MTAANI wanaitwa ‘big’, kwenye soka tunawaita
‘vibonge’, hapa tunawazungumzia watu wanene, ambao kila kona wana majina ya
utani ambayo wanatungiwa kutokana na miili yao. Mchezaji wa soka anatakiwa kuwa
fiti, mkakamavu na mwepesi ilikuweza kukimbizana na kupambana muda wote
uwanjani.
Lakini kuna baadhi ya wachezaji kutokana na vipato
vikubwa wanavyovipata, kuendekeza starehe na kusahau mazoezi, wamejikuta
wakiumuka na kuongezeka uzito, jambo ambalo limesababisha mashabiki wa soka
kuwatungia jina la ‘vibonge’, kama angekuwa siyo mcheza soka tungesema ‘big’.
Kuna wachezaji wamelazimika kuachana na soka mapema
kwa sababu ya ubonge, hivyo kujikuta wakishindwa kuendana na kasi ya soka kwa
dakika 90 uwanjani. Makala haya yanakuletea wachezaji watano vibonge kutokea
kwenye soka, kuna wengine wamestaafu na kuna wale waliokomaa na mpaka sasa bado
wanacheza.
Ronaldo
de Lima
Mbrazil huyo ambaye mashabiki walimpa jina la utani
la ‘o fenomeno’, kutokana na kasi yake na uwezo wa kufunga aliokuwa nao wakati
akicheza, ni mfano mzuri wa wachezaji ambao walishindwa kujitunza na kujikuta
akiwa kibonge. Soka lake lilianza kuporomoka baada ya kuanza kuandamwa na
tatizo la kuongezeka uzito, ambapo watu wakaacha kuangalia mabao yake uwanjani
na kujadili ukibonge wake.
Japokuwa aliendelea kufunga uwanjani na kuonyesha
vile vitu ambavyo amekuwa navyo tangu alipokuwa kinda, lakini ubonge ulionekana
kumuathiri na kuamua kuachana na soka kutokana na tatizo hilo, siku za karibuni
amekuwa akishiriki kwenye kipindi cha televisheni cha nchini kwao Brazil cha
kupunguza uzito, na kidogo anaonekana kupungua.
Adriano
Ilikuwa ngumu sana kuchukua mpira kutoka kwenye guu
lake la kushoto kipindi alipokuwa kwenye kilele cha kiwango chake, kuna wakati
picha yake ilitumika kutangaza magame ya video, lakini leo hii ukibonge
umemfanya kuachana na soka akiwa na umri mdogo tu wa miaka 30 mwaka 2012.
Matatizo ya ukibonge yalimuanza pale alipogoma
kuachana na maisha ya kujirusha, kuendekeza mademu na pombe. Ubonge wake,
kupenda starehe, mademu na mtungi, kuliwahi kuilazimisha klabu yake aliyokuwa
akichezea ya Corinthians kumzuia kutoka nje ya nyumba yake ili apunguze uzito,
lakini hilo halikufanikiwa, akaishia kustaafu soka akiwa na miaka 30 tu.
Thomas
Brolin
Msweden huyu ambaye alikuwa na sura ya kitoto,
anakumbukwa kwenye ulimwengu wa soka kwa mambo matatu makubwa – kuiua England
wakati wa michuano ya Euro mwaka 1992, kuchemka wakati akicheza Leeds United na
ubonge wake uliopitiliza.
Tatizo lake la ubonge lilianza kuonekana kwenye
mechi dhidi ya Liverpool mwaka 1995, kwa sababu tu hakuwa akipenda kukimbia
kimbia uwanjani, kupanda na kushuka kutokana na kupangwa kwenye winga ya kulia,
aliamua kucheza vibaya kwa makusudi ili timu yake ifungwe na kocha wake
asimpange tena kama winga wa kulia. Na kweli siku hiyo Leeds ilichapwa mabao
5-0 na mwenyewe alikiri kucheza vibaya kwa makusudi.
Frank
Lampard
Alipokuwa kijana mdogo, mashabiki wa timu pinzani
waliwahi kumtungia jina la ‘Fat Frank’, wakimaanisha Frank Bonge, wengi wangeweza
kuona kwamba Lampard hastahili kuwa kwenye listi hii, kutokana na umbo lake la
sasa, lakini kwa wale waliomuona alipokuwa kinda wanajua jinsi gani tatizo la
ubonge lilivyotaka kukatisha soka lake.
Mafanikio aliyokuja kuyapata ukubwani ni mfano wa
kuigwa kwa vijana wadogo ambao wanataka kucheza soka, lakini ubonge kwao ndiyo
tatizo, inaonyesha chochote mtu atakachoamua kufanya anaweza, cha msingi ni
kuwa na nia ya dhati tu.
Ronaldinho
Gaucho
Moja ya vitu vilivyoporomosha kiwango cha
Ronaldinho, kutoka alipokuwa Barcelona na AC Milan na kumfanya kuamua kurudi
kwao Brazil ni ubonge, Dinho alikuwa na tatizo la kuongezeka uzito na kupungua,
jambo ambalo liliwafanya hata mashabiki wa AC Milan kumchoka.
Kwenye soka ubonge siyo kitu kizuri. Unamfanya mchezaji
kukosa kasi na jambo hilo lilisababisha watu kumkosa Gaucho waliyekuwa
wakimfahamu wa Barca, ambaye alikuwa na uwezo wa kuwapita mabeki kadri atakavyo
kwa kasi na matendo ya ajabu, lakini uzito ulimfanya kukosa ile kasi ya
kukimbizana na mabeki na alipopoteza mpira akawa mvivu kukaba.
Gaucho alijikuta akipoteza kujiamini, na kulazimika
kurudi kwao Brazil, sasa hivi anaonekana kupungua uzito, lakini kiukweli ubonge
ndio uliomng’oa Ulaya.
No comments:
Post a Comment