“Nimelifikiria hili kwa muda mrefu na imekuwa jambo gumu kwangu, lakini nilichoamua ni kwamba siongezi tena mkataba wangu. Ndugu zangu, mashabiki, ni wazi kabisa hamtakubaliana na maamuzi yangu na siku zote nitaheshimu mawazo yenu.” – ilisomeka taarifa ya Robin van Persie kwenye gazeti la The Telegraph, iliyochapishwa wakati anaomba kuondoka mwaka jana.
Ulimwengu wa Arsenal uliingia kwenye misukosuko mingi baada ya nahodha wao huyo kuamua kutoongeza mkataba katika klabu hiyo, hasa baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa kabisa kwa msimu huo akifanikiwa kufunga mabao 37 katika michuano yote aliyoshiriki.
Arsenal ilitaka kuweka ngumu, ikakataa ofa kutoka Juventus, Manchester United na Manchester City, lakini United iliporudi tena na ofa yao nzuri, mabosi wa Washika Bunduki hao hawakuwa na namna nyingine, waliamua kumpiga bei staa wao huyo.
Jambo hilo liliibua mgongano wa mawazo kutoka kwa mashabiki wa Arsenal, baadhi yao walionekana kuumizwa na taarifa hiyo ya Van Persie, wakati wengine hawakujali kitu, walimpa baraka nahodha wao huyo kuondoka na kufunga milango kuendelea kuisapoti timu yao.
Baadhi ya mashabiki walidhani kwamba RVP alikuwa na haki zote za kufanya kile alichokitaka kwa manufaa yake. Amekuwa kwenye klabu hiyo kwa muda mrefu na kwamba hakutwaa taji lolote.
Ni lazima aliwatazama wachezaji wengine waliohama timu hiyo misimu ya hivi karibuni (Thierry Henry, Cesc Fabregas, Gael Clichy, Samir Nasri, Mathieu Flamini na wengineo), wote hao wametwaa mataji katika klabu zao walizohamia na ni wazi kabisa na yeye alihitaji kitu kama hicho.
Kipindi cha maisha ya mchezaji kiuchezaji ni kifupi sana, hivyo ni wazi alihitaji kutwaa medali na mataji ili awe na kitu cha kusimulia. Si kumbukumbu za kufunga mabao mazuri kwa timu pinzani huku timu yako ikiruhusu kufungwa mabao mengi zaidi.
Alifunga bao katika mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi mwaka 2011 kabla ya kuumia, lakini timu yake ilishindwa kunyakua ubingwa baada ya blanda ya beki Laurent Koscielny na Wojciech Szczesny katika dakika za mwisho zilizowasababisha kupoteza mchezo huo.
Kuna baadhi ya mashabiki wamekuwa wakizungumzia suala la heshima kwa Arsene Wenger akiwa kama kocha ambaye mara nyingi amekuwa akiwaamini wachezaji wake bila ya kujali amefanya hivyo mara ngapi. Wenger aliweza kumbadili Emmanuel Adebayor, Fabregas, Clichy, Nasri na RVP kuwa wachezaji bora kabisa duniani, lakini baadaye walimgeuka na kisha ni kama wanamtupia mayai usoni.
Na kwenye suala la RVP lilionyesha wazi kwamba heshima kwa Wenger ilishuka. Lakini, hilo lilitokana na Wenger mwenyewe kushindwa kunyakua chochote kwa misimu nane.
Kama Arsenal ingekuwa imetwaa mataji kwa miaka ya hivi karibuni, nyota wote hao walioondoka, wangeendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Miezi 12 imepita, wakati mashabiki wa klabu hiyo wakijaribu kusahau kilichopita, Laurent Koscielny, ndiyo, Laurent Koscielny amelipua bomu kama la RVP-wakati alipodai kwamba ataihama timu hiyo kama ukame wa mataji utaendelea.
Katika mahojiano yake na EuroSport, alisema: "Najisikia furaha kuwa Arsenal, kama dhamira yetu ni kushindana na timu nyingine ni wazi nitahitaji kubaki. Ni ngumu sana kisaikolojia.
"Tulikuwa kwenye presha muda wote kwamba kama Arsenal isingekuwamo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ingekuwa pigo kubwa.
"Nasubiri kuona kama kuna klabu zitavutiwa nami. Nahitaji pengine kuwapo kwenye ligi nyingine. Paris Saint-Germain? Bado hakuna mawasiliano.
"Ni ngumu kuona hamtwai mataji mwaka hadi mwaka. Sisi ni washindani na profesheno, tunahitaji ushindi. Nataka kitu cha kuongeza kwenye mafanikio yangu. Kama Arsenal itashindwa kunisaidia kulifanikisha hilo, nitahamia kwingine."
Kwa namna ambavyo soka la Koscielny lilivyogeuka na kuwa bora kabisa ni jambo la aina yake. Miaka mitano iliyopita, alianza kuchezea Tours FC, timu ya daraja la pili (Ligue 2) nchini Ufaransa.
Katika msimu wake wa pili Tours FC, ulikuwa wa aina yake, alikosa mechi nne tu za ligi, na aliweza kuwamo kwenye kikosi cha Ligue 2 mwishoni mwa msimu huo.
FC Lorient ilimnyakua kwa euro milioni 1.7, na hapo akaingia kwenye kikosi cha kwanza na kukisaidia kwa asilimia 100.
Kutokana na kuondoka kwa William Gallas, Philippe Senderos na Mikael Silvestre, Wenger aliamua kumchukua na kupata nafasi ya kuchezea klabu hiyo kubwa kabisa inayocheza ligi kubwa pia.
Ameweza kucheza mechi 86 katika misimu miwili aliyokuwa kwenye kikosi hicho na kufunga mabao sita. Msimu uliopita, Koscielny aliweza kuwa moyo wa beki ya Arsenal na hata kufikia kumfunika Thomas Vermaelen kwenye safu ya ulinzi.
Uwezo wa Koscielny kusoma mchezo na kuwahimili washambuliaji hilo ni jambo jingine muhimu linalompa alama kubwa mchezaji huyo.
Kasi yake ni nzuri na amekuwa akienda mbele na kurudi kutimiza wajibu wake wa kuzuia.
Amekuwa tishio kubwa kwenye mipira ya kona, ni fundi wa kufunga mabao ya vichwa na ya aina nyingine, kama lile alilofunga lililoipa Arsenal tiketi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Lakini, sasa maneno yake hayana tofauti na ya RVP aliyoyasema mwaka jana kwamba Arsenal inakosa dhamira ya dhati ya kuwania mataji na hilo ndiyo sababu kubwa inayowafanya kwenda kusaka malisho bora kwingine.
Koscielny alikuwa mtu muhimu kwenye kampeni ya Arsenal kuweza kushika nafasi ya nne kwenye ligi na tangu hapo amekuwa akizivutia timu nyingi, ikiwamo mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich.
Licha ya kwamba hivi karibuni alisaini mkataba mpya ambao utamfanya abaki kwenye klabu hiyo hadi 2017, ofa safi ikija kutoka kwa Wajerumani hao, Kos atadandia meli hiyo.
Koscielny anaweza kudharau dhamira ya Arsenal kupigania kufuzu michuano ya Ulaya, lakini kwa timu kama Bayern Munich, itakuwa tofauti sana, presha yao ni kutwaa mataji kutokana na presha ya wachezaji wao kile wanachotaka kukifanya kuliko Arsenal, ambao kwao mambo yanakuwa 'okay' kama tu wakifuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Inasikitisha.
Kwa kusema ukweli, maneno hayo ya Koscielny yatawafungua macho Arsene Wenger na mabosi wa Arsenal.
Ni vipi Arsenal itaweza kuwabakiza wachezaji wake kama itashindwa kuwapa sababu ya kufanya hivyo?
Msimu uliopita, Arsenal ilikuwa nyuma kwa pointi 16 dhidi ya mabingwa, Manchester United, na walitupwa nje ya makombe ya ndani na timu ndogo kabisa, Bradford na Blackburn.
Kwenye Ligi ya Mabingwa, kiwango kibovu kwenye mechi yao ya kwanza kiliwaponza, licha ya kushinda 2-0 dhidi ya Bayern katika mechi yao ya marudiano, hakikuweza kutosha kuwafanya watinge robo fainali ya michuano hiyo.
Kwa timu ambayo imetwaa mataji matatu ya Ligi Kuu na manne ya Kombe la FA chini ya Wenger, hiyo haitoshi.
Kwenye majira haya ya joto, mambo yanapaswa kuwa tofauti, la hakutakuwa na kisingizio tena.
Arsenal inapaswa kuwalinda wachezaji wake na kufanya usajili wenye viwango kwa nafasi tatu muhimu.
Wojciech Szczesny anahitaji upinzani. Uvumi kuhusu kipa wa Queen’s Park Ranger, Julio Cesar, itakuwa vizuri kama atatua mahali hapo.
Kutokana na Fabianski kutarajia kuondoka mahali hapo, Szczesny sasa atapata usingizi mnono usiku akitambua mpinzani wake atakuwa Vito Mannone.
Licha ya kwamba Mikel Arteta ameweza kuonyesha kiwango bora katika msimu wake wa kwanza akicheza kama kiungo mkabaji, Arsenal bado inahitaji kiungo mwingine mkabaji, ambaye ataweza kutawala uwanjani.
Kiungo wa Lyon, Maxime Gonalons, amekuwa akihusishwa na mpango wa kutua Arsenal na jambo hilo likitokea, kiungo ya timu hiyo itakuwa imeimarika zaidi.
Olivier Giroud inawezekana amefunga mabao 17 katika msimu wake wa kwanza, lakini Arsenal inahitaji mtaalamu (si Theo Walcott) atakayefunga mabao hata kama katika mazingira magumu. Mshambuliaji wa Fiorentina, Stevan Jovetic na wa Galatasaray, Burak Yilmaz, wataweza kulimaliza tatizo hilo.
Tofauti na ilivyokuwa kwa Van Persie, alionekana kama msaliti kutokana na kuihama timu hiyo akitokea kwenye kiwango bora kabisa, baadhi wanaweza kuona Koscielny kwamba nafasi yake si tishio sana kama ataondoka.
Lakini, ukweli ni kwamba huwezi kufahamu ni kitu gani kinaendelea kichwani mwa mchezaji profesheno.
Baadhi ya mashabiki watadiriki hata kumwonyesha vidole Koscielny, wakiamini kuwa Wenger amemfanya mchezaji huyo kuwa bora. Kweli.
Lakini, ni Wenger huyo huyo, aliyewatengeneza Adebayor, Fabregas, Clichy, Flamini na RVP na viwango vyao walivyonavyo kwa sasa, lakini hawakutaka kuendelea kuvaa uzi wa Arsenal wenye rangi nyekundu na nyeupe.
Kama ilivyokuwa kwenye suala la Van Persie, lazima kutakuwa na maoni tofauti kutokana na maneno ya Koscielny juu ya imani yake kuhusu kikosi cha Arsenal.
No comments:
Post a Comment