NILETEENI Yanga muone kazi yangu! Hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah ‘King’ Kibadeni, kusema vijana wake wameiva kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba
katika msimu uliopita ilipokea kipigo cha mabao 2-0, katika mchezo wa marudiano
wa Ligi Kuu uliochezwa Mei 18, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, ikiwa chini ya Kocha Mkuu wake, Mfaransa, Patrick Liewig.
Lakini
Kibadeni ameanza kujiamini mapema kuwa kikosi chake kinaweza kubadilisha
matokeo ya msimu uliopita, baada ya kujiridhisha vijana wake wameiva kwa ajili
ya ligi hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kibadeni
alisema kutokana na uwezo uliooneshwa na vijana wake kwa takribani mwezi mmoja katika mazoezi
yanayoendelea kwenye Uwanja wa Kinesi, hana shaka kabisa ya kuanza kwa ligi
hiyo.
Kibadeni
alisema vijana wake wapo tayari kucheza, ingawa anaendelea na mazoezi makali ya
kuwajengea nguvu ya mwili katika Gym ya
Chang’ombe na baadaye mazoezi ya kawaida Uwanja wa Kinesi.
Kibadeni
alisema anajivunia timu hiyo, kwani inaundwa na wachezaji wengi chipukizi licha
ya kuwemo wengine wakongwe kama Nassor Masoud ‘Chollo’, Mwinyi Kazimoto, Amri
Kiemba, Musa Mude, Abel Dhaira na Haruna Shamte.
Alisema
hana hofu kabisa kuhusu kutemwa kwa kipa na nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja
kwa kuwa anao makipa watatu katika kikosi chake, akiwemo Andrew Ntalla
aliyesajili msimu huu, akitokea Kagera Sugar.
Kikosi
kipya cha timu hiyo kinaundwa na wachezaji
Zahor Pazi, aliyesajiliwa kutoka (Azam FC), ambaye msimu uliopita
alikuwa akicheza kwa mkopo katika klabu ya Ruvu Shooting na Augustino Sino
(Tanzania Prisons).
Wengine
ni Kipa Andrew Ntalla (Kagera Sugar), Samuel Ssenkoom (URA ya Uganda), Adeyoon
Salehe (Miembeni ya Zanzibar), Ibrahim Twaha ‘Neymar’ (Coastal Union) na Issa
Rashid ‘Baba Ubaya’ (Mtibwa Sugar).
Kadhalika
wamo, Shomari Kapombe, Kiemba, Kazimoto, Chollo, Salum Kinje, Haruna Shamte,
Mude na Dhaira huku akiwapandisha wachezaji wengi wa kikosi cha pili cha timu
hiyo, Miraji Adam, Hassan Khatib, Willian Lucas, Daid Ndemla, Abdallah Seseme,
Hassan Isihaka, Marcel Kahenza, Ramadhan Singano ‘Messi’, Haruna Chanongo,
Jonas Mkude, Christopher Edward, ambao baadhi yao walipandishwa katika misimu
miwili iliyopita.
No comments:
Post a Comment