NEYMAR (21), ametua rasmi Barcelona wiki hii, kinda huyo
amekuwa akitawala vyombo vya habari na kugombaniwa na klabu nyingi tangu
alipoanza kuvuma akiwa na Santos mwaka 2009.
Uvumi wa kila aina ulitawala sakata lake la usajili, huku
dunia ikijaribu kutabiri iwapo Neymar ataondoka nyumbani kwao Brazil kabla ya
Kombe la Dunia 2014.
Sasa hivi ametua rasmi Camp Nou, swali linakuja je, lini Barcelona
walianza kuwania saini ya Neymar? Je, ni kweli kuwa Barcelona walimsajili miaka
miwili iliyopita? Kwa nini amechagua Camp Nou?
Makala haya yanaangalia safari ya Neymar hadi alipotua Barcelona.
Akiwa na miaka
13 alifanya majaribio Real Madrid
Neymar amekuwa akizivutia timu kubwa barani Ulaya kwa muda
mrefu sasa, akiwa na miaka 13 aliwahi kufanya majaribio na Real Madrid.
Baba yake Neymar alisema kwamba, mwanaye alialikwa Real Madrid
na kila kitu kilikuwa poa, lakini inasemekana matatizo ya kimkataba yalimzuia
Neymar kutua Santiago Bernabeu.
Kushindwa kwa Madrid ni faida kwa Barca miaka kadhaa mbele.
Mechi ya
kwanza Santos
Mwaka 2009, Neymar alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Santos,
kwenye michuano ya Brasileirao, wiki moja baadaye alifunga bao dhidi ya Mogi
Mirim.
Neymar alifunga mabao 13 kwenye msimu wake wa kwanza na Santos
akiwa na miaka 17 tu. Neymar alithibitisha kuwa ni moto wa kuotea mbali kila
alipoingia uwanjani.
Watu walianza kumtabiria makubwa kwenye msimu wake wa kwanza
Santos.
Ubingwa Santos,
England wamtolea macho
Neymar alifunga mabao 17 kwenye mechi 31 za michuano ya Campeonato
Brasileirao akiwa na Santos mwaka 2010, mabao yake yalichangia kuipa Santos
Ubingwa wa Jimbo la Sao Paulo.
Pia Neymar alipewa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano. Hii
ilizivutia timu za Ligi Kuu England, huku akipewa jina la The New Pele (Pele
Mpya).
Kuliibuka uvumi kwamba, Neymar alitosa kujiunga na West Ham
kwa ada ya pauni milioni 16, pia klabu kama Manchester City na Chelsea, nazo
zilitajwa kuwania saini ya kinda huyo.
Kubaki na
kupanda akiwa Santos
Mwaka 2010, Neymar alisaini mkataba mpya wa miaka mitano
kuendelea kubaki Santos na kukataa kujiunga na Chelsea iliyokuwa tayari kuweka
mezani dau kubwa.
Neymar alisema kwamba, fedha hazileti furaha na kusisitiza
kuwa alikuwa na furaha kwenye klabu yake na alitaka hali iendelee kuwa hivyo,
pamoja na kwamba uamuzi huo ulikuwa mgumu sana kwake.
Uamuzi wa Neymar kubaki Vila Belmiro akiwa na Santos, ulikuwa
mzuri kwa klabu baada ya kushinda michuano ya Copa Libertadores mwaka 2011.
Hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kunyakuwa taji
hilo, tangu mwaka 1963 na ubingwa huo uliipa Santos nafasi ya kushiriki
michuano ya Kombe la Dunia la Vilabu, fainali ya michuano hii ilizikutanisha Barcelona
na Santos na hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Barca kukutana na Neymar.
Kombe la
Dunia la Klabu: Santos vs Barcelona
Mwaka 2011, jina la Neymar lilitajwa kati ya majina 23 ya
wachezaji waliokuwa wakiwania tuzo ya Ballon d’Or.
Lionel Messi pia alikuwa kwenye orodha hiyo, hivyo fainali ya
Kombe la Dunia la Klabu, kati ya Santos na Barcelona ilipewa jina la vita kati
ya Messi na Neymar.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Messi na Neymar kucheza kiwanja
kimoja na Barca walishinda kwa mabao 4-0, jijini Yokohama, inasemekana Neymar alimwomba
Pep Guardiola amsajili, baada ya mechi hiyo kuisha.
Wengi walitaja mechi hii kama mwanzo wa majadiliano kati ya Barcelona
na Santos, inasemekana kuwa Barca walitoa kiasi cha euro milioni 10 kama malipo
ya awali mwaka 2011, ili kumsajili rasmi Neymar mwaka 2014.
Uvumi
washamiri
Licha ya mkataba kumbakisha Santos hadi mwaka 2015, huku
kipengele cha kumruhusu kuondoka kikiwa ni euro milioni 45, miamba mikubwa
barani Ulaya haikukata tamaa kwenye mbio za kumsajili.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Barca walikuwa wakimfuatilia
kwa karibu pamoja na timu nyingine nne kubwa za bara hilo, ikiwemo Juventus.
Kiwango cha Neymar kwenye michuano ya Olimpiki 2012 jijini
London, kilizidi kumpandisha chati, alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa
Amerika Kusini, mwaka 2012.
Alikuwa kwenye tatu bora ya tuzo ya Ferenc Puskas, huku
akifunga mabao 14 kwenye Ligi ya nyumbani akiwa na Santos.
2013 – Atua
Barcelona
2013 ndio mwaka Barcelona walimpata mtu wao, baada ya miaka
kibao ya kumfukuzia. Real Madrid waliibuka na kutaka kuwazidi kete, Barca kwa
ajili ya saini yake wakiweka mezani dau ambalo lilikuwa mara mbili ya lile la
Barcelona.
Lakini Neymar alichagua kujiunga na Barcelona, akitoboa juu ya
kutua kwake Barca kupitia akaunti yake ya Instagram, mwisho wa wiki iliyopita.
Barcelona walithibitisha kwamba, Neymar amesaini mkataba wa
miaka mitano Jumatatu kupitia mtandao wa klabu hiyo fcbarcelona.com.
Sababu ya Neymar kutua Camp Nou ni za kimichezo zaidi kuliko
fedha, hii ni kwa mujibu wa kocha wa Barca Tito Vilanova.
Watu wanasubiri kuona kama Neymar ataweza kufanya vizuri
barani Ulaya, hasa akicheza sambamba na watu kama Xavi Hernandez, Andres Iniesta
na Messi.
No comments:
Post a Comment