TIMU za Chelsea, Arsenal na Real Madrid, zimeripotiwa kufuatilia kwa
karibu hatima ya mazungumzo kati ya Kocha wa Manchester United, David Moyes na nyota
wake,Wayne Rooney, kama yakikwama zianze kupigana vikumbo kumwania nyota huyo.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya
habari nchini England, Moyes na Rooney pamoja na wakala wa mchezaji huyo
watakaa meza moja leo, kikiwa ni kibarua chake cha kwanza kikubwa kwa kocha
huyo tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Mkataba wa miaka sita wa Mscotland
huyo ulianza rasmi jana na kwa mujibu wa vyanzo vya habari, jana hiyo
alitarajia kuwasili Makao Makuu ya klabu yaliyopo katika viunga vya kitongoji
cha Carrington, akiwa na dhamira ya
kuhakikisha anamaliza sakata hilo la muda mrefu kuhusu Rooney.
Vyanzo hivyo vinaeleza kuwa,
Moyes anataka Rooney abaki, ingawa anafahamu fika nyota
huyo mwenye umri wa miaka 27 anatafakari
kuitema klabu hiyo ambayo alijiunga nayo mwaka 2004 kwa kitita cha pauni
milioni 25.6.
Inaelezwa kwamba nyota huyo wa timu
ya Taifa ya England anameshakuwa na mawazo ya kwamba kubadili klabu ndiyo njia mbadala ya
kunusuru kibarua chake katika timu ya taifa ili aweze kukipiga kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika
mwakani nchini Brazil.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kubaki kwa Rooney
kutategemea na jinsi mazungumzo
yatakavyokwenda, lakini ukweli ni kwamba Moyes ana dhamira ya kuhakikisha
anamshawishi ili abaki.
Timu za Arsenal na Chelsea zote kwa
pamoja zimeshaonesha dhamira ya kutaka kumnasa Rooney wakati wa usajili wa
majira haya ya joto na endapo Manchester United itakubali kumuuza, basi huenda
akatua ndani ya klabu mojawapo.
Katika hatua nyingine, nahodha wa zamani wa timu hiyo,
Gary Neville, amemshauri Rooney aendelee kuitumikia klabu hiyo.
Nahodha huyo na kocha wa England
alisema jana kuwa anaamini mambo
yatamuendea vizuri mchezaji mwenzake huyo wa zamani endapo atabaki kwenye klabu
hiyo ya Old Trafford.
No comments:
Post a Comment