JIONI ya Jumatatu, Juni 3, ilikuwa siku njema kabisa kwa mabeki wa kushoto kwenye mikikimikiki ya La Liga, wakati Sevilla ilipothibitisha kipenzi cha mashabiki Jesus Navas atahamia Manchester City.
Dili hilo linalomfanya Navas ahame Ramon Sanchez Pizjuan lilielezwa awali kuwa ni euro milioni 21 kabla halijapanda na kuwa euro milioni 25, lakini hilo litatokana na namna mzawa huyo wa Sevilla atakavyoweza kutulia na maisha ya Man City na kufanya mambo.
Hakuna shaka kwamba winga huyo mwenye umri wa miaka 27 amepevuka vya kutosha kwa ajili ya kuhimili mikikimikiki ya Ligi Kuu England na presha ya kuichezea Manchester City. Mkali huyo amewatesa mabeki mbalimbali nchini Hispania na barani Ulaya kwa karibu muongo mmoja sasa, tangu alipoanza rasmi Novemba 2003.
Kila wakati mchezaji huyo mwenye medali ya ushindi wa Kombe la Dunia anapopata mpira anakuwa na kazi moja tu: kumlamba chenga beki wa pembeni na kupiga krosi. Inaweza kuonekana kama ni mtindo wa zamani wa kuichezaji, lakini jambo hilo limemsaidia kuweza kupiga krosi maridadi 51 kwenye mikikimikiki ya La Liga msimu huu, ikiwa ni zaidi ya mchezaji mwingine yeyote.
Zao hilo la akademi ya Sevilla, Navas hatakuwa na mbwembwe za kutaka kuwaonyesha madoido mabeki wa timu pinzani zaidi ya kufanya mashambulizi yenye faida kwa timu yake. Hata alipokuwa bado kinda, mchezaji huyo alipokuwa ndani ya uwanja alikuwa akifanya mambo muhimu tu, kumiliki mpira na kukimbia nao kwa kuwa alikuwa na kasi ambayo ilikuwa rahisi kuwashinda wapinzani wake.
Mashabiki wa Man City watakuwa kwenye burudani ya kutosha kwa kumtazama Navas akiwa anapangwa pamoja na Pablo Zabaleta katika upande wa kulia. Mhispania huyo huwa anakuwa hatari sana pindi anapocheza na beki wa mbele mwenye kiwango kizuri kwa sababu jambo hilo litamfanya kwenda mbele kushambulia na kombinesheni yake na Zabaleta inaweza kuwa na aina yake kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.
Navas na Dani Alves waliunda safu ya aina yake kabisa na yenye kuburudisha kwa upande wa kulia wakati walipokuwa pamoja kwenye kikosi cha Sevilla, kabla ya mchezaji mwenzake huyo kuhamia Barcelona.
Kwa pamoja waliweza kuwanyanyasa baki wa timu pinzani, kwani Alves alipokwenda mbele, Navas aliweza kukava sehemu ya ulinzi na kuifanya Sevilla wakati huo kuwa hatari zaidi barani Ulaya.
Lakini, kwa mambo yote yasiyo na shaka juu ya uwezo wake, kuna kitu kimoja kipo kwenye kichwa cha staa huyo: hali ya kisaikolojia itakayochangiwa na kuhama mji wake wa nyumbani.
Mwaka 2006 alikuwa na mpango wa kuhamia Chelsea, lakini mpango huo ulikwama kutokana na mchezaji huyo kuzoea kuishi kwao na hapo akalazimika kushindwa kung'ara kwenye soka hilo la kimataifa.
Taratibu Navas aliweza kulizoa tatizo hilo na akaweza kujumuishwa katika kikosi cha Hispania katika fainali za Kombe la Dunia 2010 na kuwa sehemu ya ushindi wa kikosi hicho katika michuano hiyo na ile ya Euro 2012.
Bila ya kujali maendeleo ya soka lake tangu 2009, mtaalamu wa masuala ya michezo na saikolojia, Daniel Abrahams, alisema tatizo hilo linalomsumbua mchezaji huyo linaweza kuwa tatizo na tishio kwa maendeleo yake katika kikosi cha Man City.
Kutokana na uchezaji wake, Navas anatarajia kuwa burudani kubwa na kuwa kivutio kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine waliotua kwenye Ligi Kuu England, akiwamo David Silva, Juan Mata na Eden Hazard, ambao wamekuwa na viwango vya aina yake kwa nyota waliotua hapo hivi karibuni. Kutua kwa Navas kwenye kikosi cha Man City, sasa kazi ni kwao mabeki wa kushoto kama Patrice Evra wa Manchester United.
No comments:
Post a Comment