NI miaka miwili tu imepita tangu Cesc Fabregas (26), alipoondoka
London na kurudi nyumbani Barcelona, kwenye uhamisho ambao ulionekana kama
hauwezi kukamilika.
Kwa wali ambao wameanza kupenda soka juzi, Fabregas aliondoka Barcelona
na kutua Arsenal wakati wa kiangazi mwaka 2003 akiwa na miaka 16, kabla ya kurudi
nyumbani msimu wa 2011-12.
Arsenal na Arsene Wenger wanachukulia kumuuza Fabregas kwenda Barcelona
kama biashara tamu yenye chungu ndani yake. Wenger, Klabu na Mashabiki
walimshuhudia Kinda wa miaka 16 waliyemnunua kwa euro milioni 3, akiwa nahodha wa
timu hiyo katika umri wa miaka 24.
Hatimaye walimuuza Barcelona kwa ada ya euro milioni 34, baada
ya vuta nikuvute kwa misimu mitatu ya usajili.
Mashabiki wengi wa Arsenal walisahau juu ya uhamisho wa Fabregas
kwenda Barca. Wanasema kuwa kilikuwa kipindi cha kipekee, Cesc alikuwa akirudi
nyumbani kuungana na wachezaji wenzake aliocheza nao utotoni, kina Gerard
Pique, Lionel Messi na wengine wengi.
Pia alikuwa akiungana
na shujaa wake alipokuwa mtoto Pep Guardiola, Guardiola alikuwa ametengeneza
bonge la timu, haikuwa rahisi kwa mashabiki wa Arsenal kukubaliana na uhamisho
huo lakini ukweli ni kuwa Fabrigas alipata nafasi ambayo ilikuwa ngumu
kuikataa.
Maisha yaliendelea London Kaskazini, japokuwa kuziba nafasi ya
Fabrigas ilikuwa ngumu, Santi Cazorla ameleta kitu fulani cha Kihispaniola
kwenye kiungo cha Arsenal.
Baadhi ya mashabiki wa Arsenal bado wanafuatilia maendeleo ya Fabregas,
akiwa Barca. Vyombo vya habari vimekuwa vikiifuatilia sana Barcelona na ukweli
kwamba mchezaji wa zamani wa Ligi Kuu England hana furaha kwenye moja ya timu
bora duniani unazua maswali: Je, Fabregas yuko njiani kusepa?
Watu wanaanza kukumbuka mengi sana, matumaini, kuumizwa,
kujiamini na hofu. Je, ni kweli Fabregas ataondoka Barcelona? Ni kweli Cesc ni
moja kati ya viungo bora duniani. Hakuna mwenye kubisha juu ya hilo. Bahati
mbaya kwake kwa sasa kuna Xavi Hernandez na Andres Iniesta.
Ujio wa Fabregas, Barcelona ulimaanisha kuwa mabadiliko kwenye
kikosi cha timu hiyo, yaani Xavi alitakiwa kumpa kijiti Fabregas, lakini cha kushangaza
ndio kwanza kiwango cha Xavi kinazidi kupanda na hii imemnyima nafasi Cesc ya
kung’ara.
Inawezekana Fabregas akawa anafikiria kwamba, anatakiwa
kusubiri na kufanya mazoezi mengi basi na yeye wakati wake utafika. Mpango huo
ulikuwa mzuri mpaka wiki hii, Barca walipotangaza kumsajili Neymar, usajili huu
umeharibu dili lake.
Mashabiki wa Arsenal wanashangilia! Hii inatokana na taarifa
kwamba, kuna kipengele ambacho kipo kwenye mkataba wa Fabregas alipohamia Barca,
ambacho kinasema kwamba The Gunners wapewe nafasi ya kwanza kama mchezaji huyo
atataka kurudi England.
Wenger anaamini ipo siku Fabregas atarudi Emirates, kwa sababu
mchezaji huyo anaipenda Arsenal kutoka moyoni mwake.
Swali je, kweli anaweza kurudi kwenye timu ambayo haijatwaa
taji lolote kwa miaka 8? Robin Van Persie alikuwa nahodha wa Arsenal mpaka
alipoamua kuhamia Manchester United alipopata taji.
Uamuzi wa RVP kuitema Arsenal na kutua Man United, ulitoa
ujumbe tosha kwamba alikuwa akitaka makombe na kweli alishinda taji miezi 10,
baada ya kuitema Arsenal. Kiukweli wachezaji kibao wameshinda ubingwa tangu
walipohama Arsenal. Samir Nasri, Cesc Fabregas, Ashley Cole, Kolo Toure na Robin
Van Persie ni baadhi ya wachezaji waliobeba taji baada ya kuondoka Emirates.
Wiki hii Fabregas amehusishwa na Manchester United. David
Moyes anataka kufikisha ujumbe kwa mashabiki wa Man United kwa kufanya usajili
mkubwa na njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kumleta nahodha wa zamani wa Arsenal.
Fabregas ameshatwaa taji la Euro mara mbili, Kombe la Dunia
mara moja, La Liga mara moja na Kombe la FA akiwa na Arsenal mwaka 2005. Kariba
yake ya kupenda ushindani haiwezi kumruhusu kuendelea kusugua benchi Barcelona,
kariba yake ya ushindani itampeleka sehemu atakayopata mataji zaidi.
Kuna ukweli kuhusu nia ya Moyes kumtaka Fabregas. Kocha huyo
mpya wa Man United anahitaji kuimarisha sehemu ambazo zitaathiriwa na kuondoka
kwa Paul Scholes.
Anderson naye anaonekana yuko njiani, Nani pia, mchanganyiko
wa vijana na wazoefu huku Tom Cleverley na Michael Carrick wakiwa vizuri,
itakuwa jambo zuri kwake kuongeza kiungo mwenye uwezo kama wa Fabregas usajili
huu utaipeleka Man United levo nyingine.
Haijalishi Fabregas anaipenda Man United ama la, kitu kimoja
kiko wazi mashabiki wa Arsenal wanatakiwa kusubiri sakata jingine ambalo
litamshuhudia nahodha wao wa zamani akitua kwenye klabu nyingine.
No comments:
Post a Comment