KOCHA Mkuu mpya wa Manchester United, David Moyes, kwa sasa anahusishwa na usajili wa kiungo mwenye kipaji kikubwa wa Barcelona, Thiago Alcantara.
Dau la pauni milioni 17 limetajwa kuwekwa mezani kwa ajili ya kuinasa saini ya Mhispania huyo, Thiago, ambaye anaripotiwa klabu yake ya Barca inahaha na kumpa ahadi tamu ili abaki mahali hapo. Je, dili hilo litakamilika na Thiago akavaa uzi wa United msimu ujao?
Na kama usajili huo ukikamilika, ni wazi kabisa hautakuwa uhamisho mkubwa utakaofanywa na Mashetani Wekundu hao katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.
Pamoja na kwamba dirisha la usajili bado halijafunguliwa, kwenye soko la usajili kuna orodha ya majina makubwa ya wachezaji ambao wapo tayari kabisa kwa ajili ya kunyakuliwa na timu ambazo zitakuwa tayari na kuwa na fedha za kufanya hivyo.
Majina makubwa mawili yanayotikisa sokoni kwa sasa ni Gareth Bale na Cristiano Ronaldo, ambao pia wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kutua Old Trafford.
Gazeti la The Sun la Uingereza hivi karibuni lilidai kwamba United wapo tayari kutumia fedha nyingi na hata kuvunja rekodi ya dunia kwa ajili ya kuwasainisha wachezaji hao, ili kuendeleza zama mpya baada ya kuondoka kwa kocha Alex Ferguson.
Mabosi wa timu hiyo ya United, familia ya Glazers, wapo tayari kumpa fungu kubwa kocha mpya wa timu hiyo, David Moyes, ili kumnasa mmoja kati ya Cristiano Ronaldo au Gareth Bale.
Pauni milioni 85 zimetengwa kumnasa mmoja kati ya masupastaa hao kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki wao, licha ya kwamba hadi sasa bado hakuna uhakika kama kuna staa yeyote hapo atatua Old Trafford msimu ujao.
Dimba linajaribu kufanya uchambuzi baina ya wachezaji hao ni jinsi gani wataweza kuingia kwenye mfumo wa United kama watatua kwenye klabu hiyo katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, huku tukitazama zaidi ni mchezaji gani atakuwa na faida kubwa kuliko mwingine.
Gareth Bale
Kwa kutazama nje, nyota huyo wa Tottenham Hotspur, anaonekana kwamba ataweza kufiti katika mfumo wa United kama atakuwa mchezaji wa klabu hiyo.
Winga huyo wa Wales, Bale, aina ya soka lake linafanana na la mkongwe wa klabu hiyo, Ryan Giggs, ambaye pia aina ya uchezaji wake ulimhamasisha staa wa zamani wa Mashetani hao Wekundu, Cristiano Ronaldo.
United ilijaribu kumsajili Bale wakati alipokuwa akiihama Southampton, lakini kwa kipindi kile walipuuza na kutazama mchezaji ambaye alikuwa na kiwango kikubwa katika safu ya kiungo mshambuliaji ili waipate saini yake.
Wakati United wakimpuuza Bale kipindi hicho, mchezaji huyo ndani ya kikosi cha Spurs ameweza kupandisha kiwango chake cha soka na kuwa moja ya mastaa wanaotetemesha soko la usajili kwa kipindi hiki.
Kwa aina ya uchezaji wake wa sasa, akiwa chini ya kocha Andre Villas-Boas, Bale ameweza kuonyesha kwamba ni tishio kubwa anapocheza kama mshambuliaji wa kati.
Uwepo wake kwenye kikosi cha Spurs, ambacho safu yake ya ushambuliaji imekuwa ikibadilika, lakini kuwapo kwa mchezaji huyo kumeifanya timu hiyo ya Ligi Kuu England kuwa na makali ya aina yake.
Kama ilivyo kwa Ronaldo, Bale ni mchezaji wa muda mrefu, kwamba unaweza kuwekeza kupitia yeye na ukawa kwenye mipango kwa muda mrefu zaidi.
Uwezo wake wa umaliaji ni wa aina yake na kuhesabiwa kuwa mmoja wa washambuliaji ulimwenguni, huku anamiliki pia kiwango kikubwa cha uchezeshaji kitu ambacho kinaweza kumpa nafasi ya kucheza katika klabu yoyote. Je, atafiti kwenye mfumo wa United?
David Moyes anaye Shinji Kagawa, ambaye anatengeneza mfumo wa pembetatu katika safu ya ushambuliaji. Kama watamsainisha Gareth Bale, mchezaji huyo atatumika zaidi katika upande wa kushoto.
Jambo hilo halitakuwa baya sana. Ashley Young, winga chaguo la kwanza kwa sasa katika upande wa kushoto, haonekani kuwa na uwezo wa asili wa kuweza kuwa tishio na kucheza kwa kiwango cha juu kuliko alichonacho kwa sasa.
Hivyo, kuwa na Bale katika upande mmoja wa kiungo, pamoja na mkali Antonio Valencia kwenye upande mwingine, hilo litawaweka kwenye wakati mgumu mabeki wa pembeni wa timu pinzani na hapo United wataweza kuwa na safu hatari zaidi ya ushambuliaji.
Moyes siku zote amekuwa akitumia sana mfumo wa mashambulizi ya kupitia pembeni, na Bale hapo itakuwa kama umerudisha nyumbani vile kutokana na kuuweza vizuri zaidi mfumo huo.
Cristiano Ronaldo
Huyu ni kijana wa aina yake, mchezaji ambaye daima atakumbukwa kama gwiji la Old Trafford.
Kumekuwa na imani kwamba Mreno huyo anatumia uvumi uliopo kwamba anataka kurudi United ili kuifanya Real Madrid kutoa fedha nyingi kumbakiza, lakini ukweli halisi mchezaji huyo anaonekana wazi kabisa ana mapenzi na klabu yake ya zamani.
Ronaldo si mchezaji tofauti sana na yule aliyehama United mwaka 2009, kwa sasa amezidi ubora wake zaidi. Kama uhamisho huo utakamilika, hakuna shaka kwamba ataendelea kutumika kama winga, ambayo ni nafasi yake ya asili.
Kutokana na kuwa na mshambuliaji Robin van Persie kwenye kikosi chao cha kwanza, Mdachi huyo anatazamwa wazi atakuwa sehemu muhimu ya kucheza kama mshambuliaji wa kati katika kikosi hicho cha Moyes.
Lakini, kama Ronaldo atahamia United, ni wazi kabisa mabadiliko ya kiufundi yatatokea katika kikosi hicho cha Old Trafford. Kikosi hicho kitalazimika kucheza fomesheni ya 4-3-3, mfumo ambao aliutumia Sir Alex wakati ananyakua taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya 2008.
Kutumia mfumo wa kubadilisha washambuliaji, kwa safu ya wachezaji watatu mbele, Ronaldo, Van Persie na mchezaji mwingine, ambaye anaweza kuwa Valencia au usajili mpya Wilfried Zaha au hata Wayne Rooney, utaifanya United kuwa moto zaidi.
Ronaldo atapewa nafasi pia ya kuzunguka uwanja mzima kutafuta mipira. Na kwenye hilo, United haitaweza kutumia mfumo wa 4-2-3-1 kwa sababu jambo hilo litaacha nafasi kwenye kikosi, hasa kwa upande wa wachezaji wa pembeni, Patrice Evra au Rafael.
Kama Moyes atamsainisha mchezaji kama Ronaldo, ni wazi kabisa kikosi hicho kitalazimika kubadilika. Jambo hilo halina maana kwamba mchezaji huyo ana hadhi kubwa kuliko klabu, hapana, bali ni katika kutafuta namna nzuri ya kupata huduma bora ya mchezaji husika. Ronaldo, hupaswi kumuweka tu mwenyewe kwenye wingi.
Hitimisho
Litakapokuja suala la mchezaji gani hapo atakuwa na faida kubwa kwa United kuliko mwingine kati ya Bale na Ronaldo, ni jambo ambalo litakuwa gumu kulipata jibu lake kirahisi.
Lakini, usajili wa mmoja wa wachezaji hao utaifanya timu kuwa imara na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa ligi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa miaka kadha ijayo.
Kwa David Moyes, hapa anapaswa kupasua kichwa kama ataamua kufanya kweli kwa kunasa saini ya mmoja wa wakali hao. Kama United itamchukua Bale utakuwa usajili mzuri, lakini kama atakuwa Ronaldo, basi ni wazi kabisa jambo hilo linaweza kuwatoa machozi mashabiki wa United kutokana na kurejea kwa shujaa wao.
Nani ataweza kufiti vizuri kwenye kikosi cha United, Bale au Ronaldo?
No comments:
Post a Comment