USHINDI wa Rhino Rangers ya Tabora wa mabao 4-1 dhidi ya
Sports Club Villa ya Uganda umempa jeuri kocha wao Sebastian Nkoma na kujigamba
kuwa hakuna timu itakayomsumbua kwenye ligi kuu msimu huu.
Akizungumza na LENZI YA MICHEZO kwa njia ya simu toka Tabora, Seba alisema kuwa kila timu itakayokutana na
Rhino Rangers ijiandae kupata kipigo kwani mchezo wao hautofautiani.
“Timu yangu imeifunga SC Villa mabao 4-1 kama hizo timu
zinazojiita vigogo wa soka nchini, hivyo timu yangu ni bora wajiandae na vichapo
tu”, alijigamba Seba.
Rhino Rangers inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania,
Kanda ya Magharibi, iliweka kambi katika
mikoa ya Shinyanga na Mara na kucheza michezo minne huko na kushinda miwili,
sare mmoja na kufungwa mmoja imerudi Tabora ambapo ndio nyumbani.
Kwenye mchezo wao na SC Villa mabao ya Rhino yalifungwa na
na Julias Masunga dakika ya 23 na Saad Kipanga aliyefunga dakika ya 41, Ally
Ahmed dakika ya 73 na Victor Hagai aliyehitimisha karamu ya mabao dakika ya 85.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora (TAREFA), Yusuph
Kitumbo alisema timu ya Rhino imecheza mchezo mzuri na nidhamu imeimarika kwani
hata mashabiki wameridhishwa na kiwango cha wachezaji.
Rhino Rangers itafungua dimba na Simba Agosti 24, mwaka huu
kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi , Tabora wakati Yanga watakuwa Taifa
wakicheza na Ashanti United.
No comments:
Post a Comment