
wachezee timu ya Taifa, kwani wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa
wazazi. Pia tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia
wachezaji wetu,” amesema.
Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika
mwakani nchini Canada.
Iwapo Tanzania itaitoa
Msumbiji katika raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe.
No comments:
Post a Comment