Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, September 18, 2013

WILLIAM MTITU WA BONGO MUVI ATOA LA MOYONO KUHUSU STEPS ENTERTAINMENT

BILA STEPS INAWEZEKANA

Kwa muda mrefu nimekuwa nikiulizwa sababu ya kuamua kusambaza filamu zangu mwenyewe badala ya kuzipeleka kwa wasambazaji ambao nilikuwa nikifanya nao kazi kwa muda mrefu, yaani kampuni ya Steps Entertainment. 
 
Najua maswali yamekuwa mengi kwa kuwa kuna watayarishaji wengi wa filamu nchini wanaohangaika usiku na mchana ili kupata mkataba wa kufanya kazi chini ya kampuni hiyo kwa kuwa Steps Entertainment ndiyo kampuni ya usambazaji inayolipa vizuri zaidi kuliko makampuni mengine yote kwa sasa. 
 
Leo nimeamua kuongea walau kidogo …….
 
“Kwanza nikiri kuwa maneno ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, mhesimiwa Dr. Jakaya Kikwete aliyotamka siku aliyoiita Ikulu kamati ya mazishi ya marehemu Steven Kanumba ndiyo yamekuwa yakinisukuma sana hadi kufikia uamuzi huu mzito.
 
Kati ya waliounda kamati hiyo iliyoitwa Ikulu, mimi nilikuwa katibu, Mwenyekiti alikuwa Gabriel Mtitu au maarufu kama Mtitu Game, pia kulikuwa na wajumbe wengine kama Ruge Mutahaba, Asha Baraka, Jacob Steven ‘JB’ na Mzee Chilo. Baada ya kuongea mengi kuhusiana na msiba wa Kanumba na mazishi yake, mheshimiwa rais aliuliza ‘Hivi marehemu Kanumba kaacha filamu ngapi?”
 
Kwa aibu tulimjibu mheshimiwa rais kuwa marehemu Kanumba hajaacha hata filamu moja, zote ni za msambazaji wake na hata mbili ambazo zilikuwa hazijatoka yaani ‘Ndoa yangu’ na ‘Love & Power’ tayari zilikuwa ni za msambazaji kutokana na aina ya mkataba tunayoingia na msambazaji.
 
Mheshimiwa Rais alisikitika sana, akatuambia kuwa yeye hawezi kutumia nguvu kutukataza kuuza mali zetu lakini angependa kuona kuwa tunamiliki wenyewe filamu zetu na tutakapoona tumekwama tumwambie. Aliongeza kuwa kuuza haki zetu ni kama kuuza utu wetu. Maneno ya mheshimiwa Rais yalinichoma sana.
 
Mimi ni msanii wa kwanza kufanya kazi na kampuni hiyo kama mtayarishaji wa filamu na filamu yao ya kwanza kuisambaza ilikuwa ni ‘Jeraha la Ndoa’ ambayo niliitengeneza mimi. Na kwa kuthibitisha hilo, mwaka huu kampuni hiyo ya Steps ilitoa tuzo ya heshima kwa kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd kwa ajili hiyo.
 
Nasikitika kukiri kuwa filamu zote ambazo nilizitengeneza kisha zikasambazwa na kampuni ya Steps, siyo zangu tena. Kampuni hiyo imekuwa ikinunua haki zote za filamu wanazopelekewa kwa ajili ya kuzisambaza kwa hiyo baada tu ya kusaini mkataba wao unakuwa huwezi kufaidika tena na chochote kutokana na mauzo au faida nyingine zinazotokana na filamu yako. 
 
Kwa aina ya mikataba ambayo wasanii na watayarishaji tunaingia na kampuni ya Steps Entertainment, sisi tumekuwa ni wasimamizi tu wafilamu za zao, yaani ni kama manyapara kwenye mashamba ya mkonge wakati kwa ukoloni. Ni waajiriwa tusio na mafao ya uzeeni.
 
Kwa taarifa tu ni kwamba filamu zote mnazoziona mitaani zikisambazwa na kampuni siyo za hayo makampuni yanayotajwa kutengeneza filamu hizo bali ni filamu za Steps Entertainment. Ndiyo maana hata ukienda kwenye Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) utakuta wasanii wakubwa hawamiliki kabisa filamu lakini kampuni ya Steps inamiliki filamu zaidi ya 400.
 
Kifupi ni kuwa hadithi ni zetu, sehemu za kuigizia ni zetu, tunaigiza sisi, tunarekodi na kuhariri sisi lakini filamu ni za Steps Entertainment na ndiyo maana hata kampuni ya marehemu Steven Kanumba ‘Kanumba the Great’ imesambaratika baada ya kifo chake na mama yake akikabiliana na ugumu wa maisha lakini filamu za Kanumba bado zinatesa kwenye soko la filamu ndani na nje ya nchi.
 
Nawashangaa watu wanaomshutumu mama mzazi wa Kanumba kuwa amemaliza mali za mwanae na sasa anaishi kwa kufadhiliwa na Lulu, wangejua kilicho nyuma ya pazia wangemuonea huruma badala ya kumshutumu. Wakati Steps wanakiri kuwa filamu iliyowahi kuuza sana katika historia ya kampuni yao ni ‘Ndoa yangu’ ya Kanumba, hawasemi kuwa familia yake imenufaika vipi zaidi ya kupewa tuzo.
 
Pamoja na kununua haki zote za filamu, kampuni ya Steps hawatoi malipo ya filamu wanazozinunua kwa muda muafaka hivyo kutufanya tuendelee kuwa mafukara siku hadi siku. Hii ni sababu ya pili ya mimi kujitoa Steps, sitaki familia yangu ije kudhalilika baada ya kifo changu. 

Fikiria unapeleka filamu yako Steps, mnaingia mkataba wa kuuziana, lakini hawakulipi mpaka wakati watakapoamua kuiingiza sokoni hivyo hata wakikaa mwaka bila kuiingiza utakaa mwaka mzima unasuburi pesa. Hivi kweli mwaka huo utakuwa unakula nini kama umeamua kuifanya sanaa kuwa kazi yako?
 
Cha kuchekesha hata wanapoamua kuiingiza sokoni hawakulipi mpaka baada ya wiki mbili au tatu baada ya filamu yako kuwa imeingia sokoni, utasema hapo wamekulipa au umejilipa mwenyewe baada ya kuwa imenunuliwa? 

Mfano mwingine hai ni wa marehemu Said Juma Kilowoko (Sajuki) ambaye ni miongoni mwa wasanii maarufu na watayarishaji wa filamu. Marehemu Sajuki alilazimika kuzunguka na wasanii wenziye mikoani akiwa anamuwa taabani ili tu aweze kupata fedha za matibabu jambo ambalo naamini lilimzidishia matatizo ya kiafya.
 
Na kutokana na kuuza haki zetu zote ilibidi mkewe Sajuki, Wastara atengeneze ‘Mr & Mrs Sajuki’ ili aweze kupata fedha za kujikimu na kurekebisha mambo mbalimbali yaliyovurugika wakati akimuuguza mumewe. Kama tungekuwa hatulazimiki kuuza haki zetu zote, familia hiyo ingeweza japo kupeleka filamu zake kwenye vituo vya runinga barani Afrika ambako ni chanzo kingine cha mapato kwa msanii.
 
Baada ya kutafakari kwa kina niliamua kulipia leseni ya usambazaji wa filamu kupitia kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd ili niwe nasambaza filamu zangu nikitegemewa kupata sapoti kubwa kutoka kwa wasanii wenzangu hasa mastaa wakubwa lakini imekuwa kinyume chake. Kwa sasa naonekana adui mbele ya wenzangu.
 
Kupitia kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd, niliingiza sokoni filamu ya ‘Omega the Confusion’, na ndani ya masaa matano ya kwanza nilifanikiwa kurudisha gharama zangu zote na kupata faida kidogo. Toka hapo hadi sasa inaendelea kukimbia sokoni hivyo natengeneza faida tu na bado filamu ni yangu, naweza kuifanyia chochote kama kuipeleka kwenye runinga za kimataifa n.k
 
Nimalizie kwa kuweka wazi kuwa sina ugomvi wowote na kampuni ya Steps, mmiliki wake wala mtumishi yeyote wa kampuni hiyo. Pia sina chuki na yeyote kati ya wanaoendelea kufanya kazi chini ya kampuni hiyo. Kikubwa ni kuwa haya ni maisha na kila mmoja ana mtazamo wake katika kuyakabili na kujiletea mafanikio”.
 
“WOGA WAKO NDIO UMASKINI WAKO”

‘TEAM NYATI’

CHANZO UKURASA WAKE WA FACEBOOK

No comments:

Post a Comment