SIMBA
imetangaza kiama kwa timu za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, baada ya kikosi
chake kufanya mazoezi kwa pamoja na wachezaji walioongezwa kikosini.
Wekundu hao
wa Msimbazi, wikiendi iliyopita walianza ligi vibaya kwa kulazimishwa sare ya
bao 1-1 na Rhino ya Tabora, huku wapinzani wao, Yanga wakichekelea ushindi wa
mabao yao 5-1 dhidi ya Ashanti United, lakini Jumatano iliyopita hali ikawa ni
tofauti kwa Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro na Yanga kulazimishwa
sare ya bao 1-1 na Ashanti United.
Sasa timu
hizo mbili zinalingana kwa pointi, lakini kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni
amesema wataanza ligi katika mechi ijayo.
Katika mechi
zijazo ambazo ni za mzunguko wa tatu zitakazopigwa kwenye viwanja tofauti,
Simba SC watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
Coastal Union wataikaribisha Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Ruvu Shootings
watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT Uwanja wa Mabatini, Pwani, JKT Oljoro
wataikaribisha Rhino Rangers Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Mbeya City
wataikaribisha Yanga SC Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Kagera Sugar watakuwa
wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Kaitaba, Kagera, wakati Ashanti United watamenyana
na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kibadeni
aliliambia DIMBA kwamba kilichowafanya waanze ligi kwa kusuasua ni kuvurugwa
kwa mipango yake, ambapo walijikuta wakipewa taarifa za kushtukiza kwamba
hawatakiwi kuwatumia wachezaji wa kigeni, Hamis Tambwe na Kaze Gilbert, ambao
walikuwa kwenye mipango yake.
"Kusema
kweli taarifa ile ilitushtua, tulitegemea kuwatumia lakini hatukuweza kutokana
na kushtukizwa, hivyo mimi kama kocha, nililazimika kupanga kikosi ambacho
sikukitarajia," alisema Kibadeni.
Alisema hata
katika mchezo dhidi ya JKT Oljoro walipotoka sare ya bao 1-0, aliwapanga kina
Kaze lakini kutokana na ugeni wao kwenye kikosi, ndio maana waliibuka na
ushindi mwembamba.
Hata hivyo
alisema kwa hivi sasa wamerudi kwenye mstari, huku kikosi cha timu hiyo
kikiongezwa nguvu na ujio wa kiungo wa zamani Henry Joseph, ambaye jana
alikuwepo kwenye mazoezi kwenye uwanja wa Kinesi, hivyo kumpa matumaini kocha
huyo ya kufanya vizuri kwenye ligi.
Kwa sasa
ligi hiyo inakwenda mapumziko kwa wiki mbili, baada ya raundi mbili za awali,
kupisha maandalizi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ya mchezo
wa mwisho wa kufuzu Kombe la Dunia mwakani Brazil, dhidi ya Gambia, Septemba 7,
mwaka huu.
Baada ya
kila timu kucheza mechi mbili, JKT Ruvu ipo kileleni kwa pointi zake sita na
mabao matano kufuatia kushinda mechi mbili ugenini na nyumbani, wakati
inaziacha timu za nyuma yake kwa pointi mbili.
Yanga SC,
iliyoanza kwa kishindo ikishinda 5-1 dhidi ya Ashanti United, ililazimishwa
sare ya 1-1 na Coastal Union, wakati Simba iliyoanza kwa sare ya 2-2 na Rhino
mjini Tabora ikizinduka na kushinda 1-0 Arusha.
Azam nayo
iliyoanza kwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Morogoro, ilizinduka na kuifunga 2-0
Rhino Rangers mjini Tabora.
Kwa upande
wa mabao, mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu zinaanzishwa na
wachezaji watatu, Jerry Tegete wa Yanga, Bakari Kondo wa JKT Ruvu na Jonas
Mkude wa Simba SC, ambao wote kila mmoja ana mabao mawili.
Baada ya
mechi mbili za awali, timu zinakwenda kujipanga kabla ya kuendelea na ligi
hiyo, Septemba 14, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment