MCHEZO
wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam FC iliyochezwa wikendi iliyopita Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kupata ushindi wa bao
1-0, ilikuwa ishara ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kuanza. DIMBA linatathmini
timu zote 14 shiriki na nini kinachoweza kutokea mwishoni mwa msimu.
*
Ashanti United
Msimu
uliopita: Vinara Kundi B
Kocha:
Mbaraka Mbaruka
Si
wageni kwenye ligi ila wamerudi tena ambapo mara ya mwisho kushiriki Ligi Kuu
Bara ilikuwa msimu 2007/08. Ashanti United inaongeza idadi ya timu za Dar es
Salaam na ni mojawapo ya timu yenye mashabiki wengi. Uongozi wa Ashanti United
umejitahidi kuwa makini kwenye usajili lakini kinachosubiriwa ni namna gani
watakavyokabiliana na wapinzani wao.
MATARAJIO:
Hawatataka kurudia makosa yaliyosababisha kushushwa daraja na dalili
zinaonyesha watamaliza kwenye nafasi 10 za juu.
*
Azam FC
Msimu
uliopita: Nafasi ya pili
Kocha:
Stewart Hall
Kinywani
mwa wadau wa soka, Azam FC ni mfano mzuri wa namna gani klabu za soka zinapaswa
kuendeshwa. Azam FC waliweka kambi nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya
ambapo walicheza na klabu kubwa huko wakishinda moja na kufungwa tatu. Kupoteza
mchezo wa Ngao ya Jamii si kupoteza imani kwa timu hii kuelekea msimu mpya.
Kocha Hall hajafanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza na amepandisha
baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha vijana. Labda huu unaweza ukawa
msimu wa mshambuliaji Gaudence Mwaikimba kurudisha makali yake. Hata hivyo,
safu ya ushambuliaji inahitajika kuwa makini huku viungo wakicheza mpira wa
kasi badala ya kuremba.
MATARAJIO:
Kuna kila dalili huu unaweza ukawa msimu wa Azam FC kutwaa ubingwa baada ya
misimu miwili mfululizo kumaliza nafasi ya pili.
*
Coastal Union
Msimu
uliopita: Nafasi ya sita
Kocha:
Hemedi Moroko
Miongoni
mwa timu ambazo zimetumia fedha nyingi kufanya usajili ni Coastal Union ambayo
imejichimbia Tanga. Imewaongeza kundini kiungo Haruna Moshi ‘Boban’, beki Juma
Nyosso, winga Uhuru Selemani, washambuliaji Mkenya Crispini Odula na Mganda
Yayo Lutimba. Coastal Union imekuwa ikipata sapoti kubwa kutoka kwa wenyeji wa
mkoa wa Tanga ambao hujitokeza kwa wingi kujaza Uwanja wa Mkwakani hivyo basi
Moroko hatataka kuwaangusha kwa kuhakikisha ‘hatoki mtu’ Tanga.
MATARAJIO:
Kama usajili ni kigezo cha timu kufanya vizuri, hamna shaka Coastal Union
itamaliza kwenye nafasi nne za juu.
*
JKT Oljoro
Msimu
uliopita: Nafasi ya nane
Kocha:
Alex Mwangeja
Huu
utakuwa ni msimu wa tatu tangu JKT Oljoro ipande daraja ambapo imekuwa
ikiwakilisha vyema mkoa wa Arusha baada ya kushuka kwa timu ya AFC. Hata hivyo,
msimu uliopita haukuwa mzuri kwa timu hii ya jeshi ukilinganisha na msimu wao
wa kwanza. JKT Oljoro haina wachezaji wengi wenye majina makubwa lakini lengo
lao limekuwa ni kuhakikisha hawashuki daraja huku wakiamini uzoefu wanaoupata
utawasaidia kuwa miongoni mwa timu tishio.
MATARAJIO:
Watakuwa na wakati mgumu kupigana kuepuka kushuka daraja.
*
JKT Ruvu
Msimu
uliopita: Nafasi ya 10
Kocha:
Mbwana Makata
Waliponea
kwenye tundu la sindano kushuka daraja msimu uliopita na safari hii, JKT Ruvu
haitataka kurudia makosa hayo. Moja ya sifa kubwa ya JKT Ruvu ni kuzalisha
wachezaji wenye vipaja ambao baadaye huvua magwanda na kujiunga na timu za
uraiani. Kuondoka kwa kocha Charles Kilinda ambaye inasadikiwa ndiye kocha
aliyedumu na timu moja kwa muda mrefu ni pigo kwa JKT Ruvu na sasa wanaanza
maisha mapya wakijua fika safari itakuwa ngumu.
MATARAJIO:
Kama ilivyokuwa msimu uliopita, kuna kila dalili JKT Ruvu wakawa na wakati
mgumu kujinusuru na balaa la kushuka daraja.
*
Kagera Sugar
Msimu
uliopita: Nafasi ya nne
Kocha:
Jackson Mayanja
Kitendo
cha kumbakisha mshambuliaji Felix Themi kwa kumuongezea mkataba ni sawa na
usajili mpya kwa timu hiyo kwani Themi amekuwa mchezaji muhimu wa Kagera Sugar
na ni sawa na nembo ya timu hiyo. Timu hii yenye maskani yake Bukoba imekuwa
ikitumia vyema uwanja wake wa Kaitaba. Kocha Mayanja ana jukumu kubwa
kuhakikisha moto aliyouwasha Abdallah ‘King’ Kibadeni unaendelea kuwaka.
MATARAJIO:
Bado ina safari ndefu ya kuchukua ubingwa ijapokuwa huu ni msimu mwingine tena
wa Kagera Sugar kunyanyasa vigogo wa soka nchini
*
Mbeya City
Msimu
uliopita: Vinara Kundi A
Kocha:
Juma Mwambusi
Mara
ya mwisho kusikia jina la Juma Mwambusi ni wakati akiwa kocha wa Prisons, ila
safari hii anarudi akiwa anaifundisha timu ya Mbeya City aliyoiwezesha kupanda
daraja. Mbeya City inaungana na Prisons kuiwakilisha mkoa wa Mbeya. Hii ni moja
ya timu ambayo imetabiriwa kuwa na msimu mzuri katika msimu wake wa kwanza.
MATARAJIO:
Mbeya City ni miongoni mwa timu ambazo zitamaliza katikati ya ligi.
*
Mgambo JKT
Msimu
uliopita: Nafasi ya 11
Kocha:
Mohammed Kampira
Handeni
ni kwao na Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga ni uwanja wao wa nyumbani. Huu ni
msimu wao wa tatu mfululizo Ligi Kuu Bara. Hesabu ndizo zilizowaokoa kuepuka
kushuka daraja. Kosa ambalo Mgambo JKT walilofanya msimu uliopita ni kurusu
kupoteza idadi kubwa ya michezo yake. Ni dhahiri kocha Kampira atataka safu
yake ya ulinzi kuwa makini na washambuliaji kutumia vyema nafasi
zitakazotengenezwa.
MATARAJIO:
Huu ni mtihani mwingine kwa Mgambo JKT na kuna uwezekano ‘watakuwa wanapumulia
mashine’ msimu huu.
*
Mtibwa Sugar
Msimu
uliopita: Nafasi ya tano
Kocha:
Mecky Mexime
Huu
ni mwaka wa 13 tangu Mtibwa Sugar kutwaa ubingwa mara ya mwisho na ijapokuwa
wamekuwa wakimaliza miongoni mwa nafasi za juu, kiu ya mashabiki ni kuona taji
linaenda Turiani mkoani Morogoro. Hazina kubwa ya Mtibwa Sugar ni kutengeneza
vipaji ambavyo vimekuwa vikiwatoa udenda timu kubwa. Mshambuliaji wao tegemeo,
Hussein Javu, amejiunga na Yanga kumfuata Said Bahanuzi ambaye nyota yake
iling’ara akiwa Mtibwa Sugar. Kocha Mexime alivuna pointi sita kutoka kwa Simba
na nne kutoka kwa kwa Yanga msimu uliopita na ijapokuwa atataka kurudia
mafanikio hayo, mtihani mkubwa ni kuhakikisha asipoteze mechi zingine.
MATARAJIO:
Mtibwa Sugar itamaliza kwenye nafasi nne za juu.
*
Prisons
Msimu
uliopita: Nafasi ya tisa
Kocha:
Jumanne Chale
Mechi
nyingi walizotoa sare ulichangia kwa kiasi kikubwa Prisons kufanya vibaya msimu
uliopita. Timu hii inayomikiliwa na Jeshi la Magereza imekuwa ikijaribu kurudia
mafanikio ya 1999 ambapo walifanikiwa kutwaa ubingwa. Namna ambavyo
watakavyoanza ligi utakua chachu kwa timu hii kutoka Mbeya kufanya vizuri msimu
huu.
MATARAJIO:
Bado utakuwa msimu mwingine mgumu kwa Prisons na watahitaji kupambana kuepuka
kushuka daraja.
*
Rhino Rangers
Msimu
uliopita: Vinara Kundi C
Kocha:
Sebastian Nkoma
Mkoa
wa Tabora umepata mwakilishi kwenye Ligi Kuu Bara na swali kubwa ni je,
watakuwa wamekuja kupapasa na kuondoka? Katika kuonyesha dhamira yao ya kubaki
kwenye ligi, Rhino Rangers imemsajili kiungo wa zamani wa Yanga na Simba,
Nurdin Bakari. Hii ni fursa nyingine kwa wenyeji wa Tabora kuipa sapoti timu
hii yao inayomilikiwa na jeshi.
MATARAJIO:
Walikuwa na wakati mzuri Ligi Daraja la Kwanza lakini shughuli ni tofauti Ligi
Kuu Bara na vita vyao vitakuwa vya kuepuka kushuka daraja.
*
Ruvu Shooting
Msimu
uliopita: Nafasi ya saba
Kocha:
Charles Boniface Mkwassa
Hii
ni timu ya majeshi ambayo msimu uliopita ndiyo iliyofanya vizuri na sifa lazima
zimuende kocha Mkwassa kwani ni mtu anayeweza kuusoma mchezo na kubadilisha
timu. Ruvu Shooting imekuwa ikicheza kitimu zaidi na wakati mwingine soka la
burudani hususan inapopambana na timu kongwe. Kufanikiwa zaidi kwa Ruvu
Shooting kutahitaji kutopoteza katika michezo wanaocheza vizuri.
MATARAJIO:
Ni timu ambayo itamaliza kwenye nafasi za katikati.
*
Simba
Msimu
uliopita: Nafasi ya tatu
Kocha:
Abdalla ‘King’ Kibadeni
Unapotaja
Simba kwa miaka ya hivi karibuni, huwezi kuitenganisha na majina kama Juma
Kaseja na Haruna Moshi ‘Boban’. Lakini hii Simba ya sasa chini ya kocha
Kibadeni ina sura mpya huku vijana kama kina Jonas Mkude, Ramadhani Singano na
Haruna Chanongo wakipewa nafasi kuonyesha uwezo wao. Maandalizi ya msimu mpya
hayakuwa mazuri kwa Simba ila benchi la ufundi lenye watu wazoefu wameshatambua
makosa ndani ya timu na kuyafanyia kazi. Simba haitataka kurudia makosa ya
msimu uliopita ambapo walianza vizuri lakini wakapoteza mwelekeo na kujikuta
katika wakati mgumu kutetea ubingwa wao.
MATARAJIO:
Itamaliza katika nafasi tatu za juu na kwasababu haishiriki michuano yoyote ya
kimataifa ngazi ya klabu, nguvu zao zote watazielekeza kwenye Ligi Kuu
Bara.
*
Yanga
Msimu
uliopita: Bingwa
Kocha:
Ernie Brandts
Licha
ya kumrudisha kundini winga mshambuliaji Mrisho Ngassa, Yanga imehakiksha
inabakisha wachezaji wake wa kigeni hususan kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima
ambaye alikuwa chachu ya Wanajangwani kutwaa ubingwa. Yanga imekuwa na
maandalizi mazuri ya msimu mpya na hilo wamelidhihirisha kwenye mchezo wa Ngao
ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC. Ni dhahiri
kuwa hawatataka kuanza vibaya kama walivyofanya msimu uliopita na kazi kubwa
aliyonayo kocha Brandts ni kuhakikisha safu yake ya ushambuliaji inayotabiriwa
kuwa tishio msimu huu, haipotezi nafasi zitakazo tengenezwa.
MATARAJIO:
Kuna uwezekano mkubwa Yanga ikatetea ubingwa wake ila ni Ligi ya Mabingwa
Afrika ambayo Yanga safari hii inahitajika kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment