LONDON, England
AMSHA amsha za usajili zimeanza Ulaya, kila timu
inatafuta mchezaji kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake au kuziba mapengo
yaliyoachwa wazi.
Julai 1 dirisha la usajili la majira ya kiangazi
linafunguliwa rasmi na tayari Neymar, Radamel Falcao na Wilfried Zaha
wamekamilisha usajili, lakini vipi kwa wale ambao bado?
LENZI YA MICHEZO inakuletea wachezaji 10 wanaowaniwa zaidi
kwenye dirisha la usajili la Kiangazi.
Isco
(Malaga na Hispania)
Anatarajiwa kumfuata Manuel Pellegrini, Etihad baada
ya misimu miwili Malaga, Isco, ni kiungo mshambuliaji anaungana na watu
wanaocheza kama yeye, Samir Nasri na David Silva. Ana uwezo mkubwa sana wa
kupita mabeki, lakini swali ni je, atasalimika kwenye soka la nguvu la England?
Hilo tunasubiri kuona, atawabeba sana Manchester City kwenye Ligi ya Mabingwa
Ulaya.
Thamani:
Pauni milioni 27
Wanaomtaka:
Manchester City
Wayne
Rooney (Manchester United na England)
Mustakabali wa Rooney Manchester United ni utata
mtupu, kwa sasa yuko kwenye mazungumzo na kocha mpya wa Old Trafford, David
Moyes. Kama Rooney ataondoka basi klabu kibao zitamtolea macho na vita itaanzia
hapo. Hata hivyo, hamu ya Rooney kuondokana na presha na kuelekeza nguvu zake
kwenye soka ni muhimu sana.
Thamani:
Pauni milioni 30
Wanaomtaka:
Manchester
City, Chelsea, Arsenal, PSG, Real Madrid
Cesc
Fabregas (Barcelona na Hispania)
Ndoto aliyokuwa nayo Fabregas ya kurudi Barcelona na
kufanikiwa miaka miwili iliyopita, haijatimia, msimu huu amecheza mechi 32 na
kufunga mabao 11 na kutengeneza mengine 11, kitu ambacho siyo kibaya kwa
nahodha huyo wa Arsenal. Mashabiki wa England wanajua uwezo wa Mhispaniola
huyo, lakini klabu za Manchester City na Manchester United zinaweza kuwa
zimefedheheshwa na hamu ya Fabregas kuendelea kubaki Nou Camp wakati huu wa
Kiangazi.
Thamani: Pauni milioni 35
Wanaomtaka:
Manchester City, Manchester United
Gareth
Bale (Tottenham Hotspur na Wales)
Staa huyo wa Wales ndiye bidhaa adimu zaidi kwenye
ulimwengu wa soka la Ulaya na kwa sasa anaweza kuzua vita ya klabu nyingi
kumtaka. Anawaniwa sana na Manchester United ili kuziba pengo ambalo liliachwa
wazi na Cristiano Ronaldo mwaka 2009. Lakini Real Madrid ndio wanazungumza sana
kuhusu winga huyo mzaliwa na Cardiff. Pamoja na hamu kubwa ya Andre Villas-Boas
kumbakiza, usajili wa fedha nyingi utakuwa mzuri kwake.
Thamani:
Pauni
milioni 80
Wanaomtaka:
Real
Madrid, Chelsea, Manchester City, Manchester United
Luis
Suarez (Liverpool na Uruguay)
Mtata huyu wa Uruguay anaweza kuwa mmoja kati ya
wachezaji wenye vipaji sana duniani, lakini Liverpool wanaweza kumruhusu
aondoke kwa dau la pauni milioni 40. Suarez amekuwa akiwaambia wanahabari wa
nchini mwake kuwa watu wanamuonea sana England. Lakini kashfa za kumbagua
Patrice Evra na kumng’ata Branislav Ivanovic kumeharibu uhusiano wake na
mashabiki wa Liverpool.
Thamani:
Pauni
milioni 40
Wanaomtaka:
Real
Madrid, Atletico Madrid, Juventus, PSG
Edinson
Cavani (Napoli na Uruguay)
Kwa msimu wa pili mfululizo, Cavani amekuwa
akihusishwa na kuondoka Napoli, staa huyo mwenye miaka 26 msimu uliopita
alifunga mabao 40 akiwa na klabu yake na timu ya taifa na yupo kwenye mipango
ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao ya Napoli, lakini kuondoka kwa Ezequiel Lavezzi
kwenda PSG mwaka jana, kulimkera Cavani. Kama Edin Dzeko akifanikiwa
kulazimisha kuhama Manchester City, basi Cavani anaweza kuondoka.
Thamani:
Pauni
milioni 54
Wanaomtaka:
Manchester
City, PSG, Chelsea
Leighton
Baines (Everton na England)
Wakati kiwango cha Patrice Evra kikionekana
kuporomoka kila kukicha na ujio wa David Moyes, Old Trafford mtu huwezi kukosea
ukimuhusisha Leighton Baines kujiunga na Manchester United. Baines amekuwa
kwenye kiwango cha hali ya juu katika misimu miwili iliyopita na amekuwa muhimu
kwa Everton, japokuwa beki huyo wa kushoto mwenye umri wa miaka 28, haendani na
mfumo wa Man United wa kusajili wachezaji wenye umri chini ya miaka 26, lakini
atakuwa na faida sana kwao kama akisajiliwa.
Thamani:
Pauni
milioni 15
Wanaomtaka:
Manchester
United
Christian
Benteke (Aston Villa na Ubelgiji)
Mabao yake 19, yameibakisha Aston Villa kwenye Ligi
Kuu England na yalitosha kuzivutia klabu kadhaa kubwa. Benteke (22) mwenye
uwezo wa kupiga vichwa, mashuti na kucheza peke yake mbele, vinamfanya kuwa mtu
muhimu kwa Ubelgiji kuelekea kwenye Kombe la Dunia mwakani na sasa hivi
mchezaji huyo anahitaji kupata mechi zenye ushindani zaidi, ili abaki kwenye
fomu itakayombeba mwakani nchini Brazil.
Thamani:
Pauni
milioni 17.5
Wanaomtaka:
Atletico
Madrid, Tottenham, Liverpool
David
Luiz (Chelsea na Brazil)
Tatizo kubwa la Luiz chini ya Jose Mourinho, itakuwa
kuendana na mfumo wake, Mbrazil huyo amekuwa na msimu mzuri sana na kama
Mourinho atamuachia itatokana na aina yake ya uchezaji na siyo uwezo. Uwezo
wake wa kukaba umekuwa ukizua maswali tangu alipojiunga na Chelsea kutoka
Benfica mwaka 2011, lakini anaweza kufaa kwenye mfumo wa Barcelona.
Thamani:
Pauni
milioni 35
Wanaomtaka:
Barcelona,
Napoli
Wesley
Sneijder (Galatasaray na Uholanzi)
Kipara chake kinawafanya watu kusahau kuwa Sneijder
ndiyo kwanza anaumri wa miaka 28 na bado ni mmoja kati ya viungo washambuliaji
bora zaidi duniani. Kiwango chake akiwa na Galatasaray kwenye Ligi ya Mabingwa
Ulaya, vilithibitisha kuwa bado anaweza kutawala kiungo na Jose Mourinho anajua
ubora wake baada ya kufanya naye kazi alipokuwa Inter Milan.
Thamani:
Pauni
milioni 7
Wanaomtaka:
Chelsea
No comments:
Post a Comment